loader
Dstv Habarileo  Mobile
Waitara: Acheni kupitisha mifugo katika barabara

Waitara: Acheni kupitisha mifugo katika barabara

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara amewataka wananchi wa vijiji vya Sale na Masusu vilivyopo wilayani Ngorongorona kwingine kote nchini, kuacha mara moja kupitisha mifugo katikati ya barabara ili kuepusha uharibifu wa tabaka la lami inayojengwa.

Amesema kupitisha mifugo katikati ya barabara zikiwamo zinazojengwa kunarudisha nyuma shughuli za kiuchumi sanjari na kuharibu tabaka la lami linalomwagwa.

Waitara aliyasema hayo katika ziara ya ukaguzi wa barabara eneo la vijiji vya la Sale na Masusu wilayani hapa inapojengwa barabara hiyo kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 420 na ikigharimu Sh bilioni 87 kwa awamu ya kwanza inayejengwa kilomita 49.

Vipande vitatu vilivyobaki vinasubiri mkandarasi atakayechaguliwa na serikali kwa ajili ya kuendelea na ujenzi hadi kufikia Mto wa Mbu.

Barabara hiyo ya Mto wa Mbu hadi Loliondo eneo la Waso -Sale inajengwa kwa kiwango cha lami huku serikali ikiwa imetoa Sh bilioni 87 .126 kwa ajili ya ujenzi huo.

Alisema ujenzi wa barabara hiyo unatokea eneo la Musoma, Nata, Sansate kupitia Mgumu hadi Mto wa Mbu utafungua fursa ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na eneo la Ngorongoro.

Alisema endapo wananchi wataendelea kupitisha mifugo katika tabaka la lami, mifugo hao watabomoa na kuleta hasara.

Mkandarasi ambaye ni kampuni ya M/s China Wuyi Co. Ltd ameomba kuongezewa muda hadi Aprili mwakani ili kukamilisha kazi hiyo.

Naibu waziri huyo alisisitiza kazi zisizo za kitaalamu katika maeneo yanayopitiwa na mradi, wapewe kipaumbele wananchi wanaohitaji kuzifanya.

Alitoa rai kwa viongozi wa vijiji kuzungumza na wakandarasi wanaojenga miundombinu mbalimbali ili wanaojenga kambi za muda, wazijenge kwa kiwango bora na imara ili wanapomaliza miradi ya kimkakati, majengo hayo yatumike kwa huduma za zahanati, vituo vya polisi na huduma nyngine za kijamii.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwala, aliwataka wafugaji kuheshimu vibao vilivyowekwa na Wakala ya Barabara Mkoa wa Arusha (Tanrods) na kuahidi kufuatilia suala la ajira kwa wananchi walio katika maeneo jirani na ujenzi wa mradi wa barabara ya Sale hadi Waso ili kuondoa urasimu.

“Mradi huo ukikamilika utafungua fursa ya maendeleo kwa wananchi wa wilaya hii hivyo pia, naomba mzingatie sheria sambamba na kuacha tabia ya wizi wa mafuta maana Ngorongoro tunahitaji barabara ya lami na hiki ndicho kipaumbele chetu Wanangorongoro,” alisema.

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Arusha, Reginald Massawe, alisisitiza kumsimamia vema mkandarasi huyo ambaye kwa sasa amefikisha asilimia 81 ya ujenzi wa barabara hiyo kwa awamu ya kwanza.

Alitoa rai kwa Mangwala kuhakikisha wananchi wanapewa elimu ya matumizi ya barabara ili kidhibiti vinyesi vya mifugo kuzagaa juu ya barabara inayojengwa eneo hilo.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Zaitun Swai, aliiomba barabara hiyo ikamilike kwa wakati na kupunguza kero kwa wananchi wa wilaya hiyo hasa wanawake wakiwamo wajawazito wanaopata shida na kuhitaji huduma za kujifungua na nyingine zinazohusu uzazi.

foto
Mwandishi: Veronica Mheta, Ngorongoro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi