loader
Edgar Lungu, Hichilema wameonesha ukomavu kisiasa 

Edgar Lungu, Hichilema wameonesha ukomavu kisiasa 

WIKI iliyopita, wananchi wa Zambia walijitokeza katika vituo vya kupigia kura kutimiza haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua kiongozi wanayemtaka.

Katika uchaguzi huo wa saba tangu nchi hiyo irudi katika siasa za vyama vingi 1991, kinyang’anyiro kigumu kilikuwa katika nafasi ya urais kati ya mgombea wa chama tawala cha Patriotic Front (PF) Rais Edgar Lungu na mgombea kupitia chama kikuu cha upinzani cha United Party for National Development (UPND), Hakainde Hichilema.

Tunawapongeza Wazambia kwa kujitokeza katika vituo vya kupigia kura na kutumia kura zao kumchagua wanayemtaka kupitia uchaguzi huu uliovuta hisia za Wazambia wengi kutokana na sababu mbalimbali huku tukisema, Rais anayemaliza muda wake (Lungu) na Rais Mteule (Hichilema) wameonesha ukomavu mkubwa wa kisiasa Zambia.

Ukomavu huo waliouonesha wanasiasa hao ndio unanifanya tugawe pongezi zangu katika mafungu matatu kwa taifa la Zambia.

Kwanza ninawapongeza Wazambia kwa kushiriki uchaguzi kwa amani na utulivu ulioiwezesha tume ya uchaguzi nchini humo kufanya kazi zake sawia na hatimaye, kutoa matokeo ya uchaguzi huo wa rais.

Pili, nampongeza Rais wa Zambia anayemaliza muda wake (Lungu) kwa uungwana wake na uchungu kwa Wazambia na Waafrika kwa jumla kiasi kwamba, amekubali kushindwa (matokeo) hali inayostawisha zaidi amani nchini humo na demokrasia barani Afrika.

Ninampongeza Lungu nikisema ni mwanasiasa mahiri na mungwana anayejua ukweli kuwa, asiyekubali kushindwa, si mshindani ndio maana kiungawana, amekubali matokeo na hii imezidi kulijengea heshima Bara la Afrika.

Tatu, nampongeza Rais Mteule Hichilema kwa ushindi na kubwa zaidi, kwa kuahidi kushirikiana na Wazambia wote bila kinyongo wala kisasi kwa yeyote maana Zambia ni ya Wazambia wote.

Ndio maana ninawapongeza Edgar Lungu, Hichilema na Wazambia kwa jumla nikisema, huu ni ujasiri na uungwana mkubwa wa kisiasa unaostahili pongezi za dhati.

Wanasiasa wote wa Afrika waendeleze utamaduni huu wa kukubali matokeo na uamuzi wa wananchi kupitia sanduku la kura.

Hivyo, chama au mgombea yeyote anayepewa ushindi na wapiga kura, apewe madaraka kama awe ni wa upinzani, au chama tawala.

Kadhalika, chama tawala katika nchi yoyote kinaposhinda kupitia kura halali za wananchi, kiendelee kutawala hadi wananchi wenye watakapoamua vinginevyo.

Nchi za Afrika ziepuke kulishwa sumu ya kuamini kuwa, ili uchaguzi uwe huru na haki, eti lazima chama tawala kishindwe.

Ndiyo maana ninasema, ninawapongeza Lungu, Hichilema na Wazambia kwa ukomavu wa kisiasa.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/b5515babec7c3a15873c49f3ebd36a59.png

MOJA ya misemo maarufu ya Rais mstaafu Ali Hassan ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi