loader
Bado kilimo ni mkombozi kwa vijana wengi nchini

Bado kilimo ni mkombozi kwa vijana wengi nchini

HIVI karibuni Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafi ti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dk Geofrey Mkamilo alitoa mwito kwa vijana wasiopenda kulima kujiingiza katika usindikaji au kufanya biashara ya bidhaa mbalimbali za kilimo ili kujiongezea kipato chao binafsi na taifa kwa jumla.

Alitoa mwito huo akiwa katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba, yaliyofanyika katika Viwanja vya Julius Nyerere, Temeke.

Mwito huo ulilenga kuwahamasisha vijana hususan wasiopenda kilimo, kutafuta njia mbadala hususan kushiriki katika mnyororo wa thamani katika kilimo ikiwa ni pamoja na kufanya biashara ya bidhaa mbalimbali za mazao zikiwamo za kusindika mazao ili kujipatia kipato.

Katika mazungumzo yake, Dk Mkamilo akatoa mfano wa zao la zabibu kuwa, wapo watu wanaonunua mchuzi wa zabibu na kutengeneza mvinyo na kwamba, hao wanaongeza thamani na kujipatia kipato bora na halali.

Aidha katika zao la korosho, akasema wapo wanaonunua na kwenda kubangua ili waziuze kwenye viwanda, na kuhusu zao la miwa, Mkamilo anasema inaweza kununuliwa na kupelekwa kama malighafi viwandani kwa ajili ya kutengeneza sukari.

Hiyo ni mifano michache kati ya mingi iliyopo katika kilimo inayoweza kuwafanya vijana wapende na kujishughulisha zaidi na kilimo licha ya kutokulima moja kwa moja shambani kwa kuwa kilimo kina mchango mkubwa katika uchumi wa viwanda, wakulima na wadau mbalimbali katika kuongezea kipato kwa njia na fursa mbalimbali.

Ikumbukwe kuwa, zaidi ya asilimia 65 ya malighafi viwandani inatokana na kilimo, hivyo kilimo ni biashara na fursa ‘inayolipa’ inapochangamkiwa na vijana wengi hususan wasio na ajira ama waliomaliza vyuo, lakini bado wapo nyumbani wakifikiria nini cha kufanya.

Ndiyo maana ninaungana na Dk Mkamilo kusema kuwa, kilimo ni njia muhimu ya kukuza uchumi hata kwa vijana wanaokipenda kwa kushiriki kulima moja kwa moja shambani, au kupitia mnyororo wa kuongeza thamani katika mazao yatokanayo na kilimo.

Ndio maana ninasema, hamasa hiyo iwaondoe vijana kutoka katika ‘tope la fikra mgando’ za kuchukia kilimo na badala yake, wawe sehemu ya kilimo kupitia mnyororo wa thamani.

Ikumbukwe kuwa, serikali kupitia Tari inatilia mkazo usambazaji wa teknolojia zilizopo kwa wakulima na wadau mbalimbali wa kilimo ili zitoe matokeo chanya na hatimaye, kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Ili kuona mwanga na hamasa zaidi kushiriki kilimo kwa namna moja ama nyingine kama alivyohimiza Mkamilo, Tari iongeze nguvu maradufu kupitia utaalamu wake ili sekta ya kilimo iwe yenye tija zaidi kupitia utafiti unaotoa majawabu yanayotatua changamoto za kijamii.

Hili ni pamoja na kuhakikisha unafanyika utafiti wa mbegu bora zitakazotoa mazao bora ama teknolojia za kusindika ama kukaushia mazao ili wadau wa kilimo wapate tija zaidi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/0307c143ea9c14ba81810426ea16b1fe.jpg

NIPO nyumbani kwa Baba na Mama Chichi. ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi