loader
Dstv Habarileo  Mobile
Chanjo ni Salama acheni imani potofu

Chanjo ni Salama acheni imani potofu

JAMII imetakiwa kuachana na imani potofu kuhusu chanjo za kudhibiti mlipuko wa Covid 19 kuwa sio salama, na kwamba  mtu akichoma anafariki baada ya miaka miwili au kushindwa kuzaa, madai hayo si sahihi na yanalenga kupotosha jamii.

Hayo yamesemwa leo na Muhadhiri Mwandamizi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tafiti na Machapisho kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Bruno Sunguya,  katika Kongamano la tisa la Kimataifa la Watafiti  wa magonjwa mbalimbali ya binadamu kutoka ndani na nje ya nchi, lenye kauli mbiu ‘Fursa na Changamoto Katika Mapambano dhidi ya magonjwa na changamoto Mpya za Afya zinazoibuka,’

Dk Sunguya alisema kumekuwa na imani potofu nyingi kuhusu chanjo na kuwataka wananchi wanaopata fursa ya kuchoma chanjo wachome bila hofu kwani chanjo hizo ni salama na zinadhibiti kwa kiasi kikubwa ugonjwa huo ambao mpaka sasa umeshauwa watu takribani milioni nne duniani huku watu milioni 191 wakiwa wanaugua.

“Kuna dhana potofu kuhusu chanjo, na si hapa Tanzania tu hata nchi nyingine za wenzetu kuwa ukichomwa utakufa, mara unaenda kubadili vinasaba, huzai na kwamba ugonjwa haupo,  ugonjwa upo ni mbaya na umeaua watu wengi.” alisema Dk Sunguya

Alisema hata barakoa zilipoingia nchini kwa mara ya kwanza kulikuwa na maneno mengi ya kupotosha kuwa zinaleta maambukizi.

 Aidha alisema afua mbali mbali za kujikinga zinapaswa kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuvaa barakoa, kuepuka misongamano isiyo ya lazima na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni ili kudhibiti maambukizi hayo.

Kwa upande wa Makamu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi Muhimbili (MUHAS)  Profesa Andrea Pembe, akizungumzia Kongamano hilo ambalo linajikita zaidi kwenye utafiti dhidi ya Covid 19 alisema  Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa na ugonjwa huo na kwamba matokeo ya tafiti mbalimbali yamesaidia kupunguza makali ya ugonjwa huo katika kujikinga, kujitibu na kuzuia athari za muda mrefu za ugonjwa huo na kwamba kati ya afua  mbalimbali za afya chanjo imeonesha matumaini ya kudhibiti ugonjwa huo.

Hata hivyo, alisema changamoto mbalimbali zimeonekana ikiwemo upatikanaji, ubora, dhana potovu, imani na usambazaji wa chanjo hizo.

Kauli za wataalamu hao wa tafiti zimekuja ikiwa ni siku mbili tangu Tanzania ipokee chanjo milioni moja aina ya Johnson & Johson   ikiwa ni mpango wa kukabiliana na maambukizi ya Corona wa Shirika la Afya duniani WHO Covax ili kukabiliana na janga hilo.

Chanjo hizo zitatumika na mahujaji, wafanyakazi wa afya, wale wa huduma za hoteli, wafanyakazi wa balozi na wagonjwa wa corona.

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi