loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kilimo cha umwagiliaji, mbegu   bora kuongeza uzalishaji alizeti

Kilimo cha umwagiliaji, mbegu  bora kuongeza uzalishaji alizeti

"KILIMO cha alizeti nchini sehemu kubwa kinategemea mvua. Ni bora sasa tukafikiria kuingia kwenye umwagiliaji," anasema Michael Mpembwa kutoka kampuni ya Nilaje Agro Trading and General Supply.

Anatoa kauli hiyo wakati akizungumzia sababu zinazofanya uzalishaji wa alizeti kutokuwa wa kiwango kikubwa nchini.

Anasema ingawa duniani uzalishaji umeongezeka kutoka tani milioni 44.3 mwaka 2015 hadi tani milioni 51.9 mwaka 2019, uzalishaji wa alizeti nchini bado unajikongoja ukiwa umefikia tani 649,437 kutoka tani 561,297 mwaka 2018/2019. Ingawa kuna ongezeko, lakini Tanzania inahitaji kuondokana na uagizaji wa mafuta ya kupikia nje haraka iwezekanavyo, kiasi hicho bado ni kidogo.

Tanzania ambayo zaidi ya nusu ya mafuta ya kula (takribani asilimia 55) inaagiza nje, imekuwa ikiweka mikakati mingi ili kuona inajitosheleza katika eneo hilo. 

Akiwa na mazoea ya kulima ekari 500 kila mwaka, Mpembwa anasema kilimo cha alizeti cha kutegemea mvua kimefanya uzalishaji usiwe wenye tija hasa mvua zinapokuwa haba au zikichelewa na wakati mwingine kuwa nyingi kupita kiasi kama ilivyotokea katika msimu uliopita.

“Msimu uliopita tulikuwa na shida ya kuwa na mvua nyingi kuzidi kiasi. Pamoja na kuingia gharama kubwa katika kilimo tuliambulia kidogo sana,” anasema.

Mpembwa anaamini kwamba kuwa na uhakika wa mavuno kunaanzia kwenye mbegu za kisasa na za uhakika na kisha kuwepo kwa unyevunyevu unaotakiwa kupitia mifumo ya umwagiliaji badala ya kusubiri mvua.

"Kiuhalisia kwenye ekari moja huwa tunavuna wastani wa kilo 600, na gharama ya kulima hiyo ekari moja ukijumuisha mbolea, kupalilia kuvuna, kuhifadhi na kupeleka sokoni, gharama hufikia Sh 450,000," anasema.

Wazalishaji mbalimbali wa mbegu za alizeti na gharama za mafuta, wanakiri kwa nyakati tofauti kwamba utegemeaji wa mvua unachangia uzalishaji duni wa alizeti. Wanasema mvua ikiwahi, ikichelewa, ikiwa haba au nyingi uzalishaji hauwi uliotarajiwa.

Mwenyekiti wa chama cha wasindikaji wa mafuta ya kupikia Tanzania (Tasupa), Ringo Iringo, anakiri kwamba mvua kubwa zilizonyesha katika msimu wa mwaka jana ni moja ya sababu kubwa ya kuwa na mavuno kidogo katika msimu huo na kufanya upatikanaji wa mbegu za mafuta kuwa kidogo na hivyo bei ya mafuta kupanda ghafla. Anasema kimsingi zao la alizeti halihitaji mvua nyingi.

Mwenyekiti huyo anasema katika maeneo mengi ambako wanategemea kilimo cha alizeti, wengi hawakuvuna ama walivuna chini ya wastani, hivyo, kusababisha bidhaa hiyo kuwa adimu na viwanda vingi kusimamisha uzalishaji wa mafuta. 

Iringo ambaye pia ni msindikaji wa mbegu za mafuta anaamini kwamba sio kilimo cha umwagiliaji pekee kitakacholeta mapinduzi ya kilimo cha alizeti bali pia upatikanaji wa mbegu bora.

Anasema Tanzania ni ya kwanza katika uzalishaji wa mbegu za alizeti na Afrika Kusini ni ya pili lakini taifa hilo linaongoza kutoa mafuta mengi ya yatokanayo na zao hilo kuliko Tanzania kutokana na ubora wa mbegu zao.

 

 “Afrika ya Kusini inazalisha tani 700,000 hadi tani 900,000 za mbegu za alizeti kwa mwaka na huzalisha tani 700,000  za mafuta ya alizeti huku Tanzania ikizalisha mbegu za alizeti tani milioni 2.5 hadi milioni 3 lakini inazalisha tani 200,000 tu za mafuta ya alizeti kwa mwaka,” anasema Ringo.

Anasema pamoja na changamoto hiyo, ipo haja kwa serikali kuhakikisha inafanya mapinduzi katika kilimo cha alizeti kwa kuanzisha kilimo cha umwagiliaji alizeti na mbegu za kisasa ambazo zina sahani kubwa na mafuta mengi.     

Mkulima katika Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma, Jackson Shimba, naye anasema upatikanaji wa mbegu bora bado ni changamoto kwa wakulima wa alizeti na kwamba wengi bado hawalimi kitaalamu huku uvunaji ukiwa mbaya na kwamba uhifadhi usioridhisha unachangia pia kuwa na mavuno madogo.

Nguvu kazi iliyopo ikipewa nyenzo na utaalamu inawezekana kabisa kubadili kilimo na kukifanya kiwe na tija zaidi, anasema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Anasema serikali imejielekeza katika mikoa ya Singida, Dodoma na Simiyu ambayo hulima zao hilo kwa wingi akitaka asilimia 10 ya mikopo inayotengwa na halmashauri kwa makundi ya vijana, wanawake na wenye ulemavu itumike kwa kuwapatia mitaji ya mbegu za zao hilo badala ya fedha ili kupanua wigo wa uzalishaji.

Majaliwa alitoa angalizo hilo wakati akizindua kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha kilimo cha alizeti kwa wadau mbalimbali wa mnyororo wa thamani ya zao hilo kutoka mikoa ya Singida, Dodoma na Simiyu.

Waziri Mkuu anaweka bayana kwamba mkulima atakayelima ekari moja kitaalamu atatumia wastani wa Sh 250,000 kwa ekari lakini atapata takribani Sh 1,350,000 kwa ekari.

"Mathalani ukilima zao hili kwa ekari moja utatumia mbegu kilo 2 kwa gharama ya Sh 70,000 utavuna magunia 15 ya takribani kilo 65 na kwa kila gunia utapata lita 18 za mafuta, na kila lita kwa bei ya soko ni Sh 5,000, hivyo unakwenda kupata takribani Sh 1,350,000. Ukitoa Sh 250,000 za maandalizi ya shamba hadi kuvuna unajikuta na faida kubwa," anasema Waziri Mkuu.

 

Katika bajeti ya mwaka huu, Wizara ya Kilimo ilisema kwamba inaongeza bajeti katika eneo la uzalishaji wa mbegu bora za alizeti ili kuongeza uzalishaji kama njia mojawapo ya kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi ambapo taifa hutumia zaidi ya shilingi bilioni 474 kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi.

Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda anasema Wizara ya Kilimo itaendelea kuhamasisha uanzishaji wa mashamba ya pamoja (block farming) katika mikoa inayozalisha mazao ya mafuta kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma ikiwemo mbegu bora, mbolea, viuatilifu na zana bora za kilimo pamoja na mafunzo ya kilimo bora kwa wakulima. 

Aidha, Serikali inasema itaimarisha pia kilimo cha mkataba kwa mazao ya mafuta kwa lengo la kuwa na uhakika wa masoko.

Pamoja na kuongeza nguvu kuhakikisha kwamba mafuta ya kula yanapatikana nchini kwa kiasi kinachotakiwa, Serikali imeahidi kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuondoa vikwazo mbalimbali ili kuwawezesha wawekezaji na wakulima wadogo kuweza kusafirisha bidhaa zao nje.

Profesa Mkenda anasema anafahamu kuna mambo ambayo yanasababisha kukwama kwa uzalishaji mkubwa wa mafuta nchini, hivyo Serikali itapitia upya sheria na kanuni ili kuondoa mkwamo na kuwezesha uzalishaji wa ndani kukua zaidi. 

Anasema suala la mbegu za alizeti ni changamoto lakini Serikali itahakikisha mbegu za kutosha zinapatikana kwa kuendelea kutekeleza Mkakati wa Kuendeleza Zao la Alizeti kwa kuimarisha utafiti wa mbegu bora na kuboresha mazingira ya uwekezaji katika tasnia ya alizeti.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe anasema SerikaliI imeanza mchakato wa kuhakikisha wakulima wa alizeti wanapata mbegu bora kwa muda mwafaka kabla ya msimu wa kilimo kuanza.

 

Akizungumza na wadau wa uzalishaji mbegu za alizeti hivi karibuni, anasema mchakato huo una lengo la kuhakikisha wakulima wanapata mbegu kwa wakati.

 

Bashe anasema mazao ya chikichi na alizeti ndiyo yako kwenye kipaumbele zaidi, ingawa anakiri kwamba bado kuna safari ndefu katika kuhakikisha mafuta ya mawese yanapatikana kwa wingi.

 

Anasema kilimo cha alizeti kikipewa msukumo mkubwa kinaweza kuongeza uzalishaji na kuondoa upungufu wa mafuta ya kupikia nchini. 

 

Mkurugenzi Mtendaji kiwanda cha Pyxus Agriculture Tanzania, Malcolm McGrath anasema kiwanda hicho kwa sasa kinazalisha tani 20,000 kwa mwaka lakini kina uwezo wa kuzalisha mara sita zaidi ya hapo. 

 

Anasema tayari wamekuwa na mawasiliano na wakulima wadogo, wa kati na wakubwa wa alizeti kutoka mikoa ya Dodoma, Iringa, Morogoro, Manyara, Singida, Tabora na Kigoma lakini kuna changamoto kubwa ya ughali wa malighafi.

 

Hali hiyo anasema inafanya bidhaa yao kuwa ghali ukilinganisha na nchi nyingine zinazopeleka mafuta katika soko la Ulaya.

 

McGrath anaiomba Serikali kuwezesha kilimo cha mkataba ili wazalishaji mafuta wawe na uhakika wa malighafi na viwanda visifungwe kwa ajili ya ukosefu wa malighafi.

 

Anasema kiwanda hicho kimepata soko katika Jumuiya ya Ulaya ya kupeleka mafuta yaliyosafishwa mara mbili (Double Refined).

 

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao; Wizara ya Kilimo Enorck Nyasebwa, anasema timu ya wataalamu itakutana kutafuta suluhisho la kuongeza uzalishaji nchini. 

 

Anasema kuna ongezeko kubwa la mahitaji ya mafuta ya alizeti yanayozalishwa nchini katika soko la India na Afrika Kusini.

 

Mwenyekiti wa Baraza la Kilimo la Taifa, Timoth Mmbaga amesema: "Uhaba wa mafuta ya kula ni fursa pia ni onyo; Hivi Malaysia angekataa kutupa mafuta tungefanyaje? Hili ni onyo lazima tujitegemee na sasa tunajitosheleza kwa asilimia 43 tu.”

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/3eb47c3b964f50a359b4cac37809a8b1.JPG

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi