loader
Dstv Habarileo  Mobile
Ushahidi kesi ya Sabaya kuendelea leo

Ushahidi kesi ya Sabaya kuendelea leo

KESI ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai ole Sabaya(34) na wenzake wawili ya unyang’anyi wa kutumia silaha na uporaji wa mali na fedha zaidi ya Sh 3,159,000, inaendelea leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha.

Shahidi wa nne katika kesi hiyo, Hajirini Saad Hajirini (32) anaendelea kutoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mfawidhi, Adiro Amworo aliyekuja Arusha akitokea Geita maalumu kusikiliza kesi hiyo yenye mvuto kwa wakazi wengi wa Mkoa wa Arusha.

Sabaya na wenzake wawili, Silyvester Nyengu(26) na Daniel Mbura(38) wanatuhumiwa kutenda makosa hayo yaliyofanyika Februari 9 mwaka katika duka la Shahiid Store linalomilikiwa na mfanyabiashara maarufu Arusha, Mohamed Saad lililopo Mtaa wa Bondeni katikati ya Jiji la Arusha.

Hajirini mwisho wa wiki hakumaliza kutoa ushahidi wake wakati akiongozwa na Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula. Awali alidai kuwa, Sabaya na walinzi wake binafsi walikuwa dukani Februari 9 mwaka huu na waliteka watu na kuwatisha na baadaye kuwapekua, kuwapiga na kuwapora mali na fedha.

Hajirini alidai Sabaya.aliyekuwa kiongozi wa kundi hilo la utekaji, alikuwa akiamrisha watu kupigwa, kuporwa mali na fedha na kuwatisha wahudumu wa duka hilo pamoja na yeye kuwa duka hilo linauza bidhaa bila kutoa risiti na kufanya biashara haramu ya kubadilisha fedha za kigeni. Hajirini alikuwa akisema hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mkoa wa Geita, Adiro Amworo anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Mkoa wa Arusha.

Alidai alikwenda dukani hapo na kumkuta Sabaya akiwa na kundi la walinzi na alipomuuliza kulikoni Mkuu wa Wilaya alimjibu kuwa anamhitaji mmiliki wa duka hilo la Shahiid Store, Mohamed Saad kwa sababu anafanya biashara bila kufuata utaratibu wa serikali ikiwemo kuuza bidhaa bila kutoa risiti na kubadilisha Dola za Marekani.

Shahidi huyo alipoulizwa kama yeye ndiye Saad na mmiliki wa duka hilo alipojibukuwa si mmiliki wa duka hilo ila alipigiwa na ndugu yake Ally Saad aje kujua tatizo ghafla Sabaya aliamrisha walinzi wake wampige.

Alisema walinzi hao walifanya hivyo na kumpekua na kumweka chini ya ulinzi. Alipoulizwa kama aliwahi kumwona Sabaya, alikiri kumwona katika televisheni na kusikia habari zake kutoka kwa wafanyabiashara kuwa ni mtu hatari sana kwa kukomesha watu, hivyo hakusita kumtambua na alikwenda mahali alipokaa na kumshika bega kumtambua kuwa yeye ni Sabaya mbele ya Hakimu Amworo.

Shahidi alidai kuwa baada ya muda mfupi, Diwani wa Kata ya Sombetini, Bakari Msangi, alifika kwenye duka hilo kwani alipigiwa simu na Ally Saad ndugu wa Mohamed Saad ili aende dukani kujua tatizo lililopo dukani kwake, naye alikaribishwa kwa kipigo na kupekuliwa na walinzi wa Sabaya.

Katika kesi hiyo mashahidi kumi wanatarajia kutoa ushahidi wao.

foto
Mwandishi: Na John Mhala, Arusha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi