loader
Mkojani,  Sanaa haijamnufaisha chochote

Mkojani, Sanaa haijamnufaisha chochote

MKOJANI  hili ni  jina la msanii wa vichekesho, ambalo kwa siku za karibuni limekuwa maarufu sana kutokana na vituko vyake pamoja na maudhui ya kazi zake.

Abdallah Mohamed Nzunda ndio jina halisi la msanii huyo, ambaye anasema pamoja na umaarufu wake wote, lakini kazi hiyo haijabadilisha maisha yake zaidi ya kujulikana na watu pamoja na kupata pesa ya kula na kulipia pango.

Msanii huyo anasema wasanii wengi nchini wanapotea sababu kubwa ni masharti magumu, ambayo yamewekwa na serikali kitu ambacho kinasababisha watu hao kutafuta kazi nyingine ya kufanya na siyo sanaa ambayo ndiyo kipaji chao.

Mkojani anasema hata yeye ameamua kubadili staili ya uigizaji wake kutokana na ugumu uliopo kwenye uuzaji wa filamu tofauti na vichekesho, ambavyo vinamfanya mtu kutumia muda mfupi na kuendelea na kazi zake nyingine.

“Hii kazi tunafanya kama hobi sababu tunaipenda, lakini mazingira ya muigizaji wa Tanzania ni magumu na hayafanani na mcheza mpira wala mwandishi wa taifa lolote la nje, tofauti na hapa nchini kutokana na vikwazo ambavyo amewekewa ili kuonja mafanikio,”

“Mfano mzuri ni marehemu Amri Athuman ‘Mzee Majuto’ aliyefariki miaka mitatu iliyopita, ambapo licha ya uwezo na umaarufu mkubwa aliokuwa nao katika uigizaji, lakini amekufa akiwa maskini hapo utaona kwamba msanii wa taifa hili siku zote atabaki kuwa masikini mpaka anastaafu,” anasema Mkojani.

CHANGAMOTO HIZO

Msanii huyo anasema  ukiachana na tozo za Serikali, ambazo zinawaweka katika wakati mgumu kwenye usambazaji wa kazi zao, lakini changamoto nyingine inayowakwamisha wasanii ni wahariri wa kazi zao ambao wanawadhulumu kazi zao.

Mkojani anasema wahariri wengi wa kazi za wasanii hukimbia na kazi za wasanii wengi pindi wanapo wapelekea studio kwa ajili ya kuzihariri na baadaye huzigeuza kuwa zao jambo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa kuwarudisha nyuma wasanii wengi hasa chipukizi.

Anasema vitendo hivyo vinafanyika kila leo kwenye tasnia yao na mbaya zaidi hakuna wa kuvipigia kelele kitu ambacho kina sababisha wasanii wengi wenye vipaji kuchukua maamuzi ya kuachana na tasnia hiyo na kufanya shuhuli nyingine.

“Ni matatizo kila sehemu ndio maana nikikwambia kazi hii ya sanaa tunafanya kama hobi kwasababu tunaipenda, lakini kuna ukiritimba mwingi na ukweli hatuna pakusemea sababu hata hao Serikali siyo kwamba hawajui adha tunazokumbana nazo huku, lakini wako kimya,” anasema Mkojani.

KOMEDI BADALA YA FILAMU

Mkojani anasema ameamua kuachana na filamu sababu amegundua kwake binafsi hazimlipi kutokana na gharama na kipato kidogo, ambacho wanaingiza kupitia kazi hizo.

Msanii huyo anasema hiyo ndio sababu kubwa ya kumfanya ajikite zaidi kwenye vichekesho sababu amegundua zina mashabiki wengi, ambao wanazifuatilia tofauti na filamu, ambazo zinamuhitaji mtu kutumia muda mwingi kuiangalia na kuelewa.

“Tangu zamani nilikuwa nikifanya vyote filamu na vichekesho, lakini siku za hivi karibuni niliamua kujikita zaidi kwenye vichekesho sababu kwanza natumia muda mfupi, lakini kingine situmii gharama kubwa na watu wanaona kwa urahisi kupitia YouTube,  na kingine hata mtazamaji anatumia muda mfupi  hazizidi dakika 10,” anasema Mkojani.

USHINDANI KWENYE KOMEDI

Msanii huyo, ambaye amejipambanua kwamba aliingia kwenye sanaa ya kuigiza kutokana na ushawishi wa marehemu  Amri Athuman ‘Mzee Majuto anasema kwake anachukulia kama hamasa ya kumfanya alale na kuumiza kichwa ili kutoka na kitu tofauti, ambacho mashabiki wake watakipenda.

Mkojani anasema kuthibitisha hilo ndio maana  hata mwonekano wake wa mavazi  na hata visa vyake havilingani na wasanii wengine, ingawa anakiri kwamba ushindani ni mkubwa na walio wengi wanafanya vizuri ndio maana sanaa yao imekuwa na mashabiki wengi ukilinganisha na ilivyokua zamani.

“Nafurahi kuona tupo wengi na wote tunafanya vizuri kila mmoja kwa nafasi yake ndio maana tumefanikiwa kuwateka wananchi inaonesha kazi inafanyika na ujumbe unafika kwa jamii ambayo tunaikusudia iweze kuelimika au kuburudika,” anasema Mkojani.

ALIPOANZIA SANAA

Mkojani ambaye kwa sasa anafanya kazi na kampuni ya rangi ya Billion Paints,  akiwa balozi ambaye kazi yake kubwa ni kuinadi kampuni hiyo kwa wananchi,  alijiingiza kwenye sanaa ya kuigiza mwaka 2003 akianza na kundi la Mwagamwaga la kwao Manzese Dar es Salaam.

Mwagamwaga alikaa kwa muda mfupi baadae akajiunga na kundi jingine la Kipande huko alikuwa akiigiza sana filamu za kichawi, sambamba na wasanii wakongwe, akina Bi Mwenda Mzee, Msisi wa Msisiri na marehemu Jengua.

Balozi huyo wa Billion Paints anasema baada ya kukaa hapo kwa miaka mitatu alihamia Kampuni ya MT, ambako akiwa huko aliungana na wasanii mbalimbali wa komedi, wakiwemo Ringo Tin White, Mzee Majuto, Kitale, marehemu Kinyambe, Gondo Msamba, Senga  na wengineo. 

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/6ca1df7b6d1b8720634f9a109093467b.JPG

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Mohamed Akida

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi