loader
MUUMINI MWINJUMA: Muimbaji, mtunzi na mwalimu wa dansi asiyechuja

MUUMINI MWINJUMA: Muimbaji, mtunzi na mwalimu wa dansi asiyechuja

KUNA usemi usemao ‘ng’ombe hazeeki maini’ ndivyo inavyoonekana kwa mkongwe wa muziki wa dansi nchini Muumini Mwinjuma anayejivunia ubora wa sauti yake isiyochuja.

Msanii huyu aliyezaliwa miaka 51 iliyopita, kimuonekano utadhani bado ni kijana mdogo wa miaka 25 lakini kumbe umri umeenda kidogo.  Ni msanii asiyejivuna, mchangamfu na mcheshi kwa kila mtu.

Uzuri wa sauti yake bado upo ni kama vile alivyoanza kuimba miaka ya zamani kipindi hicho akiwa katika bendi ya Bantu angali kijana mdogo kabla na baadaye kupita bendi mbalimbali na kujizolea umaarufu kutokana na uzuri wa sauti yake.

Hilo alilidhihirisha hasa baada ya kutembelea Ofisi za Magazeti ya Serikali (TSN), kwenye chumba cha habari cha HabariLeo na kama haitoshi alitoa burudani kidogo kwa kuimba na kudhihirisha kuwa bado yupo sana na sauti yake itaendelea kung’ara mbele ya mashabiki wake.

Kwenye mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni, nyota huyo anasimulia safari yake ya muziki na wapi anakoelekea.

HISTORIA YAKE

Nyota huyu anayetokea Bagamoyo mkoani Pwani alizaliwa mwaka 1970 na ni baba wa watoto saba.

Kazi yake kubwa anayoitegemea ni muziki ingawa pia, ni mkulima wa  mbaazi, viazi vitamu na mihogo.

Alianza muziki mwaka 1989  katika bendi ya Lola Afrika na anasema alikuwa akifanya shughuli zake hapa nchini na hata Kenya.

Muumini anaelezea mtu aliyemfanya yeye kuingia katika sanaa ya muziki ni Hassan Rehan ‘Bitchuka’ ambaye ni muimbaji katika bendi ya Sikinde ‘ngoma ya ukae’ kwani ni miongoni mwa wasanii wakongwe anayewahusudu kutokana na ubora wa sauti.

“Bitchuka alifanya nipende muziki, napenda anavyoimba ni msanii mwenye sauti nzuri sana. Kuna wengine kama Fresh Jumbe, Benovilla Antony na wengine,”anasema.

Anasema licha ya kuimba ni msanii aliyejaliwa vipaji vingi kwani hutunga mwenyewe, huimba, hupiga tumba na hata kufundisha wengine muziki.

“Najivunia na kipaji ambacho Mungu amenipa, natumia hichi nilichonacho kuendelea kuwaburudisha wapenzi wa muziki nchini,”anasema Muumini.

BENDI ALIZOPITIA

Alipitia bendi mbalimbali ikiwemo Bantu mwaka 1991, Washirika Stars mwaka 1992 baadaye akatoka hapo na kujiunga na MCA International mwaka huo na mwaka 1994 akaenda Kenya.

Alirejea nchini mwaka 2000 akajiunga na bendi ya Twanga Pepeta na kufanya nao kazi miezi mitatu kisha baadaye akajiunga na Mchinga Sound.

Hata hivyo, hakudumu sana mwaka uliofuata akajiunga na African Revolution (Tamtam). Mwaka 2002 alianzisha bendi yake Double M Sound aliyodumu nayo miaka miwili tu.

Mwaka 2004 akajiunga na Double Extra na kufanya kazi na msanii mwenzake wa muziki wa dansi Ali Choki nayo ilidumu kwa  miwili pekee.

Mwaka 2006 akajiunga na TOT kisha miaka miwili baadaye akajiunga na bendi nyingine ya Bwagamoyo Sound.

Baadaye tena mwaka 2010 akarejea Twanga Pepeta, 2012 Victoria Sound na 2014 akurudisha bendi yake ya Double M Sound aliyokaa nayo hadi 2020.

HAZISAHAULIKI

Muumuni anasema ana nyimbo nyingi ila hatosahau zilizompa umaarufu mkubwa na kutamba mtaani ni  kuwa ni  Tunda, Kilio cha Yatima, Mgumba, Fadhila kwa wazazi, Paulina, Chande, Kiu ya Mapenzi na Ndugu Maisha Kitendawili.

Nyimbo hizo zilifanya vizuri katika soko la muziki wa dansi miaka ya nyuma kwa sababu ya ujumbe uliokuwa ndani yake lakini pia, sauti yenye kuvutia.

Unaweza kusema mashairi yake hayachuji kwa kuwa ujumbe ulioko ndani ya nyimbo hizo unagusa maisha ya wengi kizazi hadi kizazi, ni nyimbo ambazo hazichuji ndio maana leo akisema aziimbe kwa wale waliowahi kuzisikia ni lazima wataguswa.

Nyimbo hizo zilivuma zaidi miaka ya 2000 ambako muziki wa dansi ulifanya vizuri kutokana na kupigwa kwenye vyombo vya habari kabla ya muziki wa kizazi kipya kuvamia soko kwa kasi.

Baadaye muziki huo ulishuka kidogo sokoni kutokana na sababu mbalimbali bendi kadhaa zikapoteza muelekeo na hasa baada ya kutokea kwa virusi vya corona.

KILICHOWAPOTEZA

Anasema vyombo vya habari vilianza kuwatenga vikawa haviupi muziki wa dansi nafasi kubwa kama zamani, hivyo thamani yake ikashuka kidogo.

Muumini anasema  kitendo cha nyimbo zao kutosikika kwenye vyombo vya habari huku asilimia kubwa zikisikika za kizazi kipya kiliwakatisha tamaa na kuwafanya warudi nyuma kidogo.

“Ni kweli tulipoteza mwelekeo kwa sababu tulikuwa tunapeleka nyimbo hatuzisikii zikipigwa kama zamani, hii ilitukatisha tamaa tukapoteza mwelekeo kidogo…unapiga hesabu utoe wimbo utasikika wapi,”anabainisha Muumini na kuongeza kuwa ilifika mahali mambo yalikuwa mabaya zaidi kwani muziki huo wa dansi ulishuka thamani ikafikia hatua watu hawaingii kwenye shoo kwa kiingilio bali kwa kinywaji.

Kitu kingine kilichowapoteza ni uwepo wa virusi vya corona na hivyo kumbi nyingi za starehe zilifungwa kutokana na maagizo ya serikali.

Muumini anasema hakukuwa na bendi  wala matamasha yanayowaingizia fedha na matokeo yake walijikuta wakilazimika kukaa nyumbani kwa muda mrefu.

Msanii huyo anasema hata baada ya kumbi za starehe kufunguliwa bado muziki huo haukufanya vizuri.

Hata hivyo, mwaka jana alirejea akiwa katika bendi nyingine inayojulikana kama Shedai ambayo ni mpya na iko chini ya mwekezaji Asha Ramadhan aliyekuwa anataka kujaribu soko la muziki huo likoje.

Muumini anasema mwekezaji huyo aliwawezesha vifaa na fedha lakini kwa kuwa alijitokeza kipindi kibaya kilichokuwa na virusi vya corona, alishindwa kupata kile alichokitaka kwani soko la muziki huo lilidorora.

“Mwekezaji huyo alikuwa akitulipa mishahara mimi na wenzangu lakini kadiri siku zilivyosogea alikuwa haingizi kitu kwa kuwa ilikuwa kipindi kibaya cha magonjwa,  hakukuwa na soko zuri,”anasema.

Msanii huyo anasema kutokana na changamoto hiyo, mdau huyo hakudumu kwa sababu aliona kama anapata hasara kubwa kwa kulipa fedha nyingi kulipa mishahara wakati bendi haiingizi chochote,  kwa hiyo aliamua kuwaachia bendi.

Kingine wakati wakiwa kwenye harakati za kutaka kuzindua bendi hiyo Julai 25, mwaka jana ukatokea msiba wa Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamini Mkapa tukio ambalo liliwalazimu kushindwa kuendelea na mipango yao.

Bendi hiyo ilikuja kufa, kwa sababu wafanyakazi 16 waliokuwa wameajiriwa walikuwa na madai wakazuia vyombo  vya muziki.

UJIO MPYA

Muumini anasema wanakuja kivingine na wana bendi inatwa Special Tamtam ikiwa chini ya Mkurugenzi Mwezeshaji Dk Nyange Shabani.

Nyota huyo wa muziki wa dansi anasema tayari ndani ya bendi hiyo iliyoanza mwishoni mwa mwaka jana wametoa nyimbo kadhaa na baadhi amechanganya dansi  na muziki wa singeli unaotamba sasa ili kuwavuta mashabiki.

Anasema muziki umebadilika na kwamba wengi wanapenda singeli na muziki wa kizazi kipya,  hivyo yeye ameona aingie kidogo huko na kuchanganya na dansi kuendana na soko la sasa.

Miongoni mwa nyimbo alizotoa kupitia bendi hiyo mpya ni Yatima Mzee, Mwanangu, Fenesi, Kwa Mpalange, Mtumbue, Suluhu ya Ndoa na Mkonga wa Tembo na mwezi huu ataachia mwingine Vumbi la Kongo .

“Kwenye muziki wa dansi wengi wanaofuatilia ni watu wazima nikaona kuna haja ya kwenda kwa vijana nichanganye kidogo na singeli nipate mashabiki tofauti,”anasema na anaongeza kuwa Singeli ndio muziki anaoweza kujichanganya nao lakini sio bongo fleva. 

MAPOKEZI

Anasema baada ya kurejea, amepata mapokezi mazuri ingawa mambo mengi yamebadilika anahitaji kujitangaza upya  ili kuingiza muziki wake kwenye mitandao inayouza muziki.

Miaka ya nyuma walikuwa wanategemea kuweka nyimbo zao kwenye CD na Kaseti ila sasa watu wanauza muziki mitandaoni.

Muumini anasema amejiunga na mtandao wa YouTube na ameanza kuingiza nyimbo zake huko ingawa bado hajapata wafuasi wengi ila anajivunia wachache wanaoendelea kumuunga mkono akiamini kadiri atakavyotoa nyimbo zuri ipo siku wataongezeka.

CHANGAMOTO

Anasema licha ya kuwepo kwenye tasnia kwa muda mrefu bado anakabiliwa na changamoto ya kifedha kwani walivyoyumba miaka ya hivi karibuni hawakuwa na kitu cha kuwaingizia fedha.

Nyota huyo anasema zipo nyimbo kadhaa anahitaji kushuti video kama Suluhu ya Ndoa na Mwanangu ambazo zinahitaji fedha kwa ajili maandalizi kuanzia mavazi kwa ajili ya wale watakaokuwa katika bendi.

Jambo lingine anasema kuna watu wamekuwa hawapendi kile anachokifanya kwani kitendo cha yeye kurejea kimeleta maneno yasiyo mazuri hasa alioko nao katika muziki huo. 

“Kuna vita mtaani,  wapo ambao hawakutamani nirudi katika muziki, wapo wanaofurahia kuona mtu unapata shida na pengine kupotea kabisa kwa sababu baada ya kufa kwa bendi ya El Shadai  kuna walioshangilia,”anasema.

Anataja changamoto nyingine ni ukosefu wa baadhi ya vyombo muhimu kama mixer, ngoma ambayo ni muhimu katika bendi na anatoa wito kwa watu watakaotaka kuwaunga mkono wajitokeze washirikiane.

MIKAKATI

Wasanii wengi sasa wamekuwa wakikimbilia katika albamu tofauti na miaka ya nyuma ambako walikuwa wanaona ni kupoteza fedha, lakini kulingana na namna wengi wanavyouza muziki mitandaoni kuna manufaa.

Muumini anasema anatarajia kuachia albamu mbili kwa mpigo atakazozindua Desemba 4, mwaka huu. Albamu ya kwanza itakuwa na nyimbo 10 za singeli na nyingine nyimbo 10 za muziki wa dansi ili kuwakamata mashabiki wa pande zote mbili.

“Mchakato umeshaanza nimebakiza nyimbo chache kukamilisha idadi ya nyimbo ninazohitaji katika kila albamu, naamini nitakamilisha,”anasema na anaongeza kuwa mbali na albamu anajipanga mwakani Mungu akijalia kuanza ziara ya mikoani na kufanya matamasha ya wazi.

Anasema anachotaka kufanya sasa ni matamasha ya wazi sambamba na kwenda kupiga shoo kwenye kumbi kwa kiingilio cha kinywaji hadi pale mambo yatakavyokuwa sawa.

Msanii huyo anasema wameanza mpango wa kufanya maonesho ya wazi na watakachokuwa wanafanya ni kutafura wadhamini. 

Mpaka sasa wamepata makampuni mawili yaliyoonesha nia ya kufanya nao kazi ambazo ni Superdoll, Benki ya Access na RBI.

“Kupitia makampuni haya naamini nitatumia fursa ya kujitangaza kuwa nimerudi upya hivyo nategemea baadaye nipate mialiko ya kwenda kutumbuiza sehemu mbalimbali, namba yangu ni 0713-315500,  ”anasema.

Anasema iwapo kuna watu wanamuhitaji kwa ajili ya shoo anaweza kuwachaji kuanzia Sh 600,000 kwa maeneo ya karibu lakini kama ni mbali bei maelewano kwa maana inaweza kuongezeka na anaongeza kuwa wapo tayari kupiga shoo kwenye maharusi iwapo watahitajika.

Nyota huyu ameomba mashabiki wamuunge mkono katika ujio wake mpya ikiwemo kumfuatilia katika kurasa zake za mitandao ya kijamii za Youtube, Instagram kwa jina la princemwinjuma.

Wito kwa serikali 

Muumini anaiomba serikali iwakumbuke na kuwasikia wasanii wa muziki wa dansi kwani walisahaulika, wamekuwa hawaitwi tena katika shughuli za serikali na kuomba iwaangalie na wao wanufaike kupitia matamasha mbalimbali kama inavyofanyika kwa wasanii wa bongo fleva.

Muumini akimalizia mahojiano anasema wanasanii wa kizazi kipya anaowakubali ni wengi ila aliwataja kwa uchache kama Nassibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Ali Kiba, Faustina Charles ‘Nandy’, Ruby, Zuhura Othman ‘Zuchu’ na Judith Wambura ‘Lady Jaydee’.

Anasema yuko tayari kuimba wimbo kwa kushirikiana na msanii yeyote atakayemuhitaji iwe ni wa kizazi kipya, singeli au muziki wa dansi.

MIRAHABA

Muumini ni miongoni mwa wasanii waliovutiwa na kauli ya Rais Samia Suluhu aliyotoa hivi karibuni kuhusu  kuanza kulipwa mirahaba kutoka kwenye vyombo vya habari na mitandao.

Anasema anafurahia kauli hiyo anaamini Chama cha Hakimiliki(Cosota) kitawatendea haki kwa kukusanya mirahaba kwa ufanisi ili kila mtu apate kile anachostahili.

“Rais ametujali, tunaomba wale wanaokusanya watutupie macho wanamuziki wa dansi nasi tunuifaike,”anasema na kumuomba  Rais huyo awakumbuke  katika matukio ya serikali.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/bcb906b1c010ec5987f098674a7af08c.jpg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi