loader
Dstv Habarileo Mobile
Tanesco, TRA wafafanua kuhusu kodi ya majengo

Tanesco, TRA wafafanua kuhusu kodi ya majengo

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limeelekeza wanaotaka kununua umeme mwezi huu wahakikishe wananunua wa zaidi ya Sh 2,000 waweze kulipa kodi ya majengo ya mwezi huu na uliopita ambayo imeanza kukatwa kupitia mfumo wa luku za umeme.

Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) imetolea ufafanuzi masuala mbalimbali yahusuyo kodi hiyo ya majengo ikiwamo mkanganyiko kuhusu ulipaji wa kodi hiyo kwenye nyumba zenye hadhi tofauti, nyumba zinazomilikiwa na wazee na wale wenye misamaha ya kodi.

Taasisi hizo zilitoa ufafanuzi kwenye mjadala wa kitaifa kuhusu ulipaji kodi ya majengo kwa njia ya ‘luku’ ya umeme uliofanyika kwa njia ya mtandao.

Akizungumzia kuanza kukatwa kwa kodi hiyo kwa njia kupitia mita hizo za umeme, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Huduma kwa Wateja wa Tanesco, Martin Mwambene, alisema makato hayo ya kodi ya majengo ni Sh 1,000 kwa kila mwezi wa Julai na Agosti.

Mjadala huo umefanywa kutokana na uwepo wa maswali mengi kutoka kwa wateja mbalimbali wa shirika hilo walionunua umeme jana na kubaini kuwa wamekatwa Sh 2,000 kwenye manunuzi huku wengine hawakupata umeme baada ya kununua umeme wa Sh 2,000.

Wakati Mwambene akisema hayo, mtandao rasmi wa kijamii wa Twitter wa Tanesco umeweka taarifa kwa umma ikiwajulisha kiasi cha fedha wanachopaswa kuwa nacho iwapo wananunua umeme mwezi huu.

“Ndugu mteja, ili uweze kupata umeme kwa mwezi huu #Agosti, tunakushauri ununue umeme wa zaidi ya shilingi 2,000 ili uweze kulipa kodi ya majengo ya mwezi Julai (1,000/=) na Agosti (1,000/=),” ilisema taarifa ya Tanesco katika ukurasa wake wa Twitter.

Awali, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akizungumzia tozo na kodi mbalimbali zilizoanza kukatwa Julai mwaka huu, alisema zimeanza kukatwa Julai 15 mwaka huu, na nyingine zimeanza kukatwa Agosti hii kwa mujibu wa sheria.

Mwambene alijibu maswali ya wateja kwenye mdahalo huo akisema utaratibu wa kulipia kodi ya majengo kwa njia ya mfumo wa luku umeanza Agosti 20,2021 na utakuwa ukitekelezwa kwa njia hiyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alifafanua katika mdahalo huo kuwa, kwa kipindi cha mwaka mmoja mlipaji atakuwa ametozwa Sh 12,000 ambayo ndiyo kodi ya jengo kwa nyumba za kawaida.

Kwa jengo la ghorofa, lililo kwenye mji, manispaa na jiji, kila sakafu inatozwa kwa mwezi kwenye luku Sh 5,000 ili ndani ya mwaka mlipaji awe amelipa Sh 60,000 ambayo ndicho kiwango cha kodi kwa nyumba ya mtindo huo.

Aidha nyumba ya ghorofa zilizopo wilayani, halmashauri na mikoani zitalipa Sh 12,000 kama nyumba za kawaida bila kuja idadi ya sakafu zilizopo katika jengo hilo la ghorofa.

Alisema wastaafu, wazee wenye umri kuanzia miaka 60 na kuendelea wako kwenye kundi la msamaha na wataendelea kupata msamaha huo wa kodi ya majengo kwenye nyumba za makazi wanayoishi wenyewe.

Alisema utaratibu wa kupata msamaha bado unaendelea na ni wa mtu yeyote aliyekidhi vigezo vya msamaha wa kodi ya majengo kwa mujibu wa sheria.

“Kundi la msamaha ni wazee wote wenye kumiliki nyumba ambazo wanaishi wao wenyewe na isiwe nyumba ya biashara au yenye fremu ya biashara, iwe ya makazi pekee na msamaha utahusu nyumba tu,” alisema Kayombo.

Alifafanua kuwa kwa wastaafu au wazee wenye umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea ambao wana nyumba zaidi ya moja na kila moja, ina jina lake la wahusika, msamaha huo unawahusu pia.

Kuhusu mteja atakayekatwa kimakosa kwenye luku, ilifafanuliwa kwamba anapaswa kutoa taarifa ofisi ya TRA akiwa na nyaraka na kiasi kilichokatwa kitaingizwa kwenye umeme wa luku yake Kayombo alisema nyumba za nyasi na udongo na zile zilizojengwa kwa vifaa visivyodumu hazipaswi kulipiwa kodi ya majengo.

Kwa upande wa nyumba zisizo na umeme ambazo zipo kwenye kundi la kulipa kodi, zinapaswa kulipa na mmiliki ana wajibu wa kufuata ankara ya malipo TRA.

Kuhusu nyumba moja yenye mita zaidi ya moja, Kayombo alifafanua kuwa kodi hiyo italipiwa kupitia luku moja na ikiwa mteja ametozwa kwenye mita zaidi ya moja atapaswa kuwasilisha taarifa TRA ili makato yaelekezwe kwenye moja.

Kuhusu kiwanja kimoja kuwa na nyumba zaidi ya moja, ufafanuzi ni kuwa kila nyumba inapaswa kulipiwa kodi ya jengo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/4ffd3a8638b64c5a44e6373a9edbaacf.jpg

WASICHANA waliopata ujauzito katika umri mdogo ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

2 Comments

 • avatar
  Victoria funga
  04/09/2021

  Nafanyaje nataka kulipa kodi ya nyumba ya mwaka mzima, ili nisiwe nakatwa kwenye umeme?

 • avatar
  Victoria funga
  04/09/2021

  Nafanyaje nataka kulipa kodi ya nyumba ya mwaka mzima, ili nisiwe nakatwa kwenye umeme?

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi