loader
Dstv Habarileo  Mobile
Aslay Isihaka, Msanii asiyetaka kiki za kijinga

Aslay Isihaka, Msanii asiyetaka kiki za kijinga

UNAPOZUNGUMZIA wanamuziki   ambao wamekuwa wakifanya vizuri zaidi kwenye muziki wa kizazi kipya bila ya kutumia skendo au kujidhalilisha kwaajili ya kupata umaarufu, hutaacha kumtaja Aslay Isihaka ambaye anaamini kwenye kazi nzuri.

Aslay ambaye ni zao la Kituo cha Mkubwa na Wanawe, ambacho kipo chini ya Saidi Fella ‘Mkubwa Fella’, kwa sasa yupo chini ya lebo yake mwenyewe ya Dingi Mtoto akijiita jina la African Kid  amekuwa akiamini zaidi katika nyimbo nzuri na bora.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Aslay alisema katika kuthibitisha ubora wa kazi yake kwa mwaka wamekuwa wakitoa nyimbo zisizopungua 20, ili kuwapa nafasi mashabiki wachague kile, ambacho wanakipenda kupitia nyimbo zake.

Anasema  kupitia nyimbo zake ambazo hana muda wala wakati wa kusema ndiyo azitoe,  kwakuwa hatizami  nani ametoa wimbo kwa wakati huo au kuna mashindano gani, anachoangalia ni muda huo ni sahihi na mashabiki wanahitaji kazi mpya.

Anasema kwa mwaka huu hadi sasa tayari ametoa nyimbo zaidi ya tano ikiwemo ule wa Nashangaa, Kilanga Komo, Kasema na sasa wimbo wa Shangingi ambao umekuwa ukifanya vizuri kwenye mitandao ya kijamii na radio.

“Nimekuwa nikiamini katika nyimbo nzuri, natarajia mashabiki wangu wanaridhika na kile ambacho wanakipata kutoka kwangu,” anasema.

Aslay anasema katika nyimbo nyingi ambazo amekuwa akizitoa ameimba peke yake, lakini kwa sasa anajiandaa na ujio wa nyimbo ambazo ameshirikiana na wasanii tofauti tofauti kutoka ndani na nje ya nchi.

Katika nyimbo amabazo anatarajia kuzitoa kabla ya kufunga mwaka, zipo zile ambazo ameshirikiana na wanamuziki wakubwa, akiwemo  Hamisi Mwijuma  ‘Mwana Fa’, Baraka Da Prince , Temba, Chege lakini pia kuna nyimbo anatarajia kufanya na Enock Bela, Beka Flevour na Mboso, ambao wote alikuwa nao katika Yamoto Band.

Anasema lakini pia yupo kwaajili ya kupambana na soko la kimataifa, ambapo tayari ameshaongea na wasanii kutoka nje ya nchi kama Kenya, Congo, Nigeria pamoja na mwanamuziki kutoka katika nchi ya Ufaransa,  ambaye tayari wameshamaliza mazungumzo.

“Mwakani nahitaji nije tofauti kwa kufanya kazi na watu zaidi kuliko kazi zangu, nategemea kufanya kazi na watu wa nje pia,” anasema.

Aslay alisema tayari ana mikakati mikubwa kutoka katika lebo yake anayoimiliki ya Dingi Mtoto, ambayo ofisi zake zipo Mikocheni jijini Dar es Salaam, na ana wasanii zaidi ya 10 na tayari wanafanya mazoezi.

Anasema lengo la kuunda lebo hiyo ambapo ndani yake zipo studio tatu za kurekodi muziki, anahitaji kusaidia wasanii wenzake, ambao wengi wao alitoka nao katika kituo cha Mkubwa na Wanawe.

Aslay anasema kwa sasa amekuwa akipata mialiko mingi ya kwenye matamasha, lakini amekuwa akiangalia zaidi maslahi kwakuwa video zake anatengeneza kwa fedha nyingi, ikiwemo eneo la kutengenezea video, mavazi, pamoja na miundo mbinu mingine.

Anasema amekuwa akiulizwa sana kutoonekana katika matamasha ya Wasafi, ambayo yamekuwa yakiandaliwa na lebo ya WCB na kusema  inatokana na kutoitwa katika matamasha hayo.

“Mimi nipo tayari kwa tamasha lolote, ila lazima mtu anaiite tukubaliane ni kiasi gani ndipo nikubali kufanya tamasha lake” alisema.

Anasema zaidi ya matamasha hayo, lakini yupo mbioni kuandaa tamasha na mwanamuziki Faustine Charles ‘Nandy’ ambaye wamefanya nyimbo zaidi ya tatu  kwa pamoja, ambapo waliwahi kufanya tamasha kwa pamoja Escape One na kujaza.

Ingawa na changamoto zote, ambazo amekuwa akipitia katika muziki, anasema hana mtu yoyote anayemsaidia katika muziki wake tofauti na baadhi ya watu wanavyoongea kwamba kituo cha radio kinamsaidia katika muziki wake.

Asema hana ugomvi na kituo chochote, kwakuwa anaamini kila kitu anachokifanya anakifanya kwa upendo na amani, hivyo kuungwa mkono na kituo chochote hiyo ni kawaida sababu anafanya kazi nzuri.

“Mimi siamini kwamba kuna kituo, ambacho kinanisaidia katika kuhakikisha muziki wangu ufike mbali, ila uwezo wangu pamoja na heshima ndiyo maana nafika mbali” alisema.

Alisema kwa sasa yupo chini ya uongozi wake, ambao ni Meneja Yusufu Chambuso, lakini pia anashirikiana na mameneja wengine wawili, akiwemo Mwaseba Water.

Aslay ameendelea kushika nafasi mbalimbali katika mitandao ya kijamii, ambapo anaendelea kushika nafasi kati ya wanamuziki 10 bora wanaofanya vizuri katika mitandao ya kijamii.

Lakini zaidi ya hapo, Aslay ni miongoni mwa wanamuziki wachache, ambao video zao zimekuwa zikifikisha idadi kubwa ya watazamaji kiasi cha kufikia watazamaji milioni moja katika baadhi ya nyimbo zake.

Nyimbo kama Natamba ina jumla ya watazamaji milioni 12, Angekuona ina watazamaji milioni 11, Mateka milioni  2, huku nyimbo zote akiwa yupo peke yake jambo ambalo linaonesha wazi kwamba ameweza kudumu katika maisha yake ya kimuziki.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/8f129dd1a4daf8f8c7b4a276f5f5c29b.jpg

NYOTA wa zamani wa Yanga, Charles Bonifasi Mkwasa ...

foto
Mwandishi: Mohamed Mussa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi