loader
Dstv Habarileo  Mobile
Misikiti, makanisa kupunguza muda wa ibada

Misikiti, makanisa kupunguza muda wa ibada

VIONGOZI wakuu wa dini nchini wamekubaliana kupunguza muda wa ibada katika makanisa na misikiti ili kuepuka hatari ya kusambaa kwa virusi vya corona.

Walitoa msimamo huo jana mjini Moshi katika Mkoa wa Kilimanjaro wakati wa kikao cha kuweka mikakati ya pamoja kukabili wimbi la tatu la maambukizi ya virusi hivyo.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Fredrick Shoo alisema kwenye mkutano huo kuwa, walikutana ili kupanga mikakati ya kukabili wimbi la tatu la maambukizi ya corona.

"Tumeweka mikakati mingi ikiwemo kupunguza muda wa ibada na katika hili tunaishauri serikali tushirikiane kuendelea kutoa elimu," alisema Dk Shoo.

Alisema mikusanyiko katika nyumba za ibada inaweza kuwa sehemu ya kusababisha maambukizi hivyo wamekubaliana wachukue tahadhari.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristu Tanzania (CCT), Moses Matonya, alisema suala la utoaji wa huduma za kiimani katika makanisa unaweza kuchangia maambukizi usipofanywa kwa umakani zaidi, hivyo zitaendelea kwa kuzingatia tahadhari.

Alisema: "Kuna kushiriki Meza ya Bwana au sakramenti, kuozesha ndoa, mazishi na mambo mengine mengi mambo haya yataendelea kutolewa kwa kufuata kanuni na ushauri wa wataalamu wa afya ili kukwepa maambukizi zaidi."

Naye Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Nuhu Jabir Mruma, alisema Waislamu wamekubaliana kusitisha baadhi ya taratibu za kufanya ibada ili kupunguza maambukizi.

Alisema: “Viongozi wa dini tunalo jukumu kubwa la kuhakikisha nyumba zetu za ibada haziwi sehemu ya maambukizi. Kwa mfano, sisi Waislamu kuna ibada za suna ambazo ukifanya unapata thawabu zaidi na ukiacha hupati dhambi na ikiwa zinaathari, tumeamua kuziacha kama kutoa hutoba ndefu na namna ya ukaaji msikitini tumebadilisha."

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/74ecd888fc965d2a4aa0e2d4fab3d8ce.jpg

MKUU wa Chuo cha Uhasibu Arusha ...

foto
Mwandishi: Deus Ngowi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi