loader
Dstv Habarileo  Mobile
Karema; bandari muhimu kwa  shehena kwenda DRC, Burundi

Karema; bandari muhimu kwa shehena kwenda DRC, Burundi

SERIKALI imeendelea kuanzisha miradi mbalimbali, mikubwa na midogo, yenye lengo la kusisimua uchumi na kuleta maendeleo kwa wananchi. 

Moja ya miradi hiyo ni ujenzi wa bandari ya kimkakati katika kata ya Karema, wilaya ya Tanganyika, mkoani Katavi unaofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Bandari ya Karema inajengwa na Mkandarasi Xiamen Ongoing Construction Group Co., na waangalizi wa mradi ambao pia ni wawakilishi wa TPA ni kampuni ya M/S Inter-consult Ltd ya mkoani Dar es Salaam.

Bandari hiyo ya Karema ambayo ni moja ya bandari za Ziwa Tanganyika itakapokamilika inatarajiwa kuwa moja ya bandari muhimu na kubwa nchini.

Mhandisi na Mwakilishi wa Bandari katika mradi huo kutoka Inter-Consult Ltd, Elisante Edward, anasema ujenzi na usanifu wa bandari ya Karema ulianza Oktoba 25, 2019 na unatarajia kukamilika Oktoba 24, 2021.

Anabainisha kuwa eneo la mradi kwa ujumla ni mita za mraba 463,740 (sawa na eka 114) na katika hizo mita za mrada 267,2409 (eka 66) ni eneo la nchi kavu na mita za mraba 196,500 (sawa na eka 48) ni ndani ya maji na kwamba mradi huo una thamani ya Sh bilioni 47.9.

Edward anasema kinachofanyika sasa ni utekelezaji wa mradi, awamu ya kwanza unaohusisha mita za mraba 56,000 sawa na eka 14 za ardhi. Anasema ujenzi unahusisha maeneo kadhaa ambayo ni pamoja na ujenzi wa gati lenye urefu wa mita 150 litakalowezesha kusimama meli mbili kubwa hadi yenye urefu wa mita 75 kwa wakati mmoja na ujenzi wa sakafu ngumu katika eneo la mita za mraba 22,500 kwa ajili ya kuhifadhia makontena. Kingine kinachojengwa anasema ni kingo za kuzuia mawimbi ndani ya ziwa.

Anasema awamu ya kwanza pia itahusisha uongezaji wa kina cha maji kwenye gati, ujenzi wa jengo la ofisi kwa ajili ya TPA na wadau wengine kama TRA, Uhamiaji, mawakala wa forodha na wengineo, jengo la abiria na jengo ka kuhifadhia mizigo.

Anasema vingine vinavyojengwa katika bandari hiyo ni miundombinu wezeshi kwa ajili ya umeme, jenereta na transfoma, huduma ya maji, ujenzi wa miundombinu ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama), mfumo wa ulinzi, taa, maji safi na majitaka na mfumo wa kuongozea meli zinapoingia na kutoka.

Kwa mujibu wa Edward, mradi huo wa kimkakati pia umetoa ajira kwa Watanzania 150 hadi kufikia mwezi Mei, mwaka huu wakiwemo wahandisi, mafundi umeme, madereva, wasaidizi, walinzi na watu wasiokuwa na ujuzi na kwamba mkandarasi anaendelea vizuri na kazi huku wafanyakazi wakilipwa bila tatizo.

Ujenzi wa bandari hiyo umeelezwa kuridhiwa na wananchi wa eneo hilo kwa kile wanachoeleza kuwa ni mradi wa kimkakati kuwainua Watanzania kuanzia ngazi ya kijiji, tarafa, kata, wilaya, mkoa na hadi taifa.

Kaimu Ofisa Tarafa Karema, Samson Elias, anasema bandari ya Karema iko katika Tarafa ya Karema yenye kata nne na vijiji 11 na kwamba inatazamia kuzinufaisha kata hizo ambazo ni Karema, Ikola, Isengule na Kapalamsenga.

Vijiji hivyo 11 ni Karema, Itetemya, Itunya, Kafisha, Isengule, Songambele, Kapalamsenga, Ikola, Shukia, Kasangamtongwe na Mchengani.

“Wananchi waliridhia kutoa maeneo yao na asilimia 90 tayari wameshalipwa fidia. Huu ni mradi wa kimkakati na umetoa ajira kwa wanakijiji 150 ambao wanafanya kazi, wakiwemo wa kutoka hapa kijiji cha Karema na vijiji jirani. Vijana wengi wamepata ajira na wanalipwa vizuri sio chini ya Sh 10,000 kwa siku,” anasema.

Mbali na ajira, anasema kupitia mradi huo wamejengewa madarasa manne, zimetengenezwa barabara zenye ubora ambazo zinapitika tofauti na zamani na wamejengewa daraja ambalo linawarahisishia  kusafirisha vitu mbalimbali.

Anasema wafanyabiashara wananufaika kwa kuuza vyakula kama unga, mchele, kuku, mbuzi kwenye eneo la mradi na wengine wanapangisha wafanyakazi wanaohusika na mradi huo.

Elias anasema bandari hiyo itarahisisha sana usafirishaji wa mizigo na abiria na hasa reli kutoka Mapanda hadi Karema itakapokamilika kwa kuwa usafiri wa reli ni nafuu.

“Itakuwa rahisi mwananchi kusafirisha mizigo mikubwa kutoka Dar es Salaam hadi Bandari ya Karema na kisha kupelekwa katika nchi jirani kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Kule wenzetu wana utajiri wa rasilimali za asili kama madini ya shaba, hivyo itawarahisishia kusafirisha kwenda nje madini yao kupitia bandari hii,” anasema Elias.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Karema, Sililo Mpondela anaishukuru serikali kwa kuamua kujenga bandari hiyo ambayo itaifungua Tarafa ya Karema mkoa wa Katavi kwa ujumla kwani itakuwa mlango wa usafirishaji wa bidhaa kati ya Tanzania na DRC na hivyo kuiunganisha bandari hiyo na zile za Moba na Kalemii zilizoko DRC.

Anasema wafanyabiashara wa DRC wamekuwa wakipitisha mizigo Zambia ambako wanatozwa kodi kubwa kwa vile ni mbali, lakini sasa watapata unafuu kupitia Tanzania na hasa reli kutoka Mpanda itakapofika kwenye bandari hiyo.

Anasema hata wafanyabiashara wa Zambia na Burundi nao watanufaika na bandari hiyo.

Mpondela anasema wananchi katika vijiji vilivyopo Karema wanaendelea kubuni biashara mbalimbali ili wazidi kunufaika na bandari hiyo inayotarajiwa kuwa moja ya bandari kubwa za TPA katika Ziwa Tanganyika.

Kaimu Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Agustine Nyoni anasema jiwe la msingi liliwekwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Julai 4, mwaka jana ingawa ujenzi wa bandari hiyo ya kimkakati ulianza mwaka 2019.

“Bandari hii inatoa fursa kwa wananchi na wadau walioko Rukwa, Katavi na Kigoma wanaotumia Ziwa Tanganyika lakini pia kwa majirani zetu kama DRC, kwani mbali na kusafirisha mizigo kutoka Dar kwenda DRC lakini nao ni matajiri wa rasilimali za asili kama madini. Tunararajia madini mengi yatapita hapa kwenda nje na tunaamini watatumia fursa hii kupitisha shehena kubwa ya mizigo yao,” anasema.

Kwa mujibu wa Nyoni, kupitia bandari hiyo, lipo soko la uhakika la mazao kwa sababu nchi jirani za DRC na Burundi zimekuwa na uhitaji wa mazao ya vyakula kama mahindi, mchele, maharage, karanga n.k vinavyolimwa kwa wingi katika mikoa ya Rukwa na Katavi, hivyo ni uwekezaji utakaosisimua uchumi na kuongeza pato la Taifa.

Tunaweza kusema kwa ujumla bandari ya Karema ni uwekezaji maridhawa uliofanywa na serikali kupitia TPA, hatua itakayorahisisha mzigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kufika nchi jirani za DRC, Burundi na hata Zambia kwa urahisi kupitia barabara au reli ya kati.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/553138d386828397e85dffbb61d57581.JPG

*Ni salama asilimia 99.99

foto
Mwandishi: Angela Semaya 

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi