loader
Dstv Habarileo  Mobile
Msimamo wa wasomi kuhusu Katiba mpya

Msimamo wa wasomi kuhusu Katiba mpya

WACHAMBUZI wa masuala ya siasa wamesema hoja ya madai ya Katiba Mpya yaliyotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Mwenyekiti wake Freeman Mbowe siyo msimamo wa Watanzania wote.

Waliyasema hayo  walipozungumza na HabariLEO. Wakili wa Kujitegemea, Reuben Simwanza alisema katika madai ya Katiba Mpya kuna mambo mawili yanayopaswa kuangaliwa kwa kina ikiwemo hitaji la Katiba Mpya na la pili ni la sura ya kisiasa.

Simwanza alisema hitaji la Katiba Mpya haliwezi kuwa takwa la mtu mmoja au wawili, bali linatakiwa kuwa takwa la wananchi ambao katika wingi wao kupitia Uchaguzi Mkuu walipeleka dhamana ya uongozi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema CCM kina ilani yake na viongozi wanaoisimamia ilani hiyo, hivyo kwa CCM kupata dhamana ya kuliongoza taifa, ina maana kwamba watasimamia mambo ambayo waliyanadi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana kwa kuwa hayo ndiyo vipaumbele vyao.

“Kwa hiyo kama sisi wananchi kwa ujumla wetu tulikuwa tunataka Katiba Mpya, maana yake ni kwamba mwaka jana tungewapa dhamana waliokuwa wanajinadi kwa katiba mpya. Lakini kwa sasa sisi wananchi hatuna namna kwa ujumla wetu kukidai CCM kinyume na yale ambayo walijitanabaisha nayo katika Ilani ya mwaka 2020,” alisema Simwanza.

Aliongeza “Kwa hiyo watu wanaposimamia ilani ile, sisi kama wananchi hatuna deni, hiyo sasa inaweza kuwa chachu au nyongeza kwamba pamoja na haya yote, kuna hitaji hili la Katiba Mpya, kwa hiyo kwa kusema hivyo, kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba ajenge uchumi kwanza ilikuwa sahihi kabisa kwa sababu ilikuwa inaendana na Ilani ambayo anaisimamia.”

Kwa mujibu wa Simwanza, endapo Rais Samia ataona kwamba pamoja na mambo ya maendelo ambayo serikali yake inayatekeleza, lakini kama kuna tija ya Katiba Mpya na kwa nafasi yake kama ataona kuna haja ya kuruhusu kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya au kuendelea pale ulipokomea, anaweza kufanya hivyo.

“Lakini tukizungumzia hili la Mbowe, naheshimu kauli yake na yale aliyoyasema kwa matakwa yale ya kisiasa na chama chake lakini si kwa matakwa ya wengi ambao walionesha hisia zao kwa kupiga kura mwaka jana,” alisema.

Alisema pamoja na mawazo mazuri waliyonayo Chadema, haileti tija kutaka kusababisha uvunjifu wa amani usio wa lazima kwa sababu vyombo alivyokuwa akivinyooshea kidole wakiwemo Polisi kwa kuzuia makongamano yao, ni sehemu ya moja kwa moja ya katiba ambayo Chadema wanaidai.

Simwanza alisema mtu hawezi kuzungumzia Katiba Mpya bila kuwataja polisi au vyombo vya ulinzi na usalama kwa sababu vyombo hivyo viliapa kusimamia katiba iliyopo, hivyo hawanabudi kusimamia misingi ya viapo vyao.

“Kwa sababu watu wa ulinzi na usalama katika utendaji wao wa kazi na katika nafasi hizo walizozipata, moja ya vitu vikubwa walivyoapa ni utii wa kuisimamia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo ndiyo hii tuliyonayo Katiba ya mwaka 1977, kwa hiyo katika namna ambayo tunapaswa tuliangalie jambo hili na kuepusha migogoro ni namna ya kulishughulikia suala hili,” alifafanua.

Alisema katika uhalisia wa mambo, inapofikia kwenye mchakato kama huo, nafasi ya Rais inafahamika, hivyo Watanzania hawanabudi kuheshimu kile ambacho Rais wa nchi anaelekeza katika vipindi tofauti tofauti na yasifanyike mambo kama ajenda ya kutaka kujaribu serikali iliyopo madarakani kitu ambacho si sahihi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Demokrasia na Utawala Bora Afrika (ForDIA), Bubelwa Kaiza alisema suala la Katiba lina wadau wake ambao ni serikali, vyama vya siasa na wananchi wa kawaida ambao wanapaswa kukubaliana namna ya kuanza na kuuendea mchakato wa Katiba Mpya.

Kaiza alisema utaratibu wanaoenda nao Chadema hauwezi kuchukuliwa kama utaratibu rasmi kwa sababu utaratibu rasmi wa kupata Katiba Mpya lazima utangazwe na serikali.

“Huu utaratibu wa Chadema sio rasmi wa kushughulikia katiba bali ni utaratibu wao tu wa chama wa kupeana taarifa, ila utaratibu rasmi tunasubiri ule wa serikali kwa sababu itaweka sheria, utaratibu, itagharimia, itaitisha wadau wote watakaa pamoja halafu wanakubaliana namna ya kwenda mbele,” alisema Kaiza.

Alisema msimamo wa Chadema wa sasa kuhusu madai ya Katiba Mpya si wa Watanzania wote bali ni wa chama chao tu na hauna athari yoyote kwa watu wengine. Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema anaunga mkono kwa asilimia 100 madai ya Chadema ya kutaka Katiba Mpya.

Akiwa jijini Mwanza juzi, Mbowe alisema chama chao kitaendelea na msimamo wake wa kufanya kongamano la kudai Katiba Mpya litakalofanyika jijini Mwanza hivi karibuni na baadaye watafanya kwenye kila mkoa, jimbo na kata.

Alipozungumza na Habari- LEO kuhusu siku 100 za Rais Samia, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, John Shibuda alisema Serikali ya Awamu ya Sita ilichambua mambo ya serikali zilizotangulia na kufanya maboresho ili kuboresha maisha ya wananchi na kuinua uchumi.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Magdalena Sakaya alisema uongozi wa Rais Samia umeonesha dhamira ya kuwapa watu matumaini na faraja na akashauri afanye kazi na vyama vya siasa kwa sababu siasa ni sehemu ya maisha ya Watanzania.

Kutokana na hoja hiyo ya Katiba Mpya, Rais Samia alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari Juni 28, mwaka huu, aliwaomba Watanzania wampe muda ili asimamishe nchi kwanza kiuchumi, kisha atashughulikia masuala mengine.

Alisema kwa sasa vyama vya siasa vinaruhusiwa kufanya mikutano ya ndani na watu wao, wabunge kufanya mikutano ya hadhara kwenye majimbo yao.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/813fc086822fbaadd8d24c2a993b2ea8.PNG

POLISI Mkoani Mtwara imikamata watu 15 kwa ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi