loader
Uhusiano wa tozo na maendeleo ya wananchi

Uhusiano wa tozo na maendeleo ya wananchi

MIONGONI mwa mambo yaliyoshika nafasi kubwa ya mijadala mitandaoni kwa sasa ni suala la tozo ya miamala ya simu kwa kutuma na kupokea pesa nchini.

Kodi, ikiwemo tozo hizi za miamala hutumika kama njia ya uongezaji wa mapato ya ndani ya nchi.

Lakini uwepo wake umekuwa ni tatizo kwa nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kama alivyobainisha Drummond na wenzake mwaka 2012, licha ya  ukweli kwamba kodi na tozo ndiyo njia kuu ya kupunguza utegemezi wa misaada ya kigeni na kuifanya Serikali ziweze kutoa huduma muhimu kama vile maji, afya, shule na barabara kupitia makusanyo ya kodi.

Wakati hali ya sintofahamu ya tozo kwenye miamala ilipojitokeza, Rais Samia Suluhu Hassan, aliweka bayana kuwa tozo zitaendelea kuwepo kwa kuwa Watanzania wamezielewa isipokuwa tu serikali itazitazama upya tozo hizo.

Rais Samia aliyasema hayo alipowaapisha mabalozi wateule Ikulu Dar es Salaam mwezi Julai sambamba na alipofanya mahojiano na Mwandishi wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC), Salim Kikeke. 

Katika hotuba yake kwa Watanzania kupitia kwa mabalozi hao, Rais alisema: "Ninachotaka kusema makato haya yaliwekwa kwa nia njema tu. Nchi yetu sasa hivi wakulima wameamka na kilimo kikubwa lakini wakivuna wanashindwa kutoa mazao yaliko kuleta kwenye maeneo ya masoko, tatizo ni njia za vijijini hakuna, kwa hiyo sehemu ya fedha hii au sehemu kubwa itakwenda kujenga njia za vijijini tuwafanye wakulima watoe mazao walete kwenye masoko wafaidi jasho lao lakini na bidhaa zile zisiwaharibikie mikononi ziende kwenye masoko."

 

Na katika kusisitiza hili la tozo, akijibu swali la Salim Kikeke kuhusu malalamiko ya wananchi juu ya tozo, Rais alisema wananchi hawakulalamikia tozo bali wamelalamikia kiasi cha makato.

Baada ya taratibu za ndani kukamilika baada ya ripoti ya ukusanyaji maoni kutoka kwa wananchi mbalimbali kupokelewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jana wakati makala haya yanaandikwa, serikali ilitarajiwa kuja na tozo mpya za miamala zenye unafuu.

Lakini swali linabaki ni kwa kiasi gani wananchi wameelewa tozo hizi na umuhimu wake kwa maendeleo ya nchi na mtu mmoja mmoja? Nadhani hili ndilo swali la msingi ambalo linapaswa kujengewa hoja.

Kwa mtazamo wangu, shida haipo kwenye tozo yenyewe tu bali ipo kwenye elimu juu ya namna gani tozo hizi zinatumika. Pamoja na kupunguza tozo za miamala ni muhimu elimu zaidi kutolewa ili kusiendelee kuwepo malalamiko kwa baadhi ya watu.

 

Kimsingi, shida kubwa ya nchi za Afrika ni ukwepaji wa kodi na kwa kweli hili linarudisha sana nyuma maendeleo ya Afrika. Hili lilibainishwa katika ripoti ya IMF ya mwaka 2011. 

Lakini pia si Afrika tu bali ni duniani kote ukwepaji wa kodi ni mkubwa kama walivyobainisha McKerchar na Evans mwaka 2009, isipokuwa tu nchi za Afrika ndizo zinazoongoza kwa tatizo hili la ukwepaji kodi. Haya yalibainishwa na Cobham (2005), Fuest na Riedel (2009). 

Kwa kuangalia tafiti hizo, tunaona kuwa shida kubwa ya nchi zinazoendelea kiuchumi duniani na hasa hizi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ni wananchi kukwepa kodi baadhi wakifanya hivyo kwa kutoona matokeo ya kodi wanazolipa.

Tafiti mbalimbali zilizofanywa na Kamasa na wenzake (2019), Merima na wenzake na Abdu na wenzake (2020) zote zimeonesha kuwa wananchi wamekuwa wakikwepa kodi au kuwa na tabia ya kutolipa kodi kwa sababu hawaoni au hawaelezwi matokeo ya moja kwa moja ya kodi wanazolipa.

Licha ya mtazamo huo, kwa mtazamo wangu mimi naona kwamba si kuwa hawaoni matokeo ya kodi wanazolipa bali Serikali za nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara hazifanyi juhudi za dhati kuwafikia wananchi hasa wa vijijini na kuwaelimisha juu ya uhusiano uliopo kati ya kodi wanazotozwa na kile wanachoona kinafanywa na serikali katika maeneo yao ikiwemo ujenzi wa shule, hospitali, vituo vya afya, maji na barabara.

 

Hivyo, hatua inayochukuliwa na Serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu, kutangaza makusanyo yaliyopatikana kupitia tozo za miamala na mgawanyo wake katika ujenzi wa vituo vya afya na shule ni hatua kubwa na muhimu sana.

Mimi ninashauri hatua hii isiishie kwa Dk Nchemba na Waziri Ummy, bali iende kwa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, madiwani, wenyeviti wa serikali za mitaa na wenyeviti wa vijiji. 

Nafahamu kuwa baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya wameanza kufuata mkondo huo lakini bado mikoa mingine na wilaya ambako pesa hizo zimepelekwa wana wajibu wa kufanya hivyo.

 

Madiwani wa kata husika ambao kata zao zimepatiwa fedha za ujenzi wa majengo ya shule au vituo vya afya wana wajibu pia wa kuitisha vikao na kuwaeleza wananchi wao kuwa fedha hizo walizopokea zimetokana na tozo za miamala ya simu na endapo kuna fedha nyingine wanatarajia kupokea mwezi au miezi inayokuja wawaeleze pia wananchi. Ifanyike hivyo pia kwa wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji ambavyo miradi hiyo inafanyika.

 

Tatizo lingine la nchi zetu Afrika limekuwa linatajwa na wasomi katika tafiti zao kuwa ni utekelezaji wa sera na si kukosa sera nzuri. Utekelezaji huu wa sera hupata changamoto zaidi kwa sababu hakuna uelewa wa pamoja baina ya wananchi na serikali juu ya nini Serikali imekipanga au inafanya kwa wananchi wake. 

 

Kwa kifupi ni kwamba, serikali inajua nini inataka kufanya kwa wananchi wake lakini kutokana na kukosekana kwa ufikishwaji sahihi wa kile ambacho serikali inakipanga au inakifanya wananchi wanakuwa hawaelewi dhamira  ya serikali zao. Hili liliwahi kubainishwa pia katika utafiti wa OECD na SIDA.

 

Utafiti uliofanywa na Kamasa na wenzake (2019) (Tax Compliance in Sub-Saharan Africa: How Important are Non-Pecuniary Factors?) katika nchi 29 za Afrika ulibainisha kuwa tatizo la ufahamu juu ya kodi na umuhimu wake kwa maendeleo, kutokuwa na imani na usimamizi wa kodi, na kwamba utoaji wa huduma za afya elimu na mahitaji ya barabara yanatoa uwezekano mkubwa kwa wananchi kupenda kulipa kodi katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

 

Kwa kuonesha umuhimu wa serikali kutoa mrejesho kwa wananchi mpaka vijijini juu ya uhusiano wa huduma za afya, elimu, barabara na kodi wanazotozwa wananchi Merima Ali na wenzake nao walitumia utafiti wa Mzunguko wa 5 wa Afrobarometer kueleza sababu zinazofanya wananchi wasipende kulipa kodi katika chapisho lao (Factors affecting tax compliant attitude in Africa: Evidence from Kenya, Tanzania, Uganda and South Africa').

 

Lakini zaidi Abdu na wenzake (2020) waliongeza kwa kuitazama rushwa kama chanzo cha ukwepaji kodi katika utafiti wao 'Analysis of Tax Compliance in Sub-Saharan Africa: Evidence from Firm-Level Study.' 

Hivyo basi kodi ya tozo za miamala kwa kiasi fulani itasaidia kupunguza nakisi ya kutofikia malengo ya ukusanyaji kodi kila mwaka wa fedha wa serikali inayosababishwa na ukwepaji kodi kutokana na rushwa licha ya uwepo wa sababu nyingine.

 

Ninaamini kuwa kama elimu hii ya uhusiano uliopo baina ya tozo za miamala na fedha zinazogawanywa kwa maeneo husika nchini ukielezwa kwa kina mpaka vijijini, wananchi wataongeza uelewa na kupenda kulipa kodi, si tu kupitia miamala bali hata zile kodi nyingine. 

Ni muhimu wananchi wajue kwamba nchi inavyojengwa ni kama nyumba pia. Kwamba mtu ukitaka kujenga nyumba utadunduliza ukijinyima mpaka utajenga, ni sawa na tozo.

Sababu nyingine inayonifanya niamini kuwa kunahitajika elimu ya kina juu ya uhusiano wa tozo za miamala na huduma kama shule, vituo vya afya na barabara ni kwamba nchi 11 duniani ndizo zinazoongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha kutoza kodi lakini ndizo zenye huduma bora kwa wananchi wao.

Ripoti ya OECD ya mwaka 2013 na 2016 inazitaja nchi za Denmark, Norway, Marekani, Canada, Switzerland, Iceland, Uingereza, Luxembourg, Sweden, Ubelgiji na Finland kuwa ndizo zenye kiwango kikubwa cha kodi duniani. Lakini tujiulize nchi hizi si ndiyo zinakamuana kodi mpaka kufikia kutupa sisi misaada? Sisi hatuwezi kujihudumia kwa kodi zetu?

 

Kwa mfano, nchi ya Finland ina makato ya kodi mbalimbali kati ya asilimia 25 mpaka 40 katika kodi yao ya Mapato ya Taifa (National Income Tax), rejea ripoti ya Taxation in Finland.

 

Kwa msingi huo, naamini kabisa tatizo halisi la tozo za miamala ni sisi wananchi kuelewa uhusiano uliopo kati ya tozo na huduma zinazotolewa. Muhimu zaidi ni serikali kutoa huduma bora za afya, elimu, maji na barabara ili wananchi waone uhusiano wa kodi na matokeo ya kodi kwa macho yao.

Merima Ali na wenzake walibainisha katika ukurasa wa 7 wa utafiti wao kwa kusema: 'Nchini Tanzania asilimia 16 ya waliohojiwa waliona kwamba huduma zisizoridhisha za huduma za jamii ni sababu kubwa inayowafanya watu wakwepe kulipa kodi.

Kwa mantiki hiyo kuna umuhimu wa serikali kuendelea kutoa huduma bora za afya, elimu, maji na barabara lakini pia serikali iwajengee wananchi uelewa juu ya nini kinafanywa na kodi au tozo wanazokatwa.

Mwandishi wa makala haya ni mwanazuoni na mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni +255  719 258 484

foto
Mwandishi: Abbas Mwalimu 

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi