loader
ROBYN FENTY ‘Rihanna”   Aingia orodha ya mabilionea kwa jitihada binafsi

ROBYN FENTY ‘Rihanna”  Aingia orodha ya mabilionea kwa jitihada binafsi

JUHUDI binafsi na kujituma siku zote huwa kuna malipo mazuri na ndivyo ilivyo kwa mwanamuziki, muigizaji na mjasirimali Robyn Fenty maarufu zaidi kwa jina la Rihanna baada ya kufanya kazi kwa juhudi zake binafsi sasa amekuwa bilionea. 

Rihanna alianzisha Brandi ya vipodozi ya Fenty Beauty mwaka 2017 iliyomuinua zaidi kwani ni bidhaa ambazo kila mwanamke  mahali popote alijisikia mrembo na kwa namna isiyotarajiwa: brandi yake hiyo ya urembo imemsaidia kuingia katika orodha ya mabilionea. 

Kwa mujibu Forbes mshindi huyo wa Tuzo ya Grammy anakadiriwa sasa kuwa na utajiri wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.7 na kumfanya kuwa mwanamuziki wa kike tajiri zaidi duniani akifuatiwa na Oprah anayetajwa kuwa mburudishaji tajiri zaidi. 

Mbali na Rihanna kujilikana kwa vibao vyake kama Work, Umbrella na  We Found Love na uigizaji wake katika filamu iliyokuwa na bajeti kubwa ya Ocean's 8  pia ni ikoni wa mitindo. 

Mwaka 2017, Rihanna aliungana na kampuni ya Ufaransa, LVMH nyumba ya mitindo inayomiliki brandi za Louis Vuitton na Dior, kuzindua mtandao wake wa vipodozi unaojulikana kama Fenty Beauty. 

Mwaka uliofuata alitoka na Savage by Fenty, ambayo yenyewe inahusika na nguo za ndani lengo ni kuonesha muonekano chanya na jumuishi. 

“Kiasi kikubwa katika utajiri huo wa dola za Marekani bilioni 1.7 hautokani na kuimba  ila kutokana na vipodozi,” anasema Mhariri wa Forbes, Kerry Dolan.

“Imekuwa kampuni ya vipodozi yenye mafanikio, tangu ilipozonduliwa na kupata pongezi nyingi kwa sababu ilikuwa na rangi aina 40 kwa ajili ya ngozi, kitu ambacho wakati huo sio kampuni zote za vipodozi zilikuwa nazo,” anasema. 

Wakati laini ya mavazi ya kifahari ya Fenty ilifungwa mapema mwaka huu, chapa hiyo ilimfanya mwimbaji huyo aliyegeuka tajiri kuwa na hadhi ya bilionea.

Rihanna anaingia katika orodha ya Forbes kama mjasiriamali binafsi wa Hollywood aliyefanikiwa akiwa pamoja na Kim Kardashian na Kylie Jenner.

Mzaliwa huyo wa Barbados pia ana mashabiki milioni 101 katika kaunti yake ya Instagram na mashabiki milioni 102.5 mashabiki kwenye Twitter kwa kujenga brandi yake ya urembo na sasa ndio mjasiriamali aliyefanikiwa sana katika masuala ya urembo. 

Fenty Beauty, ambayo ni ushirika wa  50-50 na kampuni ya Kifaransa ya LVMH, inayoendeshwa na Bernard Arnault, mtu wa pili kwa utajiri duniani, ilizinduliwa 2017. 

Bidhaa hizo zinapatikana kwenye mtandano na maduka ya Sephora ambayo yanamilikiwa na LVMH.

Hadi kufika 2018, brandi hiyo ikiwa na mapato kwa mwaka  zaidi ya dola za Marekani milioni 550, kwa mujibu wa LVMH na kuangusha brandi za mastaa wengine kama Kylie Jenner’s Kylie Cosmetics, Kim Kardashian West’s KKW Beauty na Jessica Alba’s Honest Co.

Fenty Beauty sio brandi pekee iliyomuingiza mabilioni ya dola. Mwezi Februari brandi yake ya nguo za ndani Savage x Fenty iliongezeka hadi dola za Marekani milioni 115. 

Rihanna alizaliwa na kupewa jina Robyn Rihanna Fenty, Februari 20, 1988, eneo la Saint Michael, Barbados.

Msanii huyu ni binti wa Mhasibu Monica (née Braithwaite) na Mhasibu wa ghala, Ronald Fenty. Mama yake ni Mwafrika mwenye asili ya Guyanese, wakati baba yake kutoka Barbados ana asili ya Afrika na Ireland. 

Rihanna ana kaka wawili Rorrey na Rajad Fenty, na amechangia baba na dada wawili na kaka mmoja ambao wote wamezaliwa na mama tofauti tofauti, kutokana na mahusiano ya baba yake ya awali. 

Alikulia katika jumba lenye vyumba vitatu eneo la Bridgetown na aliuza mavazi na baba yake katika maduka mitaani.

Maisha yake ya utoto yaliathiriwa na tabia ya baba yake ya ulevi na matumizi ya dawa za kulevya na kusababisha ndoa ya wazazi wake kusambaratika. 

Mbali na ulevi, baba yake Rihanna alikuwa na tabia ya kumnyanyasa mama yake ikiwa ni pamoja na kumpiga na Rihanna alikuwa akijaribu kuingilia kati kuzuia wasipigane. 

Akiwa mtoto Rihanna alikuwa akifanyiwa kipimo cha CT Scan mara kwa mara kutokana maumivu makali ya kichwa aliyokuwa akipata, anakumbuka.

Madaktari walifikia hatua wakadhani ana uvimbe kichwani, kwa sababu alikuwa akipata maumivu makali sana. 

Akiwa na umri wa miaka 14, wazazi wake walitalakiana na afya yake ikaanza kuboreka.

Rihanna alipenda kusikiliza muziki wa reggae. Alihudhuria Shule ya Msingi Charles F. Broome Memorial na Combermere, vile vile alisoma katika shule ya kimataifa ya kriketi Chris Jordan na Carlos Brathwaite.

Msanii huyu pia alikuwa kadeti wa jeshi katika programu ndogo ya jeshi, ambapo mwanamuziki na mwandishi wa muziki kutoka Barbados Shontelle alikuwa sajenti. 

Ingawa matamanio yake ilikuwa kuhitimu masomo ya sekondari, alichagua badala yake kuendelea na kazi ya muziki. 

Kwa mara ya kwanza mwanamuziki huyo aliisaini mkataba na kampuni ya muziki ya Def Jam akiwa na umri wa miaka 16 na mwaka 2005 alitoa albamu yake ya kwanza inayojulikna kama Music of the Sun, iliyouzwa nakala zaidi ya milioni mbili duniani kote. Aliendelea kutoa albamu zingine na nyimbo kadhaa zilizofanya vizuri sana ikiwemo Unfaithful, Umbrella, Disturbia, Take a Bow, Diamonds na We Found Love.

Ameshawahi kushinda tuzo kadhaa kubwa zikiwemo za Grammys na MTV. 

Filamu

Rihanna ameshashiriki kwenye filamu kadhaa ikiwemo Battleship (2012) na alikuwa muigizaji kiongozi ambaye sauti yake ilisikika katika filamu ya katuni Home (2015).

Mwaka In 2017, Rihanna alishiriki katika msimu wa tano wa filamu Bates Motel. Mwaka huo huo kwa mara ya kwanza mashabiki wakapata vionjo vya nyota huyo wa muziki wa Pop akiwa sambamba na waigizaji wakubwa Sandra Bullock, Cate Blanchett na  Anne Hathaway katika trela ya filamu ya Ocean's 8.

Lakini pia aliigiza namuigizaji  Donald Glover aka Childish Gambino, katika filamu Guava Island.

Kazi za hisani na maisha binafsi 

Mwaka 2012, Rihanna alizindua Mfuko wa hisani unaojulikana kama Clara Lionel Foundation. Mfuko huo una jina la bibi yake na kazi yake kubwa ni kusaidia na kufadhili programu za elimu duniani na kwa kazi hiyo alitunukiwa tuzo ya Rais mwaka jana inayojulikana kama NAACP Image Awards.

Rihanna pia ameshawahi kupamba vichwa vya magazeti kwa habari za maisha yake binafsi ikiwa ni pamoja na kuhusishwa kuwa na mahusiano na mshauri wake Rapa Jay-Z,hata hvyo wote wawili walikanusha habari hizo, lakini pia alihusishwa kuwa na mahusiano na mfanyabiashara bilionea kutoa Saudi Arabia, Hassan Jameel, kabla hawajaachana mapema mwaka jana. 

Mwaka 2009, Rihanna aliandikwa sana kwenye vyombo vya habari baada ya tukio la kupigwa na rafiki yake wa kiume mwanamuziki Chris Brown. Tukio hilo lilisababisha mijadala mingi duniani kwa mashabiki wa muziki na mwanamuziki huyo wakimtetea Rihanna na baadaye akaja kiwa msemaji dhidi ya vitendo vya unyanyasaji. 

“Hili limetokea kwangu na linaweza kumtokea mwingine,” alisema katika mahojiano na mtangazaji Diane Sawyer. 

Mwaka 2012, Rihanna alionekana kuungana tena na Brown na wawili hao walifanya kazi pamoja katika wimbo Birthday Cake. 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/0bed9fce9e4f2c70e6f0b826c480733f.jpeg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: LOS ANGELES, Marekani

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi