loader
DK JUDITH YOMBO Akacha ualimu, akamata fursa tiba asili

DK JUDITH YOMBO Akacha ualimu, akamata fursa tiba asili

KAMPENI mbalimbali za afya zimekuwa zikifanywa duniani kupambana na uzito wa mwili, hamasa hiyo inalenga kuwaepusha watu wenye unene uliopitiliza kuingia kwenye athari ya kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Magonjwa hayo ni kama kisukari, presha, ugonjwa wa moyo na mengine mengi ambayo hakika yanaweza kupunguza na kutosumbua kabisa watu, kwani wakipunguza unene basi watajiepusha na magonjwa hayo.

Kampeni hizo za kupunguza unene zimekuwa zikihusisha mazoezi au matumizi ya dawa. Lakini siku hizi dawa za asili zimekuwa zikipewa kipaumbele zaidi, hasa kutokana na usalama wake tofauti na dawa za kisasa. 

Dawa za asili zimekuwa zikitumiwa zaidi katika Bara la Afrika na Asia, kutokana na uwepo wa mitishamba inayoweza kutumika kutengeneza dawa na vitu kwa ajili ya kupunguza unene. Hata hapa nchini wapo wataalamu mbalimbali wa tiba asili, waliosajiliwa kutengeneza bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na unene kwa kutumia mimea inayotokana na mitishamba inayopatikana maeneo tofauti tofauti nchini.

Miongoni mwa wataalamu hao wa tiba asili ni Dk Judith Yombo ambaye ni Daktari wa tiba asili aliyeidhinishwa, Mwanzilishi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa PUBDA CO. Ltd inayotoa elimu juu ya kupunguza mwili na kutengeneza dawa na bidhaa  za kusaidia kupunguza mwili. Maana ya PUBDA ni Punguza Mwili Bila Kutumia Dawa.

Mwanadada huyu alijikuta akiingia kwenye harakati za kusaidia watu kupunguza unene kutokana na kufanya kazi katika ofisi ya bibi yake Secilia Mugorozi, aliyekuwa akitengeneza dawa za kupunguza unene kwa kuchanganya katika maji ya moto na kunywa kama chai.

Baada ya kufanya kazi hiyo kwa muda mrefu kidogo wakati huo akiwa anangojea ajira ya ualimu, alijikuta akiipenda kazi hiyo kwa kuwa hata yeye kipindi hicho alikuwa mnene hivyo alikuwa akitaka kupungua.

Anasema: “Yaani nilikuwa ninaona ni kama najifanyia mimi mwenyewe kazi kwa kuwa nilipoanza kufanya kazi hiyo ya kumsaidia bibi kutengeneza dawa za kunywa kama chai ilikuwa ni nafasi yangu na mimi kuanza kupungua, nilijiona napungua na pia nikawa na wateja wengi.

“Nililazimika kuacha kufanya kwa bibi na kuanza kutengeneza dawa zangu mwenyewe, baada ya kujifunza kutoka kwa bibi, hapo nikawa na wateja wangu na nilianza kuajiri watu wangu, lakini muda huo wote nilikuwa nasubiria ajira ya ualimu.”

Anasema kazi hiyo aliifanya kwa mapenzi makubwa na alianza kupata mrejesho mzuri, huku akiendelea kupata oda zaidi wakitaka watengenezewe, idadi iliongezeka kupita kiwango cha dawa alichokuwa akizalisha.

Dk Judith anasema, ajira zilitangazwa na alichaguliwa kwenda kufanya kazi ya ualimu Wilaya ya Hai, Kilimanjaro na hapo akaona kama ndoto na mapenzi yake kwenye dawa asili yameanza kupungua.

Anasema alijitahidi kukwepa lakini alijikuta akipata shinikizo kutoka kwa watu wa karibu wakiwemo wazazi kuwa ni lazima aende katika kibarua hicho, hivyo alienda na anaongeza kuwa alisikitika kuwaacha wateja wake wapendwa hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa ameanza kuizoea na kuielewa kazi ya tiba asili, lakini akalazimika kwenda Hai.

Kwa mujibu wa Dk Judith, alipofika na kuanza kazi,  akawa anaikumbuka sana kazi yake ya tiba asili na kuna muda akawa anaona ni kama vile amefanya kosa kusomea ualimu na kuwa kama angejua mapema angesomea tiba asili.

Anasema kuwa kuna siku alikuwa akipokea simu za wateja wake wengine wakiwa wanataka kuchukua idadi kubwa ya dawa hizo huku wengine wakiwa wanataka kuonana naye kwa kuwa alikuwa ameshaanza huduma ya kutoa ushauri wa tiba asili.

Anaongeza kuwa mwaka 2018 aliamua kuacha kazi ya ualimu aliyoifanya kwa mwaka mmoja na kurejea tena Dar es Salaam kuwahudumia wateja wake huku akijua fika kuwa atajipanga na kazi hiyo kuwa ya kitaalamu zaidi ili apate soko la uhakika.

Anasema baada ya kuacha kazi na kurejea Dar es Salaam kuanza kazi ya kutengeneza tiba asili, wazazi wake na ndugu wa karibu hawakumuelewa kabisa kwa kuwa kwao walikuwa wakiichukulia kazi ya tiba asili kama siyo sawa na hiyo ya ualimu ndio kazi nzuri zaidi tena akiwa mwajiriwa wa serikali.

Dk Judith anasema kuwa kikubwa alichoamua ni kuhakikisha kuwa hajutii uamuzi wake huo wa kuacha kazi ya ualimu hivyo alianza kujipanga kwa kutengeneza dawa nyingi za tiba asili kwa lengo la kuwawezesha watu kupungua badala ya kuendelea kutumia majani ya chai pekee kupunguza mwili ambayo alijifunza kutengeneza kutoka kwa bibi yake. 

Hivyo mwaka 2019, ikiwa ni mwaka mmoja tangu kuacha ualimu, aliamua kwenda kusoma kozi fupi ya utengenezaji wa tiba asili katika Chuo cha Tiba Asili kilichopo Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili (Muhas) ambapo anasema baada ya kuanza kusoma kozi hiyo alianza kuuona mwanga wa mafanikio mapema katika maisha yake.

“Kwa kuwa tayari nilikuwa nimeshaingiwa na mapenzi ya kazi hii ya kutoa tiba asili na kuona matokeo yake kwa kuwa ilianza kuwasaidia watu kupungua, tena hapo nilikuwa natumia majani ya chai ya asili tu, sasa nilipoanza kuisomea nikaona hakika naenda kusaidia wengi zaidi, kwa kuwa kozi hiyo ilihusisha masuala mengi zaidi ya kupunguza mwili,” anasema mwanadada huyo.

Anasema mwezi wa kwanza wa mafunzo akabaini kuwa kuna uwezekano wa kutengeneza mkate na uji kuwasaidia wanaotaka kupunguza mwili, akabaini kuna uwezekano wa kutengeneza dawa za kutoa mabaki ya uchafu mwilini kwa njia mbalimbali na namna ya kupunguza watu uzito kwa kutumia juisi pamoja na njia nyingine mbalimbali.

Dk Judith anasema kuwa aliona fedha alizokuwa ametunza kwa ajili ya kusoma chuo hicho hazijapotea bure ila zinaweza kumpanulia wigo wa kuelewa zaidi kutengeneza bidhaa nyingi na kupata fedha zaidi, hapo akaanza kutengeneza bidhaa hizo kabla hata ya kumaliza chuo.

Anasema kuwa alikuwa akitoka darasani anakwenda moja kwa moja kuanza kujaribisha alichofundishwa hasa utengenezaji wa dawa nyingine za asili ambazo alikuwa hazijui zinavyotengenezwa, hatua hiyo ilimweka karibu zaidi na wateja wake ambao awali walikuwa wakinunua dawa moja tu kutoka kwake.

Anaongeza kuwa alianza kuingiza fedha akiwa chuo kwa kuwa alikuwa akiwauzia wateja wake kwa wingi na ikafika wakati akaamua kujiongeza kwa kutafuta vifungashio vyenye ubora na mvuto zaidi.

Dk Judith anasema aliendelea kutengeneza na kuuza bidhaa kwa wingi huku akiimarisha nidhamu kwenye utunzaji wa fedha kwa kuwa alilenga kuanzisha kiwanda kabisa cha kutengeneza bidhaa za tiba asili.

Anasema wakati anamaliza miezi tisa ya kusoma chuoni hapo alikuwa ameshatunza fedha za kutosha kumwezesha kuanzisha kiwanda chake kidogo na sasa ndoto yake imekamilika kwa kuwa ameanzisha kiwanda hicho Tabata Chama, Dar es Salaam na anazalisha bidhaa nyingi kwa ufanisi kutokana na kufunga mashine za kisasa.

Ameajiri wafanyakazi nane na ana vijana wengine wengi wakifanya kazi ya uwakala, gazeti hili lilishuhudia bodaboda zikiwa zimebeba makasha ya kusambazia bidhaa zake hizo za tiba asili.

Anasema: “Sasa hivi ninatengeneza unga wa uji maalumu kwa watu wanaotaka kupungua na pia nina mikate inayotengenezwa kwa unga wa lozi (almond) ambao haunenepi kama ilivyo kwa vyakula vya ngano, ninatengeneza dawa za kutoa uchafu mwilini na mtumiaji anatumia kwa wiki mbili na zipo za mwezi mzima.”

Kwa mikoani, anasema, “kampuni ina mawakala kila mkoa na tena tunauza hadi Kenya na Uganda kwa kuwa watu wanatumia bidhaa hizi hakika wameona mafanikio yake na wanaofuatilia kupitia mtandao wa instagram wa Punguza_Uzito_bila_dawa, ninajipanga kujiendeleza kiujuzi zaidi.”

Dk Judith anasema wako wateja wake wa mwanzo kabisa wakati anaanza biashara wengine wamekuwa mawakala wa kuuza bidhaa zake.

Anasema kuna wakati anapigiwa simu na watu mbalimbali ambao wanafika kwenye ofisi yake Mwenge kununua bidhaa ambapo hulazimika kuwashauri aina ya bidhaa wanayopaswa kuanza nayo na anaongeza kuwa wapo ambao akiwaangalia anawashauri kuanza kupunguza tumbo kwanza na wengine anawapatia ya kupunguza mwili mzima.

Anasema kwa miaka mitano ambayo amekuwa akifanya kazi ya utengenezaji na uuzaji wa bidhaa za asili, hajawahi kujutia uamuzi wake wa kuacha kazi ya ualimu badala yake anaona kuwa sasa amekuwa mwalimu mzuri wa kuwaelimisha na kuwasaidia watu kupunguza mwili.

Dk Judith anawataka Watanzania na watu wengine kutumia bidhaa za asili kupunguza mwili badala ya kutegemea bidhaa kutoka nje ya nchi.

Mwanadada huyo mrembo, anaishauri serikali kuendelea na sera zake za kutoa kipaumbele kwa tiba asili hasa kwa kuhamasisha matumizi ya dawa asili kupunguza mwili.

Kuhusu bibi yake

Dk Judith anasema kuwa bibi yake Secilia Mugorozi kwa sasa anajisikia faraja kuona kazi anayoifanya (Judith) na kuwa anapenda zaidi kutumia bidhaa za mkate na maziwa kwa kuwa ni rafiki kwa afya na anaongeza kuwa kitendo cha bibi yake kufurahia  bidhaa hizo kwake yeye Dk Judith inakuwa ni faraja inayompa hamasa ya kujipanga ili siku zijazo atengeneze kitu bora zaidi.

Maisha binafsi na elimu

Mwanadada huyu amefanya haya yote makubwa akiwa na miaka 27 tu, amezaliwa Septemba 16 mwaka 1994 Mwanza, Bugando. Mwaka 2007, alimaliza elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Nyegezi.

Sekondari alisoma katika Shule ya Nyabulogoya na Elly iliyopo Bunda mkoani Mara na kumaliza mwaka 2011, kisha akakaa na bibi yake mwaka mzima 2012 akijifunza na kumsaidia masuala hayo ya tiba asili.

Mwaka 2013 hadi 2015, akajiunga na Chuo cha Ualimu Ndala mkoani Tabora ambapo alipohitimu mwaka huo wakati akisubiri ajira alirejea kwanza kwenye tiba asili na kuendeleza ujuzi kabla ya kuja kuajiriwa na kisha kuuacha ualimu moja kwa moja na kujiajiri ndiyo hadi leo anaendeleza kazi.

Dk Judith anasema kuwa mbali na kufanya kazi zake za tiba, anapenda kujisomea masuala mbalimbali ya tiba kimataifa, anapenda kusikiliza muziki, kusoma vitabu, kupiga picha na kubadilishana mawazo na watu wengine mbalimbali ya maisha.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/67aa4ed0fc27a6acefb0a5d28eb5db48.jpg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’in

2 Comments

 • avatar
  Adrian Mbilinyi
  22/08/2021

  Dr Yudith Yombo tupe namba ya simu yako ili tuwasiliane maana dawa zako za asili ndiyo muhimu

 • avatar
  Joseph kiyenze
  18/03/2022

  Dr Kwanza nikupungeze Sana kwa jihada kubwa uliyoishe kutimiza doto yako naomba kuwasiliana nawe wa WhatsApp naomba yangu ni 0710911591/0693121648

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi