loader
Dstv Habarileo Mobile
Serikali yachukua hatua kupunguza riba ya mikopo

Serikali yachukua hatua kupunguza riba ya mikopo

SERIKALI imechukua hatua za kisera kwa ajili ya kuongeza upatikanaji mikopo kwa sekta binafsi na kupunguza viwango vya riba isizidi asilimia 10.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga alisema hayo jana alipokuwa akizungumzia na waandishi wa habari kuhusu mikakati ya serikali kuongeza ukwasi kwenye sekta binafsi.

Alisema ili kutoa msukumo wa kuongeza kasi ya utoaji mikopo kwa sekta binafsi na kupunguza riba, BoT imeamua kutekeleza hatua za kisera kuanzia jana.

"Hatua hizi za kisera zimechukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, Sura ya 197 na Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa, Sura ya 437," alisema.

Profesa Luoga alisema ili kuongeza ukwasi katika sekta binafsi, serikali imepunguza kiwango cha sehemu ya amana za mabenki kinachotakiwa kuwekwa BoT.

"Benki Kuu imetoa unafuu kwa benki za biashara kwa kupunguza kiwango cha kisheria cha amana ambacho benki na taasisi za fedha zinatakiwa kuweka Benki Kuu ikiwa ni sehemu ya kutekeleza sera ya fedha. Nafuu hii itatolewa kwa benki itakayotoa mikopo kwa sekta ya kilimo kulingana na kiasi cha mkopo kitakachotolewa,” alisema. 

Profesa Luoga alisema benki itakayonufaika itatakiwa kutoa mikopo kwa sekta ya kilimo kwa riba isiyozidi asilimia 10 kwa mwaka. 

"Hatua hii inalenga kuongeza mikopo katika sekta ya kilimo na kupunguza riba katika mikopo itakayotolewa," alisema.

Alisema hatua nyingine, BoT imeondoa sharti la uzoefu wa kufanya biashara kwa angalau miezi 18 kwa waombaji wa biashara ya wakala wa benki na badala yake watatakiwa kuwa na kitambulisho cha taifa.

"Pia tumeangalia masharti ya usajili wa mawakala wa benki ambapo tumeondoa sharti la angalau miezi 18 na badala yake waombaji wa biashara ya wakala wa benki watatakiwa kuwa na Kitambulisho cha Taifa au namba ya Kitambulisho cha Taifa.

Hatua hii  itachangia kuongeza fedha katika mabenki kutokana na ongezeko la amana na kupunguza riba za mikopo,” alisema.

Profesa Luoga alitaja uamuzi mwingine ni kuweka ukomo wa riba kwenye akaunti za kampuni za watoa huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi. 

Alisema BoT pia imeanzisha mfuko maalumu wa kukopesha benki na taasisi za fedha wenye thamani ya Sh trilioni 1 ambao utatumika kukopesha benki na taasisi za fedha kwa riba ya asilimia 3 ili taasisi hizo zikopeshe sekta binafsi. 

Alisema kabla ya utaratibu huo, mikopo inayotolewa na benki za biashara kwa sekta binafsi ilikua kwa asilimia 15, wakati riba za mikopo zilikuwa zikishuka hadi asilimia 17 kutoka zaidi ya asilimia 20, kiwango ambacho ni kikubwa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/808e12eda09cc67ad21c55bc165f28f0.jpg

SHIRIKISHO la Wafanyabiashara na wenye viwanda nchini ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

2 Comments

 • avatar
  Maida Juma
  16/09/2021

  Ni lini nmb itapunguza riba katika kukopesha watumishi wa umma kwani asilimia 17 ni kubwa mno

 • avatar
  Maida Juma
  16/09/2021

  Ni lini nmb itapunguza riba katika kukopesha watumishi wa umma kwani asilimia 17 ni kubwa mno

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi