loader
FAIZA MOHAMMED  Atimiza ndoto yake kwa vitendo 

FAIZA MOHAMMED Atimiza ndoto yake kwa vitendo 

HUWA ni kawaida mtu kuwa na ndoto yake, ingawa kila mtu hutofautiana na mwingine kwa maana ya namna ya kutimiza ndoto husika.

Wako waliokuwa na ndoto zao na wameweza kuzifanikisha na mmoja wa walioweza kufamikisha vile walivyotamani ni Mkurugenzi wa kampuni ya Fayzoor, Faiza Mohamed.

Faiza tangu utotoni alikuwa mtu wa kupenda kujihusisha na masuala ya urembo.Aliupenda urembo na alitamani siku moja aje kufanya jambo linalohusiana na masuala hayo na leo ameweza kufanikisha kile alichotamani na hadi kufungua kampuni ya utengenezaji wa bidhaa asili za urembo.

Unapokutana na mwanadada huyo, mueonekano wake, unakuthibitishia kuwa ni mdau wa masuala ya urembo kutokana na mvuto wa ngozi na muoenakno wake kwa ujumla. 

Akizungumzia na safari yake katika kutimza ndoto yake hiyo, Faiza anasema kabla hata hajafikisha miaka 10 alikuwa ameshaanza kujua thamani na umuhimu wa urembo na kwamba kila mara alikuwa akimsumbua mama yake akitaka amnunulie bidhaa za urembo.

Anasema alikuwa kwanza hawezi kukaa bila ya kupaka mafuta, poda na bidhaa nyinginezo za urembo na kuwa kadri muda ulivyokuwa ukienda alizidi kupenda bidhaa hizo za urembo.

Hadi mwaka 2012 akiwa kijana wa kuanza kufanya kazi alijikuta akipenda kuwaremba wasichana wenzake kazi aliyoifanya kwa muda mrefu.

Anasema hakuwa na mtaji na wala hakuwaza kuwa kukosa mtaji kunaweza kuwa kikwazo cha kutimiza ndoto yake hiyo, hivyo alitumia vipodozi alivyokuwa navyo kama mtaji wake.

Kwa mujibu wa Faiza alianza kwa kuwaremba wenzake kisha malipo aliyokuwa akipata alikuwa akitumia kuongeza mtaji kwa kununua bidhaa nyingine na kisha kuendelea na kazi yake ya kuwaremba wale waliotaka kurembwa. 

Anasema kukiwa na sherehe kama harusi na hafla nyinginezo alikuwa akiwaremba wasichana wenzake na kuwafanya waonekane warembo kulingana na rangi zao na muonekano.

“Najua mimi siyo kwamba hata hiyo huduma ya kuwatengeneza hao wadada nilikuwa nimeisomea, hapana sikuwahi kuisomea fani ya urembo kabisa kwa maana ya kuingia darasani ila nilikuwa najifunza tu kupitia mtandao wa Youtube… unajua ukipenda kitu, utajitoa mpaka ukifahamu, nilijikuta nikimudu kuwaremba kwa kuwa nilikuwa nina shauku ya kuijua kazi hii, hivyo nilikuwa ninaifanya kwa weledi na moyo wote kiasi cha kupata wateja wengi,” anasema.

Faiza anaongeza kuwa licha ya kuipenda kazi hiyo na kuifanya kwa weledi wote,  lakini ilifika muda akaona ni kama inamchosha kwa kuwa hata malipo hayakuwa kwa wakati na baadhi ya wateja wakiwa hawaoneshi kutambua thamani ya huduma hiyo kama inavyopaswa kuchukuliwa.

Anasema alikuwa akinunua bidhaa mbalimbali za urembo kutoka kwenye makampuni makubwa ya  urembo kwa kuagizia au kwa kununua kupitia wakala hapa nchini na hivyo alikuwa akitumia fedha nyingi lakini aliokuwa akiwahudumia hawakuwa wakiithamini kazi yake kama inavyotakiwa.

Kutokana na changamoto hiyo akakaa chini na kuona kuwa kuna haja ya kubadilisha aina ya biashara kutoka kwenye kuwaremba wateja na kuwafikia wateja hao hao kwa kuwauzia bidhaa zake.

Hapo ndipo likaja wazo la kutengeneza bidhaa za urembo, lengo kubwa likiwa ni kufanya kazi hiyo hiyo ya urembo lakini kwa staili nyingine ambayo kwa sasa ni kuuza bidhaa za urembo.

Anasema mwaka 2014 likaja wazo la kuanzisha kampuni yake ya kutengeneza bidhaa hizo na kuipa jina la Fayzoo ambalo anaona hakika ni jina linaloendana na jina lake, hapo sasa akaanza safari nyingine ya katika masuala ya urembo ambao ni kutengeneza bidhaa.

Faiza anaongeza kuwa wakati huo alikuwa bado akiendelea kuwahudumia wateja wanaotaka kurembwa lakini alikuwa akifanya kazi hiyo huku akiwekeza nguvu kubwa zaidi katika kutengeneza urembo huo wa asili.

Anasema aliamua kurejea tena kwenye mtandao wa Youtube na kuanza kusoma utengenezaji wa bidhaa hizo za asili na kwamba kila siku alikuwa akitumia saa nne hadi tano kusoma.

“Nilikuwa ninasoma kila kitu kuhusiana na biashara ya bidha za asili za urembo, nilianza kwa kusoma kwanza utengenezaji wa bidhaa husika, kusoma fursa zake, namna ya kufungasha kuhudumia na masuala mengine mbalimbali kuhusiana na biashara ya urembo,”anasema Faiza.

Kwa mujibu wa Faiza alianza kwa kutengeneza sabuni za kuogea, mafuta ya nywele ya wanawake na wanaume pamoja na watoto wadogo kisha akaanza kutengeneza shampuu, dawa za kusugua uchafu katika ngozi n.k.

Anasema kuwa licha ya kusoma wengine wanatengenezaji nywele zao, aliamua kutengeneza kwa staili yake hasa kwa kuongeza nakshi pale anapoona panafaa na kuwa  akiona kama kuna haja ya kuongeza kitu kwenye bidhaa au marashi anaongeza ili kuongezea umaridadi wa bidhaa husika.

Faiza anasema alitengeneza bidhaa nyingi kwanza kabla ya kuanza kuuza ili kujipanga kumudu soko na muda wa kuuza ulipoanza, alipata  wateja wengi ikiwa ni miezi sita tu ya kwanza ya kazi yake hiyo.

Mwanadada huyo anasema anamshukuru Mungu wateja wake mbali na kupenda bidhaa zake pia wanaonekana kuvutiwa na vifungashio vinavyotumika kwenye kuhifadhia bidhaa hizo.

Faiza anasema kila siku anapotengeneza bidhaa amekuwa akifanya utafiti kuangalia fursa mpya ya soko na kutengeneza bidhaa kulingana na uhitaji wa soko husika na kuwa siku moja akiwa anazungumza na wateja wake akabaini uhitaji wa dawa za kuotesha ndevu na nywele kwa wale wenye shida ya upara.

“Nilikuwa ninamhudumia rafiki yangu mmoja, huyu ni mwanadada ambaye amekuwa akitumia bidhaa zangu kwa muda mrefu tu na wakati tunazungumza akajikuta akisema kuwa angetamani kupata dawa ya kuotesha nywele za upara kwa ajili ya mpenzi wake… hapo nikaona kuna haja ya kuwa na dawa hiyo lakini nikajiuliza ni kwa nini nisitengeneze ya kuotesha ndevu pia, sasa bidhaa zote nimejikuta ninazitengeneza sasa,” anasema.

Faiza anasema kuna watu mbalimbali wanauza dawa za kuotesha ndevu na kuotesha nywele za kipara lakini dawa hizo zimekuwa na ualakini kutokana na utengenezwaji wake hasa ikizingatiwa kuwa wanatumia kemikali.

Anasema sasa anauza bidhaa zake Kenya na Uganda na kuwa  hapa nchini ana mawakala kadhaa huku akiwa na shauku ya kuanzisha kiwanda cha kuuzia bidhaa zake.

Faiza anasema ameshaanzisha mpango wa kuwa na kiwanda chake, huandaa bidhaa zake kisha kuzipeleka kwenye kiwanda cha watu wengine kwa ajili ya kufanya uzalishaji mkubwa zaidi huku akiwa amefungua duka lake soko la Magomeni.

Huyo ndio Faiza wa Fayzoo aliyekuwa na matamania ya kutimiza ndoto yake na amefanikiwa. Anatoa wito kwa jamii kuwa kama una ndoto, ukaweka malengo, una uwezo wa kutimiza kile unachokiamini na kukikusudia.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/3a324deaadce80abf7b1dc0f3351d72a.jpg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi