loader
Dstv Habarileo  Mobile
Viwanda vidogo vitamaliza uhaba wa sukari nchini

Viwanda vidogo vitamaliza uhaba wa sukari nchini

MWISHONI mwa mwaka huu wa fedha, mtambo wa awali wa kuzalisha sukari utakaoendeshwa na wakulima wadogo utakamilika ikiwa ni hatua ya kuanzisha viwanda vidogo vya sukari nchini.

Hatua hiyo inalenga kumaliza uhaba wa sukari uliopo kwa matumizi ya ndani wa zaidi ya tani 300,000.

Wizara ya Viwanda na Biashara inasema lengo ni kufikia tani zaidi ya 700,000 ifikapo mwaka 2025.

Hivi karibuni Mkurugenzi wa Taasisi ya Uhandisi na Ubunifu Mitambo Tanzania (Temdo), Profesa Frederick Kahimba, alinukuliwa akisema hatua hiyo ni utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo chini ya Dira ya Taifa ya Mwaka 2025.

Mpango huo unalenga kujenga uchumi shindani wa kutegemea viwanda kwa maendeleo ya taifa.

Alisema mitambo hiyo midogo imewalenga wakulima wadogo katika maeneo yanayozalisha miwa kwa wingi ikiwamo mikoa ya Morogoro, Kilimanjaro na Kagera.

Kahimba anasema mitambo hiyo midogo ya kuzalisha sukari imewalenga wakulima wadogo katika maeneo yanayozalisha miwa kwa wingi watakaojiunga kwa kushirikiana na wawekezaji wa ndani na nje kununua mitambo hiyo.

Mtambo mmoja utauzwa kwa Sh milioni 250. Mtambo kama huo ukiagizwa nje ya nchi, hugharimu Sh milioni 400 hadi milioni 500.

Mtambo wa awali utakamilika mwishoni mwa mwaka huu wa fedha. Hadi sasa uundwaji wa mtambo huo wa awali umefikia asilimia 40.

Taarifa ya Wizara ya Viwanda na Biashara inaonesha kuwa, wakulima wa miwa wanapoteza zaidi ya Sh bilioni 19 kutokana na sukari zaidi ya tani 200,000 kubaki kwa wakulima kwenye miwa inayoshindikana kuuzwa kiwandani kwa kuwa mahitaji si makubwa. 

Ndiyo maana ninasema, viwanda vidogo vitamaliza uhaba wa sukari nchini, hivyo wakulima wadogo waichangamkie ipasavyo.

Kwa mujibu wa Profesa Kahimba, mtambo mmoja utamwezesha mkulima kuzalisha tani moja ya sukari katika tani 10 za miwa kwa saa.

Hiki ni kiasi kikubwa kitakachosaidia nchi kujitosheleza kwa sukari na ziada kuuzwa nje.

Tayari wakulima wameonesha mwamko mkubwa na kuipongeza serikali kwa kuweka nguvu kwa wakulima wadogo hasa kutokana na kuwapo  kwa uchache wa viwanda vya sukari nchini unaosababisha kutokuwapo soko la ushindani sambamba na kusababisha uhaba mkubwa.

Pongezi hizi za wakulima wa Muungano wa Vyama vya Ushirika vya Mazao (Amcos) wilayani Misenyi mkoani Kagera ziwekwe katika vitendo na maandalizi yaanze mapema ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya kununua mitambo hiyo.

Kazi hii inayofanywa na Wizara ya Viwanda na Biashara ikiwa ni utekelezaji wa vipaumbele 15 vilivyo katika bajeti ya wizara ya mwaka wa fedha 2021/2022, inapaswa kusimamiwa vizuri ili kumaliza kabisa uhaba wa sukari nchini.

Ndio maana ninasema, Viwanda vidogo vitamaliza uhaba wa sukari nchini.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/92acb9fc801c84df13c527262690ecae.jpeg

WIKI iliyopita umefanyika uzinduzi wa siku ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi