loader
LULU MCHOPA  Mwanamke mwenye fani lukuki aliyepitia magumu

LULU MCHOPA Mwanamke mwenye fani lukuki aliyepitia magumu

MTU anaponiona anaweza kuniwazia kuwa mambo yangu yalikuwa safi lakini ukweli ni kwamba, nimepita kwenye changamoto nyingi. Mungu amenipigania… Kama si mkono wa Mungu nisingefika hata hapa nilipo. Ameniwezesha kufanya kazi halali mbalimbali bila kujali watu wanavyonichukulia wala kukata tamaa. Hapa nilipo, najiona mshindi.” hii ni kauli ya Lulu Mchopa, mama wa watoto watano, mkazi wa Kibamba, Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam.

Kama anavyobainisha, ukimuona bila yeye kukusimulia safari alizopitia, huwezi kufahamu kuwa amepitia milima na mabonde kiasi cha kupoteza ndoto zake, ikiwamo ya kuwa angesoma na kuwa Mwanajeshi.

Lulu akiwa na familia yake.

Mwanamke huyu mwongeaji, mwenye tabasamu kila mara na anayependa kujumuika na watu katika shida na raha, ndoto hiyo haikutimia kwani safari ya elimu ya msingi aliyoianza mwaka 1990 akiwa darasa la kwanza katika Shule ya Songea Mjini iliyopo Mtaa wa Majengo A, hakuhitimisha kwani aliishia darasa la nne.

Lulu ambaye ni mjasiriamali katika maeneo lukuki kiasi cha kumwezesha kutunza familia yake yenye watoto watano, si kwamba alipenda kutoendelea na masomo, bali kutengana kwa wazazi wake kulichangia na kuchochea changamoto nyingine nyingi katika maisha.

Lulu anajieleza akisema, “nilipata changamoto nyingi tangu utotoni zilizozidi umri wangu, nikakua nazo…sasa nasema ni Mungu tu ambaye ameniwezesha mnione hivi nilivyo.”

Lulu ambaye simulizi yake ya maisha imejaa machozi, huzuni, misukosuko na hatimaye ushindi, ana sura nyingi za ujasiriamali. Wapo wanaomfahamu kama bodaboda kwani wakati fulani, aliwahi kusafirisha abiria kwa kutumia pikipiki katika eneo la Kibamba.

Anafahamika pia kama mama lishe baada ya kuanzisha eneo maalumu la kuuza chakula na pia kutoa huduma za upishi katika sherehe na tafrija mbalimbali. Vile vile ni mtaalamu wa masuala ya saluni ikiwamo kutengeneza nywele, ususi, upambaji maharusi huku akisifika miongoni mwa wanawake kwa umahiri kwenye kazi hiyo.

Lulu ni mshereheshaji (MC) huku akisifika kwa uchangamfu na uhamasishaji katika shughuli mbalimbali. Lakini pia, mama huyu ni mwimbaji wa nyimbo za injili na mwishoni mwa mwezi huu, anatarajia kuzindua albamu yake yenye nyimbo nane

Kati ya nyimbo hizo, mmoja unaelezea maisha ya shida aliyopitia huku akimtukuza Mungu kwa kumfikisha hatua hii na kumsahaulisha tabu alizopitia na kuwa miongoni mwa watu wenye heshima na furaha katika jamii ikilinganishwa na dhiki na matatizo aliyopitia tangu utotoni.

Tabu tangu utotoni

Lulu ambaye ni mtoto wa nne kuzaliwa kati ya watoto sita wa Sufiani Mchopa na mama yake, Elizabeth Yazidu anasimulia milima na mabonde aliyopitia katika miaka 40 aliyojaliwa na Mungu duniani. Alizaliwa Machi 24, 1981 katika Kijiji cha Liwena, mkoani Ruvuma.

Anasema utoto wake ulitawaliwa na tabu, mateso na maumivu yaliyochangiwa na kitendo cha baba na mama yake kutengana. “Tuliishi maisha magumu sana mimi na ndugu zangu pamoja na mama yetu aliyeachwa kwenye nyumba ya kupanga Songea Mjini.”

Anakumbuka mama yake alivyokuwa akilima vibarua ili wapate mlo na kwenda shule. Baada ya maisha kuwa magumu sana, mama yake alipata rafiki aliyemshauri waende kwenye machimbo ya dhahabu mkoani Ruvuma na akakubali.

Hapo ndipo maisha yake yalikuwa magumu kiasi cha kutoendelea na masomo ya shule ya msingi. Akiwa na umri wa chini ya miaka 13, alianza pilika za kutafuta maisha ikiwamo kuishi kwa ndugu na kufanya vibarua.

“Mama aliondoka na kwenda kusikojulikana . Tulikuwa tukipelekwa sehemu mbalimbali kwa ndugu. Mara kwa mama mdogo, kwa mama mkubwa au kwa shangazi na huko kwa shangazi kulikuwa na maisha magumu sana. Lakini shangazi alikuwa anatupenda sana isipokuwa uwezo wake ndio ulikuwa mdogo,”anasema.

Kwa hiyo nilikaa huko na wadogo zangu wawili. Nikawa natamani kutoroka lakini nikawa nikikumbuka maisha ya hapo nyumbani na nikiwaangalia wadogo zangu, basi nilikuwa nalia sana.

Anasema mambo yaliendelea kuwa magumu. Katika pitapita za kusaka maisha, alipata ujauzito na akajifungua mtoto wa kike, Mariam mwaka 1998 wakati huo akiwa na umri wa miaka 17. Mambo yaliendelea kumuwia magumu ikizingatiwa kwamba, mwanaume aliyezaa naye pia alikuwa na umri mdogo.

Ndipo shangazi yake mmoja aitwaye Bihawa, aliamua kumsaidia ikiwamo kumtafutia vibarua mjini Songea. Alimtafutia kazi kwenye nyumba ya kulala wageni ambako alikuwa akienda kufanya usafi na shughuli nyingine akiwa amembeba mtoto wake.

Hata hivyo, anasema nyumba hiyo ya wageni haikuwa na ubora na mazingira hayakuwa rafiki kwa mtoto jambo ambalo hakukaa muda mrefu kazini hapo.

“Niliumia sana siku moja 

nilipomuacha mwanangu akiwa amelala nikaenda dukani. Niliporudi, nilimkuta akiwa ameweka mdomoni mpira wa kiume uliotumika. Nililia sana…sikuendelea na kazi,” anasema.

Shangazi yake alimtafutia nyumba nyingine ya wageni ambayo kwa mujibu wa Lulu ilikuwa na hadhi tofauti na ya awali. “Niliendelea na kazi vizuri na usafi wa hiyo gesti ulikuwa wa hali ya juu sana. Hivyo nilikaa muda mrefu huku nikiendelea kumhudumia mtoto wangu. Nikiwa kazini hapo, ndipo nilikutana na mwanaume ambaye aliamua kunioa. Huyu ni baba wa mtoto wangu wa pili.”

Anasema mwanaume huyo (sasa marehemu), alikuwa mfanyakazi katika shirika moja serikalini. “Alinipenda sana na aliniambia siwezi kuendelea kubaki hapo. Nikawa mke, akawa mume…tuliishi maisha mazuri ambayo sikuwahi kuishi. Nilikuwa na maisha mazuri sana. Nikawa mkombozi wa familia yetu. Lakini ghafla, ‘ng’ombe wa masikini hazai… mume wangu aliachishwa kazi.”

Lulu anasema kitendo hicho kilimfanya mumewe kuwa katika kipindi kigumu kifedha na kisaikolojia. “Wakati huo nilikuwa na ujauzito, kumbuka alinikuta na mtoto… nilimtia moyo mume wangu.”

Aanza ususi, kupamba

Katika kipindi hicho ambacho kipato kwenye familia kilitetereka, anasema ndipo alianza kujifunza ususi na kupamba wakati huo mumewe akifuatilia malipo yake kazini na ili kurahisisha ufuatiliaji wa mafao, mumewe aliondoka Songea na kwenda Dodoma kwa kaka yake ambako ilielezwa kuwa akiwa huko, ingelikuwa rahisi kwenda Dar es Salaam kufuatilia.

Lulu alirudi kwao huku vitu vyote vya ndani vya mwanaume vilipelekwa kwa wazazi wa mume. Lulu anasema alikuwa na matumaini kuwa mafao yakipatikana, wataendelea na maisha yao kama kawaida.

“Muda ukapita, mimba ikakua na ikiwa na miezi saba, mama mkwe akafariki hali ambayo mume wangu ilibidi kuja (Songea) msibani na baada ya matanga alirudi Dodoma.” Baada ya miezi mitatu, Lulu alijifungua mtoto wa kiume, James. Akiwa na siku 21, mwaka 2001, mumewe alifariki akiwa Dodoma na alizikwa mkoani humo.

“Nilisikia kuwa alikuwa ameshapata fedha zake na alikufa kifo cha ghafla…walileta matanga Songea na baada ya kumaliza matanga, nilirudi kuendelea kuishi kwetu,” anasimulia Lulu.

Anasema alihangaika 

kuhudumia watoto hao wawili. Anamshukuru wifi yake mmoja, alikuwa msaada kwake licha ya kwamba hakuwa na kipato kikubwa, hata hivyo baada ya kupita miezi mitatu tu , pia huyo wifi alifariki.

Mwaka 2002, wakati huo mtoto huyo wa pili akiwa na umri wa mwaka mmoja, alitafuta kazi kwenye duka la kuuza vinywaji mjini Songea. Akiwa kazini hapo, ndipo alikutana na mwanaume mwingine, wakaoana na kuzaa watoto watatu; Robert, Debora na Vicky.

Hata hivyo anasema, hakupata nafuu kubwa ya maisha kutokana na mumewe kutojitoa kikamilifu katika kujali na kuhudumia familia.

Anakumbuka mwaka 2003 alivyojifungua mtoto (wa tatu) peke yake ndani baada ya kukosa fedha za kwenda hospitali licha ya mumewe kujishughulisha na biashara za madini.

“Nililea watoto wangu watatu huku changamoto zikiendelea… mwaka 2003 niliamua kuokoka. Nikawa nimebadili dini,” anasema Lulu ambaye awali kabla ya kubadili dini, alikuwa akiitwa Zaituni.

Akiwa kanisani, alipata dada, Magreth Ponela, aliyemfundisha upambaji hivyo akawa anapamba kanisani, kwenye shughuli kama vile za kipaimara na ubatizo.

Akiendelea kuishi na mumewe, mwaka 2007 alijifungua mtoto mwingine wa kike na wa mwisho walimpata mwaka 2011.

Alivyofika Dar

Lulu anasema, mumewe alikuwa na kaka yake aliyekuwa akiishi mkoani Dar es Salaam. Alipofariki, mwaka 2010, familia ilimchagua aende Dar es Salaam kwa ajili ya uangalizi wa mali zake eneo la Kibamba wilayani Ubungo.

Baada ya mume kuwasili Dar es Salaam mwishoni mwa mwaka huo wa 2010, pia Lulu na watoto walimfuata na kuanza makazi mapya mkoani humo, wakiwa wamekaa takribani mwaka mmoja, mumewe aliwaacha na kurudi Songea kwa nia ya kwenda kufanya kazi kwenye migodi ya madini.

Kwa mujibu wa Lulu, alikaa Songea kwa takribani miezi tisa bila kuwasiliana na familia hali iliyomlazimu kuanza kujishughulisha na uchuuzi ili kutunza familia yake yenye watoto watano.

“Niliuza mapapai, machungwa ili mradi watoto wasilale njaa,” anasema na kufafanua kuwa matunda hayo aliyatoa kwenye 

shambani walikokuwa wakiishi nyumbani kwa marehemu shemeji yake.

Anaendelea kusema, “nilikuwa nikitunza hilo shamba likaniwezesha kupata fedha kidogo ya kutunza familia huku nikisali mume wangu arejee …nilikuwa nikifunga na kuomba Mungu.”

Ikiwa imepita takribani miezi tisa, anasema mumewe alirudi lakini hakukaa muda mrefu kwani mwaka 2013, aliondoka tena kwa kile alichodai kuwa anakwenda kutafuta fedha. “Hakurudi tena. mpaka sasa (2021) ni miaka minane. Natunza familia ya watoto watano .”

Kwa kuwa nyumba aliyokuwa akiishi ilikuwa ni ya marehemu kaka yake mumewe, Lulu aliamriwa na ndugu kuachia nyumba na eneo hilo lililokuwa na matunda mbalimbali, migomba na mboga, katika eneo la Kibamba.

Lulu anasema ilikuwa kazi ngumu kuondoka na kutafuta nyumba ya kupanga wakati hakuwa na kipato cha kuendesha familia katika jiji la Dar es Salaam.

Mama lishe

Katika kile anachoeleza kuwa Mungu alijibu maombi yake, Lulu anasema alifanikiwa kufungua banda la kupika na kuuza chakula maeneo ya Kibwegere, Kibamba.

Akiendesha shughuli za mama lishe, Lulu aliendelea na harakati za kujikwamua kiuchumi kwa kufanya shughuli za ushereheshaji, saluni na upambaji kazi ambazo anaendelea nazo hadi sasa.

Alikuwa bodaboda

Vile vile Lulu ambaye aliwahi kumiliki pikipiki ya biashara ya kusafirisha watu (bodaboda), anasema kuna wakati aliamua kufanya kazi ya boda boda.

“Ilinibini wakati mwingine niendeshe mwenyewe ili pikipiki isikae tu bila kuleta hela,” anasema Lulu na kusimulia namna ambavyo jamii ilimshangaa ikizingatiwa kwamba wengi wa wanaofanya kazi hiyo ni wanaume.

Uimbaji

Kipaji kingine alichojaliwa ambacho amedhamiria kimwezeshe kujiongezea kipato na kutunza familia, ni uimbaji. Mwisho wa mwezi huu, Lulu anatarajia kuzindua albamu yake ya nyimbo za injili.

Anasimulia kipaji cha uimbaji akisema, anacho tangu utotoni kwani alikuwa mahiri wa kuimba kaswida akiwa Madrasa.

“Nilipookoka, niliendelea na uimbaji kwenye kwaya mbalimbali mjini Songea na mpaka sasa ni mwanakwaya…nina albamu ya nyimbo nane nitaizindua mwezi huu wa Agosti huku Kibamba,” anasema.

Anasema katika albamu hiyo ambayo amemshirikisha kifungua mimba wake, Mariam, upo wimbo ambao ameelezea changamoto, maumivu na shida alizopitia na kisha kuonesha ukuu wa Mungu katika maisha yake.

W anawake wameninyanyua

Mama lishe

Akielezea safari ya maisha yake yenye milima na mabonde, Lulu anasema watu waliomfanya afike kwenye ahueni, wengi ni wanawake wenzake kutokana na kumshika mkono kwa kumuongoza kwenye shughuli mbalimbali za ujasiriamali.

Lulu anashauri wanawake wenye maisha yanayoshabihiana na ya kwake hususani waliotelekezewa watoto, wajane akisema, “usiweke mkono kwenye shavu ukaona huwezi kuvuka changamoto…fursa zipo na zaidi ukimuamini na kumtegemea Mungu.”

Mwanamke huyu ambaye anawashirikisha watoto wake wote shughuli zote za ujasiriamali anazofanya ikiwamo mama lishe, upambaji, ususi bila kujali umri na jinsi, anasisitiza wazazi kuwaandaa watoto kujitegemea katika maisha yao.

Ingawa Lulu anaendelea kupambana na maisha, anasema, “nikilinganisha na safari yangu ya maisha niliyopitia, hivi sasa nina kila ujasiri wa kusema nimepumua. Sina maisha tena ya kuhangaika nile nini, nivae nini, watoto waishije. Mungu amefanya.”

Anatamani kupata wafadhili wa kumwezesha kupata vifaa vyake vya muziki ili ajikite kikamilifu katika muziki wa injili na ushereheshaji wakati akiendelea na ujasiriamali mwingine.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/7a80025251f3df334b3ab115e28328f0.png

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi