loader
Dstv Habarileo  Mobile
Manula anavyojipanga kutawala Afrika

Manula anavyojipanga kutawala Afrika

AISHI Salum Manula sio jina geni katika masikio ya wapenzi wa mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini kutokana na mchango wake katika timu ya Simba na timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars'.

Kipa huyo ambaye amezaliwa Septemba 13,1995, amekuwa katika kiwango bora tangu alipoanza kucheza soka la kulipwa, ambako hivi sasa amekuwa kipa wa daraja la juu barani Afrika.

Manula alitua Simba mwaka 2017, kwaajili ya kwenda kuziba nafasi ya Daniel Agyei raia wa Ghana, ambaye wekundu wa Msimbazi walikuwa wameachana naye.

Tangu ametua Simba ameisaidia timu hiyo kubeba mataji manne ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Nago za Hisani tatu, makombe mawili ya Shirikisho ya Azam pamoja na kuifikisha timu hiyo hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili.

Katika ngazi ya taifa, Manula ameisaidia timu kufuzu Michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) nchini Cameroun pamoja na michuano ya CHAN kwa wachezaji wanaocheza Ligi ya ndani.

Manula amekuwa mfano kwa vijana wengi wanaochipukia katika soka kutokana na nidhamu yake ya ndani na nje ya uwanja.

Ni nadra sana kumuona Manula akikutana na adhabu kwa kosa la utovu wa nidhamu kutokana na muenendo huo ndio maana kila uchwao ameendelea kuimarika na kuwa chaguo la kwanza katika timu yake na taifa kwa ujumla.

Habari leo limefanya mazungumzo na nyota huyo mzaliwa wa Morogoro ambaye amefunguka baadhi ya mambo muhimu kumuhusu katika karia yake ya soka

SAFARI YA SOKA

Manula alianza kucheza soka tangu akiwa mdogo, ambapo safari yake ilianzia katika timu ya Mtibwa Sugar, ambako hakudumu sana akajiunga na timu ya Azam FC mwaka 2012 akiwa na umri wa miaka 17 tu lakini kiwango alichoonyesha kilikuwa gumzo.

Akiwa Azam FC, ndipo alipoanza kutambulika zaidi kutokana na kiwango chake pale alipopewa nafasi mbele ya mzoefu Mwadini Ali Mwadini ambaye alikuwa katika kiwango bora kwa wakati ule.

Tangu alipoanza kucheza soka Manula amehudumu katika vilabu vitatu pekee Mtibwa Sugar, Azam FC na Simba ambayo yuko nayo hadi hivi sasa.

ALIVUTIWA NA NANI

Mlinda mlango huyo anasema wapo wengi ambao anavutiwa na uchezaji wao, lakini kwa hapa nyumbani kipa ambaye anamuhusudu zaidi ni Juma Kaseja, ambaye anaamini kuwa ni miongoni mwa wachezaji wenye vipaji vikubwa na pia anatumia kujifunza mambo mengi kutokana na uzoefu wake.

Anasema kuwa ubora wa mlinda mlango huyo ndio sababu iliyomfanya adumu katika soka kwa muda mrefu ndio sababu hata yeye amekuwa akijifunza kupitia kwa mkongwe huyo.

KIPA BORA

Licha Tanzania kusheheni walinda mlango bora na wenye vipaji lakini Manula, ameendelea kuwa katika kilele cha ubora wake na kuwa kipa namba moja katika klabu yake na timu ya taifa ya Tanzania.

Manula amekuwa kipa bora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa misimu sita mfululizo akianza msimu wa 2015/16, 2016/17, 2017/18,2018/19,  2019/20 na 2020/21 amekuwa kipa bora tangu akiwa na  Azam FC, ambapo alifanya hivyo mara mbili  na mara nne akiwa na Simba.

Anasema kuwa haya ni mafanikio ambayo hayaji hivi hivi bali ni kutokana na kujituma pamoja na kufuata maelekezo ya kocha.

MICHEZO MIGUMU

Michezo ambayo hawezi kuisahau ni mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar, waliopoteza mbele ya hayati Rais wa Awamu ya Tano, John Pombe Magufuli,  michezo mingine ambayo ilimpa wakati mgumu ni ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya As Vita na Al Ahly, ambayo alipoteza kwa mabao 5-0 kwa  kila mchezo.

Lakini pia michezo mingine iliyompa wakati mgumu ni dhidi ya Yanga, waliopoteza kwa bao 1-0 mzunguko uliopita na msimu huu, ambao pia walipoteza kwa bao 1-0, lakini anafurahi kwakuwa amefanikiwa kuisaidia timu yake kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu na kombe la Shirikisho la Azam.

10 BORA AFRIKA

Manula anasema kuwa kitendo cha kuingia katika orodha ya walinda mlango 10 bora  kimemuongeza morali ya kupambana ili siku moja ashike namba moja kama walinda mlango wengine waliowahi kufanya hivyo kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.

Manula ameingia katika orodha ya walinda mlango 10 bora wa Afrika waliofanya vizuri zaidi katika Ligi ya Mabingwa Afrika, akiwa hajaruhusu wavu wake kuguswa katika michezo minne, hivyo kushika nafasi ya sita jambo ambalo sio dogo.

MALENGO YAKE

Mlinda mlango huyo anasema kuwa baada ya kuwa kipa bora Tanzania kwa muda mrefu sasa akili yake ameihamishia Afrika ambako ndio jicho la wachezaji wengi wanaangalia ili kupata fursa ya kwenda kucheza soka nje ya bara hili lenye vipaji lukuki.

SAFARI BADO

Manula anasema kuwa licha ya kuonekana kama ameimarika zaidi na kupata nafasi katika timu yake na Taifa kwa ujumla,  lakini anaamini kuwa bado ana safari ndefu zaidi ya kuyafikia malengo yake aliyojiwekea tangu akiwa anaanza kucheza soka.

ASICHOPENDA

Manula anasema kati ya mambo ambayo hayapendi basi ni kukatishwa tamaa katika jambo lake ambalo anaamini ipo siku litamfanya azidi kukua kwenye karia yake ya soka.

Nyota huyo anasema anachukizwa pia na tabia ya baadhi ya watu wasiowatakia mema wengine pindi wanapokosea badala yake wanafurahia kutokana na magumu wanayopitia.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/1ab0d44b9e8ece6ebbadafe792c95460.jpg

NYOTA wa zamani wa Yanga, Charles Bonifasi Mkwasa ...

foto
Mwandishi: Martin Mazugwa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi