loader
MWADHAMA POLYCARP KARDINALI PENGO:  Miaka 50 ya Upadri, safari yenye utukufu na giza nene

MWADHAMA POLYCARP KARDINALI PENGO: Miaka 50 ya Upadri, safari yenye utukufu na giza nene

 

*Kiongozi wa kwanza wa dini kupewa cheti na Rais Samia

*Amejiandalia kaburi eneo la kanisa Pugu

 

WAKATI alipozaliwa mwaka 1944 wilayani Sumbawanga, mkoani Rukwa, pengine wazazi wake hawakujua kama mtoto huyu wa kiume angekuwa kiongozi mkubwa wa kiroho aliyejaa unyenyekevu na uvumilivu na moyo wa kuwatumikia watu.

Safari ya maisha yake, imejaa simulizi za kufurahisha na kuhuzunisha pia, zinazotia moyo na kumuongeza mtu tumaini na majawabu ya maswali mengi ambayo mtu angeweza kujiuliza maishani.

Historia ya maisha yake imeandikwa na imesomwa sana, lakini leo kilichonisukuma kumuandika gazetini ni jubilee ya miaka 50 ya upadri iliyodhihirisha hakuwa kiongozi wa Wakristo pekee bali amegusa watu wa kawaida na kusaidia kutoa ufumbuzi wa migogoro katika jamii.

Ukimsikiliza akizungumza huwezi kujua kama anaweza kukemea mtu au kukasirika. Lakini waliofanya nae kazi wanamuelezea kuwa ni zaidi ya kiongozi, baba, mlezi, mshauri anayejua kuisoma saikolojia ya mtu na kumpa maelekezo yanayokidhi matamanio yake bila kumkosea Mungu.

Rais Samia amtunuku cheti

Safari hiyo ya maisha yake na uongozi wake uliotukuka ndio sababu iliyomfanya Rais Samia Suluhu Hassan kwa mara ya kwanza kumtunuku cheti cha shukrani cha uongozi uliotukuka kutambua mchango wake kwa serikali na kwa Watanzania.

Sina takwimu kamili lakini nina uhakika kwamba cheti hicho ni cha kwanza kutolewa na Samia kwa kiongozi wa dini namna hii tangu kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania Machi 19 mwaka huu.

Akiwa na umri wa miaka 27 tu, Juni 20 mwaka 1971, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, alipewa Daraja Takatifu la Upadri hivyo Juni 20 mwaka huu alifanya ibada ya shukrani ya Misa Takatifu kwa kufikisha miaka 50 ya upadri.

Ni katika ibada hiyo iliyofanyika katika Viwanja vya Kanisa la Msimbazi, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Rais Samia kupitia Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, alimkabidhi cheti cha shukrani Askofu huyo Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwa kutambua mchango wake wa utumishi uliotukuka katika miaka hiyo 50 ya upadri.

Samia alimuomba aendelee kuwaombea viongozi wa serikali ili waongoze kwa haki na hekima ya Mungu. Katika ibada hiyo pia Rais Samia alimkabidhi Kardinali Pengo fedha taslimu (hazikutajwa kiasi) ili kuendeleza ujenzi wa Kanisa la Makurunge lililopo Bagamoyo aliyouanza kabla hajastaafu kuliongoza Jimbo Kuu la Dar es Salaam mwaka 2019.

“Umeliunganisha Kanisa na serikali, umekemea uovu bila woga. Watumishi wa serikali tuna mengi ya kujifunza kutoka kwako, kwanza uvumilivu na kujitoa huku ukitekeleza majukumu yako ukiamini neema ya Mungu yatosha,” alisema Dk Mpango akiwasilisha salamu za Rais Samia.

Alisema serikali inatambua mchango wa Kardinali Pengo katika usuluhishi wa migogoro na huduma za kijamii na yeye (Dk Mpango) pamoja na Rais Samia wanamuomba aendelee kuwaombea viongozi wa serikali wapate roho ya hekima katika kuliongoza taifa kwa amani na utulivu.

“Naleta salamu za Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa jubilei hii. Rais anakuombea afya njema, amewaomba viongozi wa dini mtuombee sisi viongozi wa serikali tuongoze vyema na kuwataka Watanzania muendelee kuwa watulivu na kuijenga nchi yetu,” alisema Dk Mpango.

Dk Mpango alisema kwa kutambua mchango wake kwa taifa na utumishi uliotukuka kwa miaka yote 50 ya upadri wake, Rais Samia amemtunukia cheti cha shukrani na kumpa fedha kidogo kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Kanisa la Makurunge, Bagamoyo aliyoanzisha Kardinali Pengo kabla hajastaafu.

Kwa upande wake Dk Mpango na familia yake walimkabidhi Kardinali Pengo Moistransi (chombo) ya kuabudu Yesu wa Ekaristi.

Sifa alizotoa Dk Mpango kwa Kardinali Pengo si za kumvika mtu kilemba cha ukoka bali ni za kweli kabisa. Alisema Pengo ni kiongozi wa mfano ambaye katika miaka hiyo 50 ya utume wake wa upadri amevumilia mapito mengi ikiwamo vipigo, kufunga mara kwa mara, tabu na kukesha mara nyingi kama linavyosema neno alilolinukuu kutoka katika Biblia Takatifu, Kitabu cha 2Wakorintho 3.

Aliyoyafanya kwa Kanisa

Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mbeya, Gervas Nyaisonga, akitoa salamu za baraza hilo, alisema Kardinali Pengo amelifanyia mengi baraza hilo na kumpongeza kwa utume wake wakati wote wa dhoruba na furaha.

“Umefanya utume uliogusa mtu mmoja mmoja na jumuiya mbalimbali, sisi TEC umetufanyia mengi. Tunakutakia matashi mem ana masiha yenye furaha na amani, tutaendelea kukuombea,” alisema Askofu Mkuu Nyaisonga.

Waumini wa kanisa hilo Jimbo Kuu la Dar es Salaam wana mengi ya kumkumbuka Kardinali Pengo. Miongoni mwa mambo hayo yanayoacha alama kubwa ya imani ni pamoja na kuanzisha Seminari Kuu ya Segerea.

Kardinali Pengo akiwa Kardinali wa pili Tanzania baada ya Mwadhama Laurian Rugambwa, ndiye muanzilishi wa utaratibu wa kuchangia jimbo uitwao tegemeza jimbo.

Aliyekuwa Askofu Msaidizi wa jimbo hilo na ambaye sasa ni Askofu wa Jimbo la Mpanda, Eusebius Nzigilwa, alisema katika ibada hiyo kuwa, Kardinali Pengo atakumbukwa kwa mengi ikiwamo kuanzisha utaratibu huo wa tegemeza jimbo.

“Mwaka 1994 alianzisha utaratibu wa tegemeza jimbo na wakati huo zilipatikana Sh milioni 17, mwaka 2019 wakati anastaafu tegemeza jimbo ilipatikana Sh bilioni tatu. Fedha hiyo imesaidia kuendesha shughuli za kichungaji jimboni na kuondoa utegemezi na sasa majimbo yote 34 yana mpango huo,” alisema Nzigilwa.

Pengo ndiye muasisi wa Shirika la Kimisionari la Kipapa la Utoto Mtakatifu mwaka 1996. Katika majimbo mengine likiwamo Jimbo la Moshi, shirika hili lilianzishwa miaka ya 80.

Mwaka 1992, Pengo alianzisha utaratibu wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (Wawata) wa jimbo hilo kulea wanafunzi wa Seminari ya Visiga na kwa upande wa Utume wa Wanaume Katoliki (Uwaka) jimboni humo mwaka 2008 aliwakabidhi kulea masista wa Shirika la Dada wa Dogo.

Utaratibu huo umewezesha Wawata zaidi 14,000 kushiriki malezi hayo kwa kuwapelekea mahitaji waseminari hao ikiwamo fedha na vyakula. Pia Uwaka hufanya hivyo kwa masista.

Kardinali Pengo alianzisha mkakati wa kutafuta mapadri wa mashirika mengine kutumikia jimboni humo na kuratibu mshikamano wa kichungaji ulioondoa tofauti ya mapadri wa mashirika na wa jimbo na kuwezesha kupatikana kwa parokia 118. Kwa sasa jimbo hilo lina parokia 126.

Katika Uaskofu wake aliwezesha kupatikana parokia mpya 98 kutoka 20 alizozikuta wakati akipokea jimbo kutoka kwa mtangulizi wake Kardinali Rugambwa (sasa marehemu).

“Sasa Jimbo Kuu la Dar es Salaam lina parokia 126 na linaongoza katika ukanda wa Amecea (Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki wa Nchi za Ukanda wa Afrika ya Mashariki) likifuatiwa na Jimbo Kuu la Nairobi nchini Kenya lenye parokia 114,” alieleza Askofu Nzigilwa.

Alisema Pengo ametengeneza mshikamano wa kichungaji na umoja wa mapadre wa jimbo na wa mashirika ya kitawa kiasi cha wote kujisikia kuwa Dar es Salaam ni nyumbani kwao.

“Ulikuwa ukienda kuomba likizo, ukikosea ukasema unataka kwenda nyumbani kwenu kusalimia hupati likizo, lakini ukisema unakwenda kusalimia marafiki, hata kama ni Marekani utaenda sababu alisema unaenda nyumbani wapi? Dar es Salaam ndio nyumbani kwako,” alisema Nzigilwa.

Aliwasihi waumini kuendelea kumuombea afya njema kwani amemtuma kuwajulisha kuwa, anaamini ni sala zao zimemfikisha hapo alipo hasa akikumbuka kuwa, aliwahi kufikia mahali pa kuwa tayari kufa baada ya kuugua sana na kufanyiwa upasuaji nchini Roma.

Kipindi hicho kinafananishwa na kipindi cha zamani wakati Petro alipofungwa gerezani na kanisa likamuombea mpak akatoka salama. Kwake Kardinali Pengo anaamini kuwa maombi ya waumini na watu mbalimbali ndio yaliyomvusha katika bonge la uvuli wa mauti (ugonjwa).

Wakati wa kumbukumbu yake ya kuzaliwa iliyofanyika Agosti 9, mwaka 2019, Kardinali Pengo alitoa kauli kadhaa ikiwemo ya kusubiri kumtii Mungu wakati wowote atakapomuita kwa pumziko la daima.

Kardinali alisema, “kuna kaburi langu pale Pugu, naomba liheshimiwe. Nawasihi viongozi wote wa kanisa, waamini na wengine wote, nikifa nizikwe kwenye kaburi langu lililoko Pugu (eneo maarufu kwa hija za kikanisa jimboni humo).”

Pengo katika salamu zake za shukrani alizozitoa katika ibada hiyo, aliwashukuru wote waliomuombea na kumtia moyo katika utume wake huku akieleza kuwa wakati alipoteuliwa kuja Dar es Salaam akitokea Tunduru-Masasi, alitii tu kwa sababu ya kiongozi mkuu wa kanisa lakini aliogopa sana.

“Niliwaza mimi mtu kutoka Tunduru-Masasi nitawaeleza nini wataalamu wa mambo wa Dar es Salaam? Lakini niliwahi kuwaambia na ninasema tena nilitii tu kwasababu ya kutii ila niliogopa sana. Lakini Wana Dar es Salaam mlinitia moyo sana, mapadri, masista na waumini, mlishiriki utume wangu kwa sala zenu. Asanteni sana Wana-Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

“Kwenye televisheni kuna tangazo linasema “bibi, nakupenda jana, leo na kesho” na mimi hivyo hivyo, nawapenda jana, leo na kesho,” alisema Pengo katika shukrani zake za shukrani.

Kiongozi huyu si mtu wa kupenda kujigamba kwa ujuzi, akili na uwezo mkubwa wa kufikiri alionao. Ni katika ibada hiyo watu wengi walisikia kwa mara ya kwanza kuwa Pengo ni daktari wa falsafa ya Maadili katika Kanisa. Shahada hiyo ya uzamivu aliipata katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Alphonsiano, Roma, Italia.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Yuda Thadeus Ruwa’ichi, alimshukuru kwa utume wa Daraja Takatifu la Upadri aliyoupokea akiwa na miaka 27 pekee na kwa safari ndefu, ngumu iliyokuwa na changamoto nyingi.

Pengo aliteuliwa kuwa Askofu mwaka 1983 na kuwekwa wakfu mwaka 1984 kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo jipya (wakati huo) la Tunduru-Masasi lililozaliwa baada ya kuvunjwa kwa jimbo la Nachingwea.

Aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam mwaka 1990 na mwaka 1992 alianza rasmi kuliongoza jimbo hilo. Mwaka 1998 aliteuliwa kuwa Kardinali na Papa Yohane Paulo wa II.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/d0970a6883af3f592727e14c25c47e46.jpg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi