loader
Jicho pevu Dar lahitajika kunusuru mtoto wa kike miji ya pembezoni

Jicho pevu Dar lahitajika kunusuru mtoto wa kike miji ya pembezoni

Majiji ya Afrika yanashuhudia ukuaji wa kasi wa idadi ya watu na kusababisha mahitaji ya huduma za msingi kuongezeka.

Jiji la Dar es Salaam linatajwa kuwa miongoni mwa majiji hayo. Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030, jiji la Dar es Salaam litakuwa miongoni mwa majiji makubwa zaidi (mega-cities) Afrika.

Ukuaji wa jiji hilo kubwa kibiashara Tanzania una matokeo chanya na hasi katika nyanja mbalimbali za maisha ya wakazi wake  ikiwemo kiuchumi na kijamii. Kila kukicha, idadi kubwa ya wahamiaji kutoka mikoa mingine inaongezeka kwa kuwa jiji la Dar es Salaam ndilo kinara wa biashara Tanzania.

Mji umepanuka tofauti ilivyokuwa awali ambapo Posta na Kariakoo ndio maeneo yaliyojulikana kwa biashara. Ongezeko la watu limesababisha umeasukuma watu kuanzisha makazi kilomita 20 au zaidi kutoka katikati ya jiji.

Mfano dhahiri ni maeneo ya Mbopo na Mabwepande, wilayani Kinondoni au Mbezi Mwisho na Kibamba wilayani Ubungo. Achilia mbali au Kitunda wilayani Ilala na kwinginepo.

Japo serikali inafanya juhudi kuhakikisha inatoa huduma kwa watu wake, bado kasi ya ongezeko la watu ni kasi zaidi.

Mathalani waliohamia maeneo kama ya Mbopo na Mabwepande walikuwa wapangaji katika maeneo ya Sinza, Ubungo au Mwenge  ambako huduma za kijamii kama afya na elimu zilikuwa jirani.

Katika kukabiliana na gharama za maisha, walijitahidi kuhakikisha kuwa wanapata viwanja nje ya miji-ambako wanaweza kumudu gharama ya chini na kuanzisha makazi.

Kwa kuwa huduma hazijaimarika kama ilivyo kwenye miji walikotoka, changamoto inakuja namna ya kuzipata kwa ukamilifu wake.

Adha kwa mtoto wa kike

Watoto wa kike wamekuwa ni miongoni mwa waathirika wa maisha mapya nje ya jiji la Dar es Salaam.

Umbali wa kupata huduma kama elimu na usafiri wa kwenda kuipata huduma hiyo nyeti (elimu) unatishia mustakabali wa elimu yake na azma ya  kuleta usawa wa kijinsia katika nyanja zote za maisha ya mwanadamu.

Daladala ni usafiri salama kwani wazazi na wanafunzi wanaweza kuutumia kwa pamoja. Lakini miundombinu mibovu ya barabara imekatisha safari za kuelekea pembezoni mwa mji kama Mabwepande. Madereva wanahofia usalama wa vyombo wanavyoviendesha kuharibika.

Usafiri mkuu ni ‘bodaboda’ kwa sasa ambapo wengi wa wakazi wa maeneo hayo hawana imani nao hasa linapokuja suala la maisha ya mtoto wa kike.

Hofu kubwa ni kukatizwa kwa ndoto za wasichana kwa kuhadaiwa na kuishia kupata ujauzito. Hata hivyo, ni hatari kwa usalama barabarani japo Jeshi la Polisi limekuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa madereva wa bodaboda huku Serikali ya Mtaa wa Mabwepande ikipiga marufuku wanafunzi kupanda bodaboda.

Hata hivyo, vipato duni vya wazazi ni mzigo mkubwa kwao kutoa fedha ya usafiri wa bodaboda au bajaji kila siku. Kwa kuwa wanafunzi wanalazimika kuwahi  alfajiri na kurudi usiku, hofu kwa wazazi limekuwa jambo la kawaida. “Je, atarudi salama” ndilo swali ambalo mzazi hujiuliza baada ya kufanikiwa kumpandisha mwanafunzi kwenye bodaboda alfajiri.

Kwa kuwa ‘mchawi’ wa watoto wa kike yupo katikati ya shule na nyumbani, Serikali ni mdau muhimu wa kuhakikisha kuwa upatikanaji wa huduma muhimu unakuwa wa uhakika ili wananchi walioko pembezoni waweze kumudu mahitaji yao, ikiwemo elimu bora na ya uhakika kwa watoto wao.

Kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo ambayo huduma kama maji ni kero na changamoto zaidi umekuwa ni mzigo wa akina mama na wasichana, serikali inapaswa kuweka nguvu kuhakikisha usawa katika uletaji maendeleo kwa wote.

 

 

 

 

 

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/8e787062058e6ecb151ca29a2f499d11.jpeg

MOJA ya misemo maarufu ya Rais mstaafu Ali Hassan ...

foto
Mwandishi: SAULI GILIARD

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi