loader
Tujitokeze vituoni kuchanja corona

Tujitokeze vituoni kuchanja corona

ZOEZI la utoaji wa chanjo ya kudhibiti virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa hatari wa covid- 19 imeanza kusambazwa katika maeneo mbalimbali nchini na baadhi ya mikoa ukiwamo wa Pwani imeanza kutoa chanjo hiyo kwa makundi mbalimbali. Chanjo hiyo inatolewa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuizindua rasmi kitaifa katika Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam.

Katika uzinduzi huo, mbele ya baadhi ya viongozi wa serikali, dini na watu wengine akiwamo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na akitazamwa na mamilioni ya Watanzania kupitia vyombo vya habari, Rais Samia pia alichanjwa ili kujikinga na ugonjwa huo hatari ambao umepoteza mamilioni ya watu duniani wakiwamo Watanzania.

Rais Samia amechukua uamuzi huo akitambua kuwa chanjo hiyo ni salama, imefanyiwa utafiti wa kutosha hivyo akiwa mkuu wa nchi ameonesha njia kwa wale wenye nia ya kuchanjwa, kwamba watafanya hivyo wakiwa na uhakika wa chanjo yenyewe, kinyume cha wale wanaodai zina madhara.

Ubora na usalama wa chanjo hizo pia umethibitishwa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ambayo kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wake, Profesa Yunus Mgaya amesema zitakazotolewa nchini dhidi ya ugonjwa huo ni salama kwa asilimia 99.99 na zimethibitishwa na jopo la wanasayansi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO).

Kwa mujibu wa Profesa Mgaya, chanjo sita zilizopitishwa na WHO kuwa zinafaa, haziwezi kumdhuru mtu kwamba akinywa atakufa au kuugua au kugeuka ‘zombie’ kama baadhi ya wapotoshaji wanavyodai, kwani kiwango cha athari ni kidogo mno kinachofikia asilimia 0.00004.

Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa, manufaa ya chanjo za corona ni pamoja na kupunguza vifo, kuzuia watu kulazwa hospitalini, kupunguza makali ya ugonjwa na maambukizi, pamoja na kupunguza mateso ya kushindwa kupumua vizuri.

Kwa msingi huo, tunawahimiza wananchi hasa makundi ya awali ambayo yameanishwa kupatiwa chanjo hiyo wakiwemo watumishi wa afya, viongozi wa dini, wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea na wenye magonjwa sugu kujitokeza kwa wingi katika vituo vilivyopangwa ili kupata chanjo hiyo.

Tunaitoa hofu jamii kuwa, hakuna shaka kwamba chanjo hizo zimepitishwa baada ya kukidhi mahitaji ya kisayansi ya chanjo kwa mujibu wa miongozo ya WHO, hivyo upotoshaji wa baadhi ya watu usiwatie woga kujitokeza kwenda kuchanja kwa hofu ya kudhurika.

Kwa miaka mingi sasa duniani, Watanzania na watu wengine duniani wamekuwa wakichanjwa kudhibiti magonjwa mbalimbali kama vile surua, pepopunda, polio, homa ya ini, ndui na nyinginezo na hakujawahi kusikika kauli za kupinga chanjo hizo na watu wamedhibiti magonjwa hayo na mengineyo.

Hivyo, tunawasitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupata chanjo hiyo katika vituo vilivyopangwa huko mikoani ili kujilinda na kuupa mwili kinga ya kupambana na ugonjwa wa covid-19 ambao unaua watu wengi na kwa kasi kubwa.

foto
Mwandishi: MHARIRI

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi