loader
Vyama visafishe katiba zao kabla ya kung’ang’ania ya nchi

Vyama visafishe katiba zao kabla ya kung’ang’ania ya nchi

JUNI 28, 2021 wakati akizungumza na wahariri na wandishi wa habari Iluku Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu alisema anatambua umuhimu mkubwa wa katiba mpya nchini sambamba na mikutano ya hadhara ya vyama vyote vya siasa vya upinzani, na hata chama tawala; Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Rais akasema anatambua umuhimu wa mambo hayo, lakini anawaomba Watanzania wampe muda ili aimarishe nchi kiuchumi kwanza.

Kauli hii ilipokewa na Watanzania kwa ‘mikono miwili’ na kuungwa mkono kwa kuwa wanajua nchi ikiimarika kiuchumi, ni rahisi kuimarika katika nyanja nyingine zikiwamo za kidemokrasia hasa katika nchi zenye vyama makini vya siasa na viongozi makini wasio na tamaa za mali wala madaraka.

Hili ndilo liliwafanya Watanzania ndani na nje ya Tanzania, ndani na nje ya CCM yaani katika vyama mbalimbali vya upinzani, kujitokeza na kumpongeza Rais kwa mwono na mwelekeo huo mzuri unaopanga mambo kwa mujibu wa vipaumbele yaani mambo ya LAZIMA kwanza, kisha yafuate mambo ya MUHIMU.

Suala la kuimarisha nchi kiuchumi kwa yeyote mwenye akili timamu na matashi mema kwa nchi, ni la LAZIMA hivyo, linapaswa kupewa kipaumbele kama alivyosema Rais Samia, kisha yafuatie mambo mengine kama katiba mpya na mikutano ya hadhara ya vyama ambayo ni muhimu, lakini si ya lazima kwa sasa.

Siku zote jambo la lazima, lazima lishughulikiwe kwanza, kisha yafuate mambo ya muhimu.

Hivi sasa Rais Samia aliyeingia madarakani Machi 19, mwaka huu akianza kulisimamisha taifa kiuchumi kupitia mambo mbalimbali muhimu kama kujenga mazingira rafiki zaidi ya uwekezaji, kuondoa utitiri wa kodi na tozo zinazowadhulumu au kuwaumiza Watanzania na kuongaza mapambano dhidi ya maambukizi ya janga la virusi vya corona, ili Watanzania wawe hai, salama na wazima wa afya.

Hata hivyo wakati hayo yanafanyika, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeanza kuwawekea Watanzania vigingi ili ‘wasivuke mto salama.’ Katu hili si jambo jema.

Julai Mosi, mwaka huu wakati akifungua Kongamano la Katiba Mpya, Tabata jijini Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kitaifa wa Chadema, Freeman Mbowe, aliushangaza umma aliponukuliwa akisema Chadema hawako tayari kumpa muda Rais Samia ili ajenge na kuimarisha nchi kiuchumi, badala yake wanataka aache hayo, aende katika katiba mpya.

Mbowe akazidi kuushangaza umma hasa wakati huu ambao Watanzania wanamuomba Mungu huku wakifuata maelekezo ya viongozi na wataalamu wa afya dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona, eti yeye anawataka wanachama wa Chadema wajiandae kwa mikutanao ya hadhara eti katika siku itakayotangazwa.

Hii inaonesha namna ambavyo Mbowe anapenda kuwaburuza WanaChadema ili waishi kama bundi ambaye wakati wanyama na ndege wengi wakitembea na kufanya shughuli zao mchana, bundi yeye analala na wanapolala wengine usiku, yeye bundi anaamka na kuzurura na ndiyo maana anahusishwa na imani za ushirikina.

Ninasema hivi kwa kuwa wakati Watanzania wakihimizwa kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima hata katika mazishi (misiba) na sherehe zikiwamo za harusi, Mbowe yeye anataka Watanzania walundikane kwenye mikutano ya hadhara; labda anataka corona iwatafune zaidi eti kwa kisingizio cha kutafuta katiba mpya.

Wakati Watanzania wanamuunga mkono Rais Samia, wakimwombea na kumsaidia afikie lengo lake la kuijenga nchi kiuchumi, Mbowe yeye bila aibu katika kongamano hilo ananukuliwa akisema: “Hatuko tayari kumpa Mama (Rais Samia) muda….”

Hii ni ajabu kwelikweli kwa kiongozi wa chama kama yeye siku zote kutaka kupotosha umma kwa kuwaamrisha wanachama wake: “myumaa greuka!” dhidi ya maendeleo na usalama wao; ajabu kwelikweli.

Juni 29, mwaka huu, Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Ujerumani (DW) iliwanukuu wachambuzi kadhaa wa masuala ya kisiasa wakisema, kuna haja kubwa kwa Watanzania wote kumpa nafasi (muda) Rais Samia ili akamilishe aliyoyawekea kipaumbele kwa manufaa ya taifa.

Wakasema wazi kuwa, katika kipindi cha siku 100 za kuwa kwake madarakani, amefanya mengi makubwa na mazuri yaliyotazamwa awali kama ni ukiukaji wa haki za raia, demokrasia na hata uchumi kwenda kombo.

Mmoja wa wachambuzi hao wa siasa na diplomasia, Saidi Msonga, alinukuliwa na DW akisema, kila kitu hakiwezi kufanyika kwa usiku mmoja, hivyo Rais Samia apewe muda.

Tangu aingie madarakani mwezi Machi mwaka huu, Rais Samia amekuwa akikutana na makundi mbalimbali katika jamii nchini na kuainisha vipaumbele vya serikali yake na pia, kusikiliza maoni ya makundi hayo.

Miongoni mwa makundi aliyokutana nayo hadi sasa na kuzungumza nayo ni pamoja na wazee, viongozi wa dini, wanawake, wafanyabiashara, vijana na watendaji wa sekta ya habari.

Kimsingi, maajabu ya kiuongozi yanayooneshwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani nchini, ndiyo yamewasukuma hata wanachama wa Chadema kusema wazi juzi kuwa, suala la mabadiliko ya Katiba mpya Tanzania si ajenda yao kwa sasa, bali wanachokata ni mabadiliko ya katiba ya chama chao na ujenzi wa chama kuanzia ngazi ya shina.

Wakiongozwa na Mkuu wa Data Kanda ya Mashariki wa Chadema, Macdeo Shilinde na Katibu wa Chadema Temeke, Martin Kalugendo, wanasema madai ya katiba mpya yaliyozushwa n Mbowe si ajenda yao kwa sasa.

 “Unapotaka kufanya jambo jema na zuri, anzia nyumbani, sisi wajumbe wa Baraza Kuu la Chadema na wanachama tumeona kuna mapungufu makubwa kwenye chama chetu, Mwenyekiti kaibuka na ajenda ya kudai mabadiliko ya katiba mpya ya nchi, wakati si ajenda ya chama chetu kama ambavyo Kamati Kuu iliridhia na kuleta kwenye Bazara Kuu; na tukaamua tuanze kujenga chama kuanzia ngazi ya shina,” anasema Shilinde.

Alisema kama ni kudai katiba mpya, Chadema kingeanza kufanya maboresho katika katiba yake kwa sababu ina upungufu mkubwa ukiwamo suala la muda wa kukaa madarakani kwa mwenyekiti wa chama hicho na suala la mapato na matumizi ya fedha ya chama.

“Katiba yetu ina udhaifu mkubwa sana, imempa mwanya mwenyekiti kuwa wa milele. Nawasihi chama changu kitu tunachokwenda kukifanya si sahihi, tujitahidi kurudi kwenye majadiliano kwanza ya kwetu tuone katiba yetu imekaaje ili tunapowashawishi wananchi kudai katiba mpya ya nchi, tuwe mfano,” alisema Shilinde.

Naye Katibu wa Chadema Temeke, Kalugendo akasema: “Rais Samia Suluhu Hassan ni msikivu, alishasema jambo la katiba mpya atalifanyia kazi; tumpe muda, leo hii hata muda hatujampa Mwenyekiti wetu ‘anafosi’ (analazimisha) kudai katiba mpya ya nchi, huyu huyu waliambiwa wakajadiliane mustakabali wa nchi na wenzake wa vyama vingine, akagoma, ana mambo binafsi kuliko maslahi mapana ya chama.”

Kimsingi, watu mbalimbali wanasema kinachofanywa na baadhi ya wanasiasa ni dalili za wazi kuwa hawapendi maendeleo wala utulivu wa nchi, bali wanataka chokochoko ili wanapokataliwa na umma, wakimbie kutafuta huruma kwa ‘wajomba.’

Kubwa zaidi walilolibaini Watanzania wengi ni kwamba, wanaong’ang’ania katiba mpya wanafanya hivyo kutafuta mianya ya wao kuwa madarakani kwa muda mrefu na hata kupewa vyeo na si kwamba wanadai katiba mpya kwa manufaa ya umma.

Hivi katiba mpya kwa wenye njaa ina faida gani; ndiyo maana ninasema, vyama vijenge na kuboresha demokrasia na katiba zao kwanza, kabla ya kung’ang’ania katiba mpya ya nchi.

Viondoe ubabe na unyanyasaji unaoliliwa na kulalamikiwa kila kukicha na hata unyanyasaji wa namna mbalimbali ukiwamo wa kijinsia huku vikikumbuka kuwa, huwezi kufanya mapinduzi ya kuondoa sultani, wakati wewe mwenyewe unaendeleza usultani wa aina nyingine.

MUNGU IBARIKI TANZANIA.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/395c0e6a40ca2401e49275a8831d5dcb.JPG

NIPO nyumbani kwa Baba na Mama Chichi. ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi