loader
Dstv Habarileo  Mobile
Dk Mwinyi: Tumedhamiria kupaisha uwekezaji Pemba

Dk Mwinyi: Tumedhamiria kupaisha uwekezaji Pemba

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali ya Awamu ya Nane ina mikakati ya kukiwezesha Kisiwa cha Pemba kuwa eneo maalumu la uwekezaji.

Dk Mwinyi alisema hayo wakati akilihutubia Baraza la Eid Al Adha kwenye ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Wete, Pemba.

Alisema katika kujenga mikakati na malengo hayo serikali inakusudia kuufanyia ukarabati mkubwa Kiwanja cha Ndege cha Pemba pamoja na bandari ya mkoani na barabara zinazokwenda katika maeneo huru ya uchumi na uwekezaji.

“Serikali ya awamu ya nane tumejipanga na kukifanya Kisiwa cha Pemba kuwa kituo maalumu cha uwekezaji wa miradi mbalimbali itakayosaidia kuongeza ajira kwa vijana,” alisema Dk Mwinyi.

Aidha alisema mafanikio hayo yatakuja kama wananchi wataendelea kudumisha amani na utulivu uliopo sasa ambao umesaidia kufungua milango ya wawekezaji kuonesha nia ya kuwekeza.

Aliwataka viongozi kuwaasa vijana wao kuacha kuchukua sheria mikononi mwao kwani matukio hayo yanaweza kusababisha vurugu na kuhatarisha amani ya nchi iliopo ambayo ni ya kupigiwa mfano.

Kwa mfano alisema ibada ya hijja inatoa mafunzo mengi kwa Waislamu pamoja na watu wengine ambayo ni tabia ya kukaa pamoja kushirikiana bila ya ubaguzi kwa makabila mbalimbali ulimwenguni.

''Hayo ndiyo mafunzo makubwa yanayopatikana katika ibada ya hijja nchini Makka, Waislamu mbalimbali hukusanyika pamoja na kufanya ibada hiyo bila ya kujali tofauti zao zinazotokana na rangi au kabila,” alisema.

Hata hivyo Dk Mwinyi aliwataka Waislamu na waumini wengine nchini kutokata tamaa kutokana na kushindwa kuhudhuria ibada mbalimbali ikiwamo ya hijja nchini Makka kwa mara ya pili mfululizo kutokana na matatizo yaliyojitokeza ya ugonjwa wa virusi vya corona (Covid-19).

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilikuwa tayari imekamilisha masharti yote iliyotakiwa kutekelezwa na Serikali ya Sauda Arabia kwa mahujaji watarajiwa ikiwemo kupata chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa corona.

Hata hivyo wakati serikali ikitayarisha kukamilisha taratibu muhimu Serikali ya Sauda Arabia ilitoa taarifa nyingine na kupiga marufuku mahujaji wa nchi nyingine kuhudhuria ibada hiyo ikiwa ni sehemu ya tahadhari ya ugonjwa wa Covid 19.

“Nawaomba Waislamu waliokuwa wamejitayarisha kutekeleza ibada ya hijja nchini Makka wasikate tamaa kutokana na kuahirishwa kwa mara ya pili mfululizo...taasisi zinazosafirisha mahujaji watunze fedha zao,” alisema.

Mapema Dk Mwinyi alivitaka vyombo vya ulinzi kuhakikisha vinapambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia pamoja na dawa za kulevya ambavyo vimekuwa vikisababisha kuleta athari kubwa kwa jamii.

Alisema atahakikisha taasisi zilizokabidhiwa majukumu hayo ikiwemo Tume ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya wanawachukulia hatua kali wahusika pamoja na kuziba mianya yote inayopitisha dawa hizo ikiwemo bandari bubu.

“Yapo mambo mawili yananikosesha usingizi kila siku ambayo ni udhalilishaji wa kijinsia pamoja na wimbi la dawa za kulevya....tutahakikisha tunarekebisha sheria mbalimbali kuona tunawadhibiti wahusika,” alisema.

Mapema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman alimpongeza Rais Dk Mwinyi kwa kuonesha nia ya dhati ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar kwa kuwaunganisha katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

“Mheshimiwa tunakupongeza kwa dhati kwa kazi kubwa ya kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar na sasa wamejipanga wakisubiri maendeleo ya uchumi wa bluu,” alisema.

Baraza la Eid limehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa kitaifa akiwemo makamu wa kwanza wa rais Othman Masoud Othman,makamu wa pili wa rais Hemed Suleiman Abdalla pamoja na viongozi wastaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/541d34bf288e62de58328e0daeeb3e88.jpeg

MKUU wa Chuo cha Uhasibu Arusha ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Pemba

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi