loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wanaosoma Chuo Kikuu cha Kilimo China waishauri serikali

Wanaosoma Chuo Kikuu cha Kilimo China waishauri serikali

WANAFUNZI Watanzania wanaosoma Chuo Kikuu cha Kilimo China (CAU), wameishauri serikali kuangalia namna ya kuwapunguzia gharama za uzalishaji wakulima ili kuendana na kipato chao.

CAU inatekeleza mradi wa pamoja wa kupunguza umaskini kwa wakulima wadogo mkoani Morogoro.

Wanafunzi hao wanaosoma kwa njia ya mtandao kutokana na changamoto ya usafiri iliyosabishwa na ugonjwa wa virusi vya corona (Uviko-19), walitoa ushauri huo juzi baada ya kufanya ziara ya mafunzo kwa vitendo katika vijiji mbalimbali vinavyotekeleza mradi huo mkoani humo.

Ziara hiyo ililenga kuangalia namna chuo hicho kinavyotekeleza miradi mbalimbali hasa ya kilimo cha mahindi katika kusaidi kuwapunguzia gharama za uzalishaji kwa wakulima maskini kwa kutoa mafunzo mbalimbali ya kuzalisha mazao kwa tija.

Mwanafunzi wa chuo hicho, Juliet Frank alisema pamoja na mambo mengine, mradi huo umewanufaisha wakulima wengi baada ya kupata elimu ya kilimo cha kisasa.

Alisema ipo haja ya wataalamu kuangalia namna bora ya kuwapunguzia kazi za uzalishaji na hivyo kuiomba serikali ya mkoa huo kwa kushirikiana na chuo hicho kuendeleza mradi huo wa pamoja wa kupunguza umaskini kwa wakulima wadogo hasa kupitia kilimo cha mahindi.

"Licha ya mradi huu kuwasaidia wakulima wadogo lakini kuna kila sababu ya kutafuta njia mbadala ya kuwasaidia kupunguza mzigo wa kazi, kuwapo na vitendea kazi kama mashine za kupandia na kupalilia mahindi kama ilivyo katika mazao mengine," alisema Juliet.

Mwanafunzi mwingine, Salma Shehe alisema mabadiliko ya tabia ya nchi yamekuwa yakiwaathiri wakulima wadogo pale mvua zinapokosekana ama kuzidi kiwango na kusababisha mazao kuharibika yakiwa shambani.

Awali, mratibu wa mradi huo, Ernest Mkongo alisema  utekelezaji wake ulianza mwaka 2011 kwa kuanza na kijiji kimoja cha Peapea wilayani Kilosa  na  baadaye kuhamishiwa katika kijiji cha Mtego wa Simba, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro mwaka 2014.

Mkongo alisema kupitia mradi huo, wakulima walijifunza njia za kisasa na kuwawezesha kuvuna magunia 18 ya mahindi kwa ekari moja, wakati awali walikuwa wakivuna magunia manne hadi matano kwa ekari moja.

Alisema baada ya mafanikio katika majaribio hayo, mradi ulipanuka na kuvifikia vijiji vinane katika wilaya zote za mkoa huo katika kipindi cha mwaka 2018 hadi mwaka huu.

Mkongo alivitaja vijiji vingine na wilaya zake kwenye mabano ni Letugunya na Ngayaki (Gairo), Kitete (Kilosa), Kisegese (Kilombero), Kiswago (Malinyi), Kikundi (Morogoro), Makuyu (Mvomero) na Mwaya kilichopo wilaya ya Ulanga.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/ef5d012d0fb30034d9f9bc368403f2fa.jpeg

POLISI Mkoani Mtwara imikamata watu 15 kwa ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi