loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kiemi: Tumeleta mabadiliko   makubwa ufugaji nyuki 

Kiemi: Tumeleta mabadiliko  makubwa ufugaji nyuki 

PHILEMON Kiemi ambaye ni Rais wa Umoja wa Vijana Wajasiriamali na Wataalamu wa Miradi Mkoa wa Singida (SYECCOS) ni mmoja wa wafugaji wakubwa wa nyuki wenye mafanikio makubwa nchini. Ameleta mabadiliko katika ufugaji wa nyuki kwa kuanzisha kijiji na jiji la nyuki ulimwenguni huku akitoa mafunzo kwa wafugaji wapya. Maeneo yake ya ufugaji yanahudumia mizinga 20,300. Anasema yeye ni mtu watatu kuhudumia mizinga mingi duniani. Amefanya mahojiano na HAMISI KIBARI, baada ya kutoa wasilisho lake kuhusu ufugaji wa nyuki katika moja ya mijadala inayoendelea nchini kote kuhusu namna ya kuboresha Mifumo ya Chakula nchini. 

Swali: Hebu tupe dhana nzima ya kijiji au jiji ya nyuki. Ni kitu gani hasa?

Jibu: Ni vigumu katika hali ya kawaida watu kufuga nyuki na kuwa na vitu vyote muhimu kama mizinga, mavazi na kila kinachohitajika ikiwemo kutoa elimu kwa wahitaji wengine katika eneo moja. 

Kuna watu ambao hawana muda wa kufuga nyuki, lakini wana mitaji na wanataka kuelekeza pesa zao kwenye ufugaji wa nyuki.

Hivyo ni muhimu maeneo yanayoweza kufuga nyuki yakaitwa vijiji au majiji kutegemea ukubwa na wingi wa mizinga ili kujibu changamoto hizo.

Vijiji na majiji ya nyuki yanakuwa na sifa zake. Kwa mfano, vitu vyote vya huduma na mazao ya nyuki vinapatikana pamoja. Kijiji cha kwanza cha nyuki kuanzishwa duniani, kiko Kisaki, Singida. Nilikianzisha mimi na fikra hiyo imekuwa na manufaa makubwa.

Watanzania wengi walikuwa wanahangaika. Hata mimi nilipitia hizo changamoto. Kwa mfano, unaagiza vazi la nyuki kutoka Pakistan. Miaka ya nyuma kulikuwa hakuna Mtanzania anayeweza kushona vazi la kujikinga na nyuki. Kwa hiyo unaagiza vazi halafu linakaa bandarini miezi minne, wakati ulikuwa unatarajia kulitumia hilo kurinia asali kwenye msimu wake. Unajikuta msimu wa kuvuna unapita, kwa sababu asali huvunwa kwa msimu fulani, mfano mwezi wa sita kwa hiyo ikifika mwezi wa nane kabla hujapata vazi, hupati kitu.

Hata sasa hivi kuna watanzania wengi wanavuna asali bila kutumia mavazi, wanang’atwa sana na nyuki, wanakimbia, wanaacha asali kwenye mizinga. Mimi nikaona kwamba ni lazima tuwe na sehemu moja ambayo mtu akiingia anapata huduma zote. Anapata mafunzo na vifaa.

Kwa hiyo kijiji cha nyuki, kama nilivyokwisha sema, kinakuwa na huduma zote za nyuki pamoja na mazao.

Tofauti iliyopo kati ya kijiji na jiji la nyuki ni kwamba kwenye jiji ni eneo kubwa zaidi. Kijiji huanzia ekari 50 hadi 5,000 lakini kwenye jiji ni kuanzia ekari 30,000 na kuendelea. 

Kwenye jiji unakaribisha hata wawekezaji wakubwa, watu ambao watamiliki kuanzia ekari 50, wakaweka mizinga 100, mizinga 1,000 au 500,000 na kuendelea.

Kwa hiyo ili uweze kukuza ufugaji wa nyuki na uweze kuongeza huduma ya mazao ya nyuki ni vyema utafute watu wenye pesa nyingi uwatengenezee jiji. Na kwa upande wa wafugaji wadogo, unawetengenezea kijiji. 

Kwenye kijiji, mfugaji hanunui ardhi. Kwa mfano, wewe unaweza kuwa na mizinga yako 10, mizinga 20 au zaidi unaenda kuiweka kwenye kijiji cha nyuki. Waliopo kwenye kijiji wanasimamia mizinga yako na kukupa matokeo.

Ukishaleta mizinga yako kwenye kijiji, unaingia mkataba na wenye kijiji. Kwa mfano, unasema mimi kila mwaka nitahitaji kilo 30 kutoka kwenye kila mzinga wangu au pesa taslimu. Bei ya soko ya asali kwa kilo moja ni kati ya Sh 10,000 na 15,000.

Hili wazo limepokelewa vizuri sana na serikali kwa sababu linalinda misitu na linaongeza ajira. Pia linasaidia mtu anayetaka kufuga nyuki lakini yuko mbali au hana eneo na muda kutekeleza azma yake. Unaleta mizinga yako kwenye kijiji, unasubiri mavuno na kugharamia huduma kidogo. Unapata pesa au asali, kwa hiyo ni uwekezaji mmoja mzuri kabisa.

Lakini pia mpango huu unaongeza ajira kwani kila mizinga 100 inaajiri kijana mmoja wa kitanzania mwenye kiwango cha chuo kiku au kiwango chochote cha elimu alimradi awe na uzoefu.

Kumbuka kwenye kijiji kuna shule. Mpaka sasa mimi nimefundisha watu 2,300. Mwaka huu tunaoendelea nao  malengo yetu ni kufundisha watu 1,000 na mwaka ujao nitaongeza kiwango hadi kufikia watu 5,000. Ninafanya hivyo kwa sababu watu wengi hawana maarifa ya kutosha na ninaamini kwamba nitakuwa nimesaidia watu wengi. 

Swali: Ni sehemu gani inafaa kuanzisha kijiji cha nyuki?

Jibu: Kwanza pawe na ardhi yenye misitu ambayo haina mabaki yoyote ya kemikali. Misitu iwe ni yenye maua mbalimbali. Mfano, unaweza kukuta eneo la miti ya aina mbalimbali hata zaidi ya 1,000 ambayo huchanua kila mara kwa mwaka mzima, iwe kiangazi au masika. Hilo ni zuri kwa kuanzisha kijiji cha nyuki.

Lakini napenda wananchi pia waelewe kwamba kila anakoishi bindamu nyuki pia anaweza kufugika. Tanzania nzima takribani kila sehemu mtu anaweza kufuga nyuki, lakini cha kuzingatia ni kwamba nyuki anauma na hivyo anatakiwa atengwe. Na pia ufugaji unapaswa kuangalia eneo lisilo na kemikali au yale yote tunayoyajua yanaharibu chakula.

Nahimiza watu watafute maarifa na kuanzisha mfumo wa kijiji cha nyuki, watapata nafanikio mengi kama mimi ninavyopata.

Swali: Ulipata elimu yoyote ya masuala ya ufugaji nyuki au ni utundu na ubunifu wako?

Jibu: Nilianza kwanza kwa kutafuta maarifa kabla sijaanza ufugaji mkubwa. Mimi sasa hivi nina umri wa miaka 33, lakini kabla sijafikisha umri wa miaka 32 nilitembelea nchi 32 duniani nikitafuta maarifa. 

Nusu ya safari yangu ya kuzunguka dunia kutafuta maarifa nilifadhiliwa na serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini nusu ya safari nilitumia gharama zangu mwenyewe.

Swali: Huko kote ulikuwa unajifunza ufugaji wa nyuki pekee au ulikuwa unajifunza na mambo mengine.

Jibu: Nilikuwa ninajifunza ufugaji wa nyuki pekee. Unajua nyuki ni kitu kipana sana. Japo hapa Tanzania inaitwa sekta ndogo lakini si sekta ndogo. Ni pana yenye vipengele vingi.

Kwa mfano, nilipokuwa Uturuki, niligundua kwamba kwa asilimia 75, ili nchi iweze kufanya vizuri kwenye kilimo, lazima mtumie nyuki kwa ajili ya uchavushaji wa mazao.

Kwa nchi ya Uturuki hilo wanalizingatia sana. Wanaamini kwamba endapo nyuki watotoweka kwenye ardhi yao, sekta ya kilimo pia itaathirika vibaya. Kwa hiyo hapo unaona umuhimu wa nyuki kwenye maisha yetu ya kila siku.

Nije kwenye mifugo. Unaweza kuona nyasi zimechanua kila mwaka, lakini hujui, anayefanya mwendelezo wa zile nyasi ni nyuki. Kwa sababu ili ua litengeneze mbegu yoyote lazima liguswe na nyuki. 

Kuna viumbe wengine wanafanya uchavushaji kama manyigu, vipepeo na kadhalika lakini mchavushaji mkubwa kwenye uso wa dunia, kwa takribani asilimia 75 ni nyuki.

Kimsingi, asilimia 85 ya mimea iliyoko kwenye uso wa dunia inahitaji uchavushaji kwa njia ya cross pollination (kutoka kwenye mti mmoja kwenda mwingine) na silimia 15 ndio inafanya self-pollination (inajichavusha yenyewe). Mfano ni mhindi ambao unatoa mbelewele juu na huku chini unatoa kitu kama ndevu.

Hata hivyo, kwenye mimea inayofanya self-pollination, ukiongeza nyuki, unaongeza pia ufanisi kwa asilimia 10.

Nyuki akitumika kwenye mashamba kama ya alizeti na mazao mengine ambayo yanahitaji cross pollination, maana yake ni kwamba kama ulikuwa unapata gunia kumi, basi idadi itaongezeka.

Swali: Mtu akitaka kujifunza kwenye kijiji chako maarifa ya kufuga nyuki, ni vigezo gani anavyotakiwa kuwa navyo?  

Jibu: Kwanza kabisa kwenye kijiji nimejenga sehemu za kulala, sehemu za kusomea, kucheza na hata starehe. Mtu anasoma kwa starehe. Kuna watu wanadhani kwamba ili kupata maarifa lazima uumie sana. Hapana, maarifa pale unayapata huku unakunywa kahawa na maziwa. Ndio maana nina wazee wastafu pale wanafurahia.

Mimi siamini kwamba kupata maarifa mpaka uweke miguu kwenye beseni la maji ndio uelewe. Mambo kama hayo yanatakiwa yawe kwenye sehemu za kurekebisha tabia kama kwenye magereza. 

Gharama za kujifunza kwa Watanzania kwa mwezi ni Sh 975,000. Kiwango hicho kinahusisha malazi mwezi mzima, chakula mwezi mzima na unapewa vazi la kurinia asali unapohitimu pamoja na mzinga mmoja wa kuanzia. Lakini kwa watu wa nje mbao ninwafundisha pia, wanalipa Dola za Marekani 800.

Swali: Mwezi mmoja unatosha mafunzo kwa mtu?

Jibu: Mwezi unatosha sana. Mimi ninashauri hata watu wanaokwenda vyuo vikuu kunakupotezeana sana muda huko. Mtu asome maarifa anayoyahitaji kufanyia kazi mwezi mmoja tu kama si michache tu. Mtu anasoma miaka mitatu lakini ukimuuliza umepata maarifa gani ya kufanyia kazi katika hiyo miaka mitatu mwingine hana kabisa.

Kama maarifa fulani, kama ya nyuki yanahitaji mwezi mmoja tu na mtu kuelewa kila kitu, kwa nini umpeleke miaka mitatu? 

Itandelea

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/d63c8f2c70cd7ac78332524bc22577aa.jpg

*Ni salama asilimia 99.99

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi