loader
PETRA NA VIRGINIA KIDANKA;  Watunga vitabu kuelimisha watoto wenzao

PETRA NA VIRGINIA KIDANKA; Watunga vitabu kuelimisha watoto wenzao

KILA Juni 16 ya kila mwaka Tanzania inaungana na nchi nyingine za Afrika kusherehekea Siku ya Mtoto wa Afrika ni kumbukumbu ya mauaji ya watoto zaidi ya 10,000 yaliyotokea Afrika Kusini.

Watoto hao waliuawa wakiwa kwenye maandamano katika kijiji cha Soweto nchini humo mwaka 1976 wakipigania haki zao kama vile elimu bora, afya bora na huduma nyingine muhimu.

Mwaka huu imetimia miaka 30 tangu yaanze maadhimisho ya siku hiyo ambapo mwaka 1991 Mkutano wa iliyokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) kwa sasa Umoja wa Afrika(AU)ulipoidhinisha maadhimisho ya siku hiyo.

Hivyo kila Juni 16 wadau wa haki za watoto hukutana kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu haki za watoto na hupitia utekelezwaji wa mikakati ya serikali katika kuimarisha usalama wa watoto.

Lakini pia hutumia wasaha huo kuja na mikakati kwa ajili ya utekelezaji wa malengo mengine ya watoto kwa miaka mingine ijayo, lakini pia inakuwa ni nafasi kwa wadau wengine kushauri nini kifanyike kuwasaidia watoto katika ngazi za shule au familia.

Zimekuwepo taratibu mbalimbali zinazotumiwa na wadau kuadhimisha siku hiyo ambapo hutumia muda wao kuzungumzia utekelezwaji wa mapendekezo kadhaa kuhusiana na haki za watoto huku wakija na mapendekezo mengine pamoja na mafunzo.

Watoto wawili Petra Kidanka (11) na mdogo wake Virginia Kidanka (9) mwaka huu wameshiriki kikamilifu kusherehekea Siku ya Mtoto wa Afrika kwa kutunga vitabu kuhusiana na watoto wenzao.

Watoto hao ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Masaka iliyopo Gongo la Mboto, Dar es Salaam. Petra anayesoma darasa la sita ameandika kitabu cha kurasa 32 na ni mchanganyiko wa hadithi tofauti kuhusiana na watoto, wakati mdogo wake, Virginia anayesoma darasa la tano ,kitabu chake kinahusu umuhimu na namna ya kupaka rangi na chenyewe kina kurasa 16.

Petra anasema alikiandika kitabu chake wakati wa likizo ya ugonjwa wa corona mwaka jana wakati huo akiwa na miaka 10.

Anasema kitabu hicho kinafundisha watoto masuala mbalimbali kwa njia ya simulizi, zinazotokana na hadithi tofauti tofautu zilizopo ndani ya kitabu hicho.

“Kupitia simulizi zilizopo katika kitabu hiki, watoto wenzangu ni rahisi kujifunza masuala mbalimbali… kitabu kinatoa simulizi za matukio ya aina tofauti na ndani yake wanaendelea kujifunza. Nimetumia miezi kama sita hivi kukamilisha.

“Ilikuwa ni muda mzuri kwangu kufikiria masuala mbalimbali  yanayohitajika kwa watoto na niliunganisha hadithi na kuanza kuandika, namshukuru mama yangu kwa kuwa karibu wakati naandika,” anasema.

Mbali na kuandika, Petra pia anapenda kusoma vitabu na majarida yenye machapisho ya masuala mbalimbali ya maendeleo kwani anaamini kuwa hatua hiyo inamuongezea uwezo zaidi wa kutambua mambo mbalimbali.

Petra anasema kuwa hupendelea kutazama vipindi maalumu vya Televisheni ambavyo vinafundisha na kuwa hujifunza masuala mbalimbali ya msingi.

Kwa upande wake  Virginia anayesoma darasa la tano shuleni hapo, anabainisha kuwa ameamua kuwaelekeza watoto na wanafunzi wenzake namna ya matumizi ya rangi ikiwa ni pamoja na namna ya kupaka huku akiwataka wanafunzi kutumia kitabu hicho kujifunza.

“Nimejipanga kuhakikisha kuwa vipaji vya kupaka rangi kuchora vinakuwa zaidi nchini na kwa kuanzia nimewapatia zawadi ya kitabu hiki watoto wenzangu hawa na mengine makubwa zaidi yanakuja,” anasema Virginia.

Mama mzazi wa watoto hao, Secelela Balisidya, anabainisha kuwa kuna umuhimu kwa wazazi kusikiliza na kuendeleza mambo ambayo watoto wanapenda na anaongeza kuwa katika kuwasadia watoto kufikia malengo yao kuna haja ya kusikiliza na kuwasaidia kwa hali na mali.

“Katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika,  watoto hawa wakaona wazindue vitabu vinavyohusiana na masuala kadhaa ya watoto kwa ujumla, lakini kwa sasa napenda kuwakaribisha wadau kuvinunua na kuvisambaza vitabu hivi ili viwafikie watoto sehemu mbalimbali za nchi,” anasema.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania, (Tamwa) Rose Reuben akizungumzia kuhusiana na hatua ya watoto hao kuadhimisha siku hiyo kwa kuandika vitabu, aliwataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuendeleza vipaji vya watoto na kuinua uwezo wao katika fani mbalimbali.

Alisema watoto wakianza kuandika vitabu wakiwa bado watoto wanaweza kuja kuwa waandishi wakubwa baadaye na wenye uwezo wa kuchambua masuala mbalimbali katika jamii wanazoishi.

“Siku ya Mtoto wa Afrika ni siku ambayo Afrika na Dunia nzima kwa ujumla wadau wa haki za watoto, elimu na maendeleo wanakaa kujadiliana masuala mbalimbali ya haki za watoto. Inafurahisha pia kuona watoto wenyewe sasa wanajitokeza na wanafanya mambo makubwa kama haya ya kuandika vitabu, hapa wameasisi yale yaliyopiganiwa na watoto wenzao Afrika Kusini ya kupigania haki za elimu bora na hawa wamewawezesha wenzao kielimu pia,” anasema.

Rose anawataka wazazi, walimu, walezi na jamii nzima kwa ujumla kutambua kuwa mbali na jukumu lao katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowafika watoto, bado wanatakiwa kuendeleza uwezo na vipajo walivyonavyo watoto katika masuala mbalimbali kama uchoraji, uandishi, michezo na mengineo.

Mwanahabari mkongwe  Rose Mwalimu aliyezindua kitabu hicho alitoa wito kwa wazazi kutodharau mawazo au vipaji vya watoto wao.

“Ili mradi mtoto anakuwa kwenye mstari bora zaidi wa kimalezi na anachokifanya ni shughuli halali, mzazi au mlezi ni wajibu pia kuendeleza shughuli husika anayopenda kuifanya mtoto, siyo kumuachia mwalimu peke yake,  ila kuna haja ya wote kushirikiana katika kuendeleza vipaji vyao,” anasema.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/0712388dd48c9228104a3325a073b12c.jpg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Evance Ngingo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi