loader
Dstv Habarileo  Mobile
Usikivu wa TBC wapanda kwa asilimia 14 ndani ya siku 60

Usikivu wa TBC wapanda kwa asilimia 14 ndani ya siku 60

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amesema hadi kufikia Mwezi Septemba, mwaka  huu usikivu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) utapanda kuzifikia Wilaya 120 sawa na 76%  kutoka Wilaya 103  ambapo ni sawa na 64% za usikivu wa sasa ili kuhahakikisha wananchi wote wanapata habari kwa uhakika.

Waziri Bashungwa ameyasema hayo leo Julai 30, 2021 kwenye uzinduzi wa kituo cha kurushia matangazo ya redio eneo la Kisaki mkoani Morogoro ambapo amesema katika Bajeti ya Maendeleo ya Wizara yake kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021, TBC inatekeleza miradi ya upanuzi wa usikivu katika Wilaya za Karagwe (Kagera), Same (Kilimanjaro), Sikonge (Tabora), Kahama (Shinyanga), Bunda (Mara), Nkasi (Rukwa) na Kasulu (Kigoma)ambapo amefafanua kuwa kukamilika kwa miradi hii kutawezesha usikivu wa TBC kufikia 76% ya nchi nzima.

“Nataka kuwahakikishia wananchi wote kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi shupavu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakusudia kupanua usikivu wa redio za TBC nchi nzima” amesisitiza Mhe. Bashungwa

Ameyataja maeneo mengine ambayo miradi inaendelea kutekelezwa kwa ushirikiano wa TBC na UCSAF kuwa ni pamoja na wilaya za Ngara (Kagera), Kyela (Mbeya), Ruangwa (Lindi), Kilombero/Mlimba (Morogoro), Ludewa (Njombe), Tanganyika (Katavi), Makete (Njombe), Uvinza (Kigoma), Mbinga (Ruvuma) na Ngorongoro (Arusha).

Pia ametoa wito kwa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kupeleka miundombinu ya umeme kwa vituo vyote ambavyo vinatumia genereta mfano Karagwe ili kuendelea kupunguza gharama za uendeshaji wa miradi hii.

“Kabla ya mradi kuanza kutekelezwa TBC, TANESCO na UCSAF kaeni pamoja mjadiliane namna ya kutekeleza miradi hii kwa ufanisi ili kutatua shida zinazowakabili wananchi wetu kwa kukosa huduma ya Habari na Mawasiliano” amesisitiza Bashungwa

Kwa upande mwingine ameiomba Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS na TAMISEMI kupitia TARURA waone namna ya kuwezesha kufikika eneo hilo la mradi wa Kisaki kwa urahisi zaidi.

Alisema, “Ombi hili ni sambamba na maeneo mengine yenye mitambo ya kurusha matangazo ambayo miundombinu yake haiko vizuri mfano eneo la Mnyusi- Tanga, Imagi – Dodoma, Matogoro – Songea  na Mlima kampuni – Katavi)”. 

Aidha ameisihi Menejimenti ya Shirika hilo kuendelea kuwa wabunifu katika kuhabarisha umma na kuwahakikishia kwamba Wizara yake itaendelea kuwapatia msaada wowote wanaohitaji ili kutimiza malengo yake. Amelitaka TBC kuhakikisha linaandaa maudhui yatakayokidhi matakwa ya jamii nzima ya watanzania katika kukuza uzalendo, kudumisha mila na desturi za Watanzania na kulinda tunu za Taifa.

Pia amelipongeza TBC kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwahabarisha wananchi wa makundi yote, ambapo amesema anatambua jitihada zinazofanywa za kukamilisha uzinduzi wa chaneli mpya ya televisheni ya TBC2 itakuwa mahususi kwa ajili ya vipindi vya vijana, michezo na burudani ambayo ujenzi wa studio zake umekamilika  Mikocheni, Dar es Salaam.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/df0d3e083f725ec6e60c0d83ad7ba15a.jpg

WASICHANA waliopata ujauzito katika umri mdogo ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi