loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mamia wamzika  kijana aliyeuawa baa 

Mamia wamzika kijana aliyeuawa baa 

MWILI wa kijana aliyeuawa kwa kupigwa risasi katika baa ya Lemax Sinza kwa Remmy, Dar es Salaam, Zawadi Mushi maarufu Gift umezikwa katika makaburi ya Vikunai, Mtoni Kijichi jijini humo jana.

Mamia ya waombolezaji walishiriki kumzika Gift likiwemo kundi kubwa la vijana kutoka Sinza alipokuwa akiishi na Mtoni ambako ni nyumbani kwa mama yake mlezi.

Kabla ya maziko, waombolezaji waliuaga mwili wa Gift katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mtoni Kijichi.

Wakati wa ibada ya kuuaga mwili wa marehemu, Mchungaji Paul Mziray aliitaka jamii iishi kwa kuzingatia maelekezo ya vitabu vitakatifu.

“Hatujui ni lini Mungu atatuita hivyo tunapaswa kujiandaa muda wote na wakati wote hasa kwa kufanya mambo mema yanayompendeza Mungu ili siku akituita atukute tupo tayari kwenda kushiriki maisha mema mbinguni,”alisema.

Alisema Gift ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 30, huenda alikuwa na malengo makubwa hivyo vijana licha ya kuyahangaikia maisha ya duniani wajipange pia kwenda mbinguni.

Msemaji wa familia, Gideon Mushi alisema Gift alikuwa mtu mwenye maono na aliishi kwa kujituma kazini na hata nyumbani.

Mushi alisema kijana huyo ameacha alama ya urafiki kwa wenzake aliokishirikiana nao kupamba magari, pia marafiki aliosoma nao Sekondari ya Biafra, Dar es Salaam kuanzia mwaka 2006 hadi 2009 na waliosoma pamoja shule ya msingi mwaka 1999 hadi 2005 mkoani Kilimanjaro.

Baada ya ibada ya kuuaga mwili ilianza safari ya kwenda makaburi ya Vikunai yaliyopo Mlimani.

Takribani magari 50 yalipanda mlima huo, madereva wengine waliyaegesha kando ya barabara na kupanda kwa miguu kwenda sehemu ya kuzikia.

Gift aliaga dunia jioni ya Julai 17 baada ya mfanyabiashara, Alex Korosso kumpiga risasi kadhaa sehemu mbalimbali za mwili.

Baada ya Korosso kumuua kijana huyo, naye alijiua kwa kujipiga risasi shingoni akiwa kwenye eneo hilohilo alilomuua Gift.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/b62f5352eb11dfdd971b1f66f554ee34.jpg

POLISI Mkoani Mtwara imikamata watu 15 kwa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi