loader
Dstv Habarileo  Mobile
Ukweli kuhusu chanjo ya corona

Ukweli kuhusu chanjo ya corona

*Ni salama asilimia 99.99

DUNIA ipo katika harakati za kukabiliana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid 19).  Wataalamu wanabainisha kwamba, virusi vya corona vina uwezo wa kubadilika na aina nyingi husababisha magonjwa yasiyo hatari sana upande wa binadamu.

Kutokana na kudhoofika kwa mwili kutokana na mashambulio ya virusi kunafungua milango kwa bakteria wabaya kuvamia na kusababisha maambukizo ya mfumo wa upumuo, kama mafua au homa ya mafua yanayoisha kwa kawaida baada ya siku kadhaa. Lakini kuna pia maambukizo ya hatari kama nimonia inayoweza kusababisha kifo.

Aina hizo za virusi zina uwezo wa kubadilika. Awamu ya kwanza na ya pili ya kirusi hicho ilikuwa inashambulia zaidi nchi za Magharibi lakini sasa hali inazidi kuwa mbaya katika wimbi la awamu ya tatu kwa kugusa maeneo yote duniani ikiwemo nchi za Afrika.

Matumaini ya kukabiliana na ugonjwa huo sasa yanaonekana baada ya watalaamu wa masuala ya afya kuja na chanjo takribani 200 zinazoendelea kufanyiwa kazi huku chanjo sita zikipitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Hata hivyo, tangu kuanza kutambulishwa kwa uwapo wa chanjo dhidi ya corona, kumekuwepo na taarifa mbalimbali za kuogopesha kuhusu usalama wake, ikiwemo madai kwamba nyingine zinasababisha vifo na nyingine kuzuia uzazi.

Wakati taarifa hizo zikienea, nchi mbalimbali zimeendelea na mpango wa kuchanja raia wake kwa nia ya kuzuia maambukizi, kupunguza vifo na kupunguza makali ya ugonjwa huo.

Ndani ya miezi minne tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, amechukua hatua kubwa katika kukabiliana na corona kwa kuhakikisha hatua muhimu za kujikinga na ugonjwa huo zinachukuliwa sambamba na kuruhusu chanjo kupatikana nchini.

Alipozungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari hivi karibuni,  Rais Samia alisema: "Kwa hiyo hatua tuliyochukua kwanza tuliamua kwamba twende na ulimwengu tuchanje na tuchanje kwa hiari. Mtanzania anayetaka atachanja na asiyetaka ataangalia kwa nafsi yake.”

Rais aliweka bayana kwamba, Tanzania imeshaijiunga na Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuchagiza upatikanaji wa chanjo (COVAX) kwa nchi za kipato cha chini.

Siku kadhaa, baadaye Tanzania ilitoa mwongozo wa chanjo dhidi ya corona uliobainisha nia ya kuingia aina nne ya chanjo za kipaumbele na utaratibu wa kuzipata.

Chanjo hizo ni pamoja BioNTech/Pfizer BNT162b2, Moderna mRNA 1273, Novavax NVX-CoV2373 na Johnson & Johnson (Janssen) Ad26. Ambapo tayari chanjo ya Johnson imeshawasili na Rais Samia amezindua utaratibu mzima wa kuchanja.

Hata hivyo, ujio wa chanjo hizo umeleta sintofahamu na taarifa nyingi potofu kuhusu usalama wa chanjo hizo za corona, kiasi cha kumuibua Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Profesa Yunus Mgaya.

Profesa Mgaya anawatoa wasiwasi Watanzania kuhusu chanjo zinazotolewa nchini dhidi ya ugonjwa huo akisisitiza kuwa ziko salama kwa asilimia 99.99 na zimethibitishwa na jopo la wanasayansi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO).

Uthibitisho wa chanjo

Anasema hakuna chanjo yoyote duniani inayoruhusiwa kutumiwa na wananchi endapo haijathibitishwa usalama wake.

Anasema mpaka sasa kuna chanjo zaidi ya 200 duniani zilizo kwenye majaribio mbalimbali lakini zilizopitishwa na WHO zitumike chini ya mpango wa dharura, ni sita .

Chanjo hizo nne kutoka Marekani ni BioNTech, Pfizer, Johnson & Johnson, Moderna NIAID na Novavax, kutoka Uingereza na Sweden AstraZeneca, China chanjo mbili ambazo ni Sinovac-CoronaVac na Sinopharm.

Anasema chanjo ya Urusi ya Sputnik V ambayo pamoja na kwamba imeshaanza kutumika kwenye nchi nyingi duniani, inafanyiwa tathmini na WHO, huku Cuba ikitengeneza chanjo inayoitwa Abdala.

Profesa Mgaya anaeleza kuwa chanjo zikipitishwa kwamba zinafaa zitumike ni baada ya si tu ya utafiti bali ni baada ya kujiridhisha na mamlaka mbalimbali kwamba ziko salama kwa matumizi.

“Mfano chanjo inatengenezwa Marekani ni lazima ipitiwe na udhibiti wa Mamlaka za Marekani pia lazima WHO iidhinishe. Hata hii iliyoingizwa Tanzania, hapa kuna mamlaka ikiwemo NIMR, TMDA lakini pia WHO ina kamati zake za kitaalamu zinazokagua mpaka kujiridhisha kitaalamu na kubwa zaidi huangalia usalama na ufanisi,” alisisitiza.

Anasema chanjo sita zilizopitishwa na WHO zote zimefaulu, haziwezi kumdhuru mtu kwamba akinywa atakufa au kuugua. Kiwango cha athari ni kidogo kinachofikia asilimia 0.00004 ikilinganisha na manufaa.

Anakiri kwamba baadhi ya chanjo zilisababisha athari kwa watu wachache lakini si athari kubwa. “Yaani walioathirika ni kati ya milioni moja basi wanne ndio waathirike tena si sana. Athari ni ndogo sana faida ni kubwa,” anasema Profesa Mgaya.

Anataja manufaa ya chanjo hizo za corona kuwa ni pamoja na kupunguza vifo, kuzuia watu kulazwa hospitalini, kupunguza makali ya ugonjwa na maambukizi.

 

Dk Mgaya anasema kwa sasa dunia ina jumla ya watu bilioni 7.4 lakini waliochanjwa ni bilioni 1.5 sawa na asilimia 20 hadi 25 ambao hata robo hawajafikia jambo linaloashiria kwamba bado kuna kazi kubwa ya kudhibiti ugonjwa huo wa Covid 19.

Anasema asilimia kubwa ya watu ambao hawajachanjwa ni kutokana na kutopatikana kwa chanjo hizo kwa kuwa mahitaji ni makubwa kuliko uzalishaji wake.

Wanaosambaza hofu

Akizungumzia wanaosambaza hofu kuhusu matumizi ya chanjo hizo, mkurugenzi huyo anasema kitalaamu katika utafiti, mtu hana haki ya kuongea kama hana data na kwamba data hizo zinapatikana kwenye utafiti.

Anasema chanjo hizo zimehakikiwa na kupitiwa na wataalamu na kuthibitishwa kwa ushahidi wa kitaalamu.

“Nikisema Panadol inapunguza au inaponya maumivu si majaribio au kubahatisha imethibitishwa. Kwenye chanjo pia, ukweli unabaki wa kisayansi kabisa kwamba, ziko salama kwa asilimia kubwa,” anasisitiza.

Mkurugenzi huo anabainisha kuwa chanjo ya Pfizer imeshatumika kwenye nchi 91, Moderna 54, Johnson ambayo imeingizwa Tanzania nchi 53, Sinopharm 56, AstraZeneca 117, Sinovac 33 na Sputnik V nchi 69.

Anaeleza kuwa nchi zote hizo zimeamua kutumia chanjo hizo baada ya kujiridhisha na ushuhuda wa kisayansi uliopo kwamba chanjo zote ni salama kwa kiwango kinachokubalika.

“Chanjo zote au dawa zote zina athari kidogo ila kinachoangaliwa ni faida inayopatikana ikilinganishwa na athari hasi. Athari ya Johnson kwa baadhi ya watu hupata damu kuganda, idadi ilikuwa kwenye milioni moja watu wanne tu sawa na asilimia 0.00004,” anasema.

Anataja nchi zinazotumia Johnson kuwa ni Marekani, Canada, Norway iliyoikataa na sasa imerejea kutumia pamoja na Denmark.

Kuhusu hoja kwamba chanjo hizo si salama kwa kuwa zimetengenezwa kwa muda mfupi, anaeleza kuwa utaratibu wa kawaida wa kutumia teknolojia ya zamani kutengeneza chanjo ilikuwa inatumia mpaka miaka 20 lakini kwa teknolojia ya sasa chanjo zinatengenezwa ndani ya mwaka.

“Kirusi kilipogundulika China watu waliingia maabara na kusoma vinasaba vyake vyote kwa teknolojia ya sasa hiyo ni kazi ya saa mbili tu tofauti na zamani. Na hata teknolojia iliyotumika kutengenezea Pfizer au Johnson zimeshatumika kutengenezea chanjo nyingine ambazo nazo zimetumika vya kutosha na machapisho yapo ya kujiridhisha,” anafafanua.

Anasema katika kufanyia majaribio chanjo ya Pfizer na Johnson zimetumia zaidi ya watu 43,000 na kuthibitisha usalama wake.

Ujazaji fomu

Akielezea kuhusu ulazima wa kujaza fomu kabla ya chanjo, Profesa Mgaya, anashangaa kuona watu wameshtushwa na suala hilo ambalo ni la kawaida katika taaluma ya tiba.

“Leo hii ukienda kufanyiwa operesheni ndugu zako wanajazishwa fomu kama ile. Hata tunapoenda kufanya utafiti kwenye jamii tunakuwa na fomu. Hii ni kitu cha kawaida katika taaluma ya tiba,” anasema.

Rais aongoza kuchanja

Matumizi ya chanjo nchini yalizinduliwa juzi na Rais Samia ambaye amehakikishia wananchi  kuwa chanjo hiyo ni salama na isingekukwa hivyo, asingekubali kuongoza Watanzania kuchanjwa.

Katika hafla hiyo ya uzinduzi wa chanjo ambayo viongozi mbalimbali wa kitaifa pia walichanjwa, Rais Samia anaweka bayana kwamba wapo wanaozikataa na wanaozikubali.

“Nawaambia chanjo ni salama kama si salama…ninachanjwa baada ya kujiridhisha usalama wake. Hao wanaozikataa huenda familia zao au koo zao hazijaathiriwa na janga hili,” ni sehemu ya maneno katika hotuba ya Rais aliyoitoa kwenye hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Licha ya Rais Samia, pia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anasisitiza kuwa serikali haiwezi kuleta kitu kinachoharibu afya ya Watanzania. Pia Waziri a Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima anasema chanjo hiyo isingekuwa salama, asingeweza kumshauri Rais vibaya.

Wakati ugonjwa wa Covid-19 ukiendelea kuwa tishio duniani na hata hapa nchini, Dk Gwajima anawataka Watanzania kupuuza maneno ya watu kuwa chanjo ya Johnson & Johnson si salama.

Kwa mujibu wa mtandao wa Worldometer, takwimu za hadi jana zinaonesha jumla ya watu milioni 195.43  duniani wamepata maambukizi ya corona. Kati ya hao, watu milioni 4.21 wamefariki dunia kwa ugonjwa huo na watu milioni 177.25 wamepona.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/6fd53fcd65c51c2d89a40973674bbfcc.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi