loader
Dstv Habarileo  Mobile
Bunge labadili umri wa mtoto bima ya afya

Bunge labadili umri wa mtoto bima ya afya

BUNGE limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ya Mwaka 2021 ikiwemo Sheria ya Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) inayobadili umri wa mtoto kufikia miaka 21.

Sheria nyingine zilizorekebishwa ni Sheria ya Madini inayolenga kuimarisha mfumo wa Serikali kusimamia hisa zake na Sheria ya Bohari ya Dawa, Sura ya 70 ili kuwezesha Idara ya Bohari ya Dawa kuzalishaji wa dawa ili kuboresha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, mitambo na uchunguzi katika shughuli za afya.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Adelardus Kilangi alisema bungeni Dodoma jana kuwa, muswada huo unapendekeza marekebisho katika sheria 13.

Dk Kilangi alisema kuhusu marekebisho katika Sheria ya Mfuko wa Bima ya Afya, Sura 395, Kifungu cha 3 kinarekebisha tafsiri ya msamiati wa "mtoto" ili kuongeza umri wa mtoto kutoka miaka 18  hadi miaka 21 ili kuongeza muda wa mtoto kuendelea kunufaika na huduma za bima ya afya zitolewazo na NHIF.

Alisema marekebisho yamefanyika katika Kifungu cha 25 ili kuweka utaratibu ambao fedha zote zinazolipwa na mfuko kwa vituo vya umma vya kutolea huduma za afya zitaingizwa moja kwa moja katika akaunti ya vituo hivyo ili kuwezesha matumizi sahihi ya fedha zake na kuwezesha kutimiza wajibu wake wa kifedha kwa wakati. 

"Pia marekebisho ya Kifungu cha 27 kuboresha utaratibu wa ufuatiliaji wa vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya vilivyoingia makubaliano na NHIF kutoa huduma," alisema. 

Alisema pia yamefanyika marekebisho Sheria ya Madini, Sura ya 123 ili kurekebisha Kifungu cha 10 kwa kuongeza Kifungu Kidogo cha (4) ili kuimarisha mfumo wa ushiriki wa Serikali kusimamia hisa za serikali zinazotolewa na kampuni za madini yanayomiliki leseni kubwa na za kati.

"Marekebisho yanakusudia kutambua kisheria utaratibu ambao umekuwa ukitumiwa na serikali wa kushiriki moja kwa moja shughuli za uendeshaji wa kampuni ambazo Serikali inamiliki hisa asilimia 16 kwa mujibu wa Kifungu cha 10 cha Sheria hiyo ili kulinda maslahi ya serikali," alisema.

Alisema Kifungu cha 18(4) kinarekebishwa kwa kuongeza adhabu chini ya kifungu hicho kwa lengo la kudhibiti ukiukwaji. 

Kifungu cha 83 kinarekebishwa ili kutambua, katika leseni ya madalali wa madini, haki ya madalali kununua madini ya ujenzi na madini ya viwandani ili kukuza biashara ya madini na ongezeko la mapato ya Serikali. 

Dk Kilangi alisema marekebisho ya Muswada ya Sheria ya Bohari ya Dawa, Sura ya 70 yamelenga kuiwezesha Idara ya Bohari ya Dawa kufanya uzalishaji wa dawa ili kuboresha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, mitambo na uchunguzi katika shughuli za afya. 

Aidha, Kilangi alisema marekebisho katika Sheria ya Uratibu wa Ajira za Wageni, Sura ya 436 yamelenga kuhakikisha  utaratibu wa utoaji wa vibali vya kufanya kazi kwa wageni nchini unaboreshwa ili kuwafanya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia wajuzi wa kigeni ambao huacha ujuzi nchini.  

“Kifungu cha 12 kinaongeza muda wa mfanyakazi wa kigeni kufanya kazi nchini kutoka miaka mitano ya sasa hadi miaka nane akiwa na uwezo wa kuhuisha maombi ya kibali hicho kila baada ya miezi 24,” alisema. 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/32aa21abfb9422104ec1a3d019ed1002.jpeg

MKUU wa Chuo cha Uhasibu Arusha ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi