loader
Dstv Habarileo  Mobile
Ushindi mkubwa kwa Tanzania kimataifa

Ushindi mkubwa kwa Tanzania kimataifa

SERIKALI imesema kitendo cha Tanzania kushinda katika utetezi wake kupinga Pori la Akiba la Selous kuondolewa katika orodha ya Urithi wa Dunia ni ushindi mkubwa kwa nchi.

“Ushindi mwingine mkubwa kwa Tanzania.:Tanzania imeshinda katika utetezi wake UNESCO) ambayo ilitaka kuliondoa Pori la Akiba la Selous katika orodha ya Urithi wa Dunia kutokana na kutekelezwa kwa mradi wa Bwawa la umeme la Julius Nyerere katika mto Rufiji (Stiegler’s Gorge),” ameandika Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa kwenye akaunti yake katika mtandao wa kijamii wa twitter.

Wizara ya Maliasili na Utalii jana ilisema serikali itaendelea kutekeleza ujenzi wa mradi huo katika Mto Rufiji na eneo hilo la Selous litaendelea kutambulika kama sehemu ya urithi wa dunia.

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Allan Kijazi alisema hayo alipozungumza na HabariLEO.

Hivi karibuni kulikuwa na tetesi kwamba Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), lilitaka kuliondoa eneo la Selous kwenye orodha ya maeneo ya urithi wa dunia kutokana na Serikali ya Tanzania kutekeleza mradi huo wa umeme kwenye eneo hilo

. Dk Kijazi alisema Unesco ndiyo wanaosimamia maeneo ya urithi wa dunia na wakiona taratibu zinakiukwa wana mamlaka ya kufuta maeneo kutoka katika eneo la urithi wa dunia.

Alisema Unesco walileta hoja hiyo kwa Serikali ya Tanzania ya kukusudia kuifuta Selous kutoka katika orodha ya maeneo ya urithi wa dunia.

“Hoja ya msingi ya Unesco ni kwamba Tanzania tunajenga bwawa kubwa katikati ya eneo la urithi wa dunia na kutokana na masharti ambayo wameyaweka ni kwamba mradi mkubwa kama huu ukifanyika lazima washirikishwe kwanza ili watoe kibali,” alisema Dk Kijazi.

Aliongeza “Lakini wao (Unesco) wanadai kwamba Tanzania haikuwashirikisha na mradi huo ni mkubwa, wanavyoona ni kwamba utakuwa na athari kubwa kwenye eneo hilo.”

Dk Kijazi alisema Tanzania ilijenga hoja kwamba eneo ambalo linajengwa bwawa ni eneo dogo linalochukua asilimia 1.8 tu ya eneo lote la Selous ambalo lina ukubwa wa kilometa za mraba 50,000. Alisema eneo hilo la Selous ni kubwa kudhidi hata ukubwa wa baadhi ya nchi.

“Hivyo tukawaambia kwamba eneo ambalo bwawa linajengwa ni eneo dogo sana na eneo kubwa linabaki kwenye hifadhi,” alisema Dk Kijazi.

Kwa mujibu wa Dk Kijazi, sababu ya pili waliyoitoa kwenye utetezi wao kwa Unesco ni kwamba utaratibu unawataka Unesco kutoliondoa eneo lolote katika urithi wa dunia bila kutoa nafasi kwa nchi mwanachama kujitetea.

Alisema katika suala la ujenzi wa bwawa hilo, Unesco walitoa tu tamko bila kuishirikisha Tanzania ili nayo itoe maoni yake.

“Hivyo hoja zetu zilipita katika mazingira haya kwamba Unesco hawakufuata taratibu na pili eneo la bwawa ni dogo sana ikilinganishwa na ukubwa wa Selous. Kwa hiyo sisi tumesema mradi unaendelea na tumekubaliana kwamba tutawapa taarifa sahihi na watafanya marejeo baada ya miaka miwili tukishawapa taarifa sahihi kwa sababu taarifa walizonazo zimepotoshwa,” alisema Dk Kijazi.

Alisema hoja hiyo ya kutaka kuifuta Selous kwenye orodha ya maeneo ya urithi wa dunia iliibuliwa na Unesco wenyewe kwa sababu wana kituo cha ufuatiliaji wa maeneo ya urithi wa dunia.

Alisema kazi ya kituo hicho ni kufuatilia kila kinachoendelea na kuona kama kinazingatia masharti ya maeneo ya urithi wa dunia, hivyo pia walifuatilia mradi wa bwawa la Nyerere na kuona kwamba utakuwa na athari katika hilo eneo.

Dk Kijazi alisema katika suala hilo, hoja za utetezi za Tanzania zilitolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii na Tume ya Taifa ya Unesco ambayo iko chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa kupitia ukurasa wake wa Twitter ulisema hoja zenye nguvu zilizowasilishwa na ujumbe wa Tanzania ziliungwa mkono na wajumbe wa Kamati ya Urithi wa Dunia (Uganda, Ethiopia, Afrika Kusini, Nigeria na Mali).

Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) unatekelezwa na wakandarasi kutoka nchini Misri ambao ni kampuni za Arab Contractors na JV Elsewedy Electric kwa gharama ya Sh trilioni 6.5 na utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 za umeme. Utakamilika Juni mwakani.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/53f4521ed0abdf92927916b2a0b0acfd.PNG

MKUU wa Chuo cha Uhasibu Arusha ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi