loader
Dstv Habarileo  Mobile
Dk Mpango aitaka Jumuiya  ya  kimataifa kuwekeza kilimo

Dk Mpango aitaka Jumuiya  ya kimataifa kuwekeza kilimo

TANZANIA imeitaka jumuiya ya kimataifa kushughulikia namna ya kuwekeza katika kilimo ili kiwepo chakula cha kutosha duniani.

Ushauri huyo umetolewa na Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango wakati akizungumza katika Jukwaa la Mapinduzi ya Kijani barani Afrika(AGRF)  mwishoni mwa wiki.

Alisema Tanzania imedhamiria kuhakikisha kwamba inajibidiisha kwenye kilimo chake na kuboresha mifumo ili kuhakikisha usalama wa chakula na hivyo kuboresha ustawi wa jamii.

Akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo kwa njia ya video, Dk Mpango alisema Tanzania imeshatengeneza na kuboresha mifumo ya uwekezaji ili kilimo kiendelee kukua.

Kwa mujibu wa Dk Mpango, uwekezaji na hasa fedha ni muhimu kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla katika kuhakikisha mfumo wa chakula unakuwa salama.

Alishauri katika mkutano ujao wa Umoja wa Mataifa wa mifumo ya chakula duniani unaotarajiwa kufanyika Jiji la New York, Marekani Septemba 23 mwaka huu, kujikita zaidi katika uwekezaji kwenye kilimo ili kukibadili na kuwa chenye tija.

Alisema katika mkutano huo wa kimataifa wa New York, Tanzania itazungumzia upatikanaji kirahisi wa mbegu bora, viuatilifu na kuimarishwa kwa utafiti na uhawilishaji wa teknolojia za kilimo na ufugaji kwa wakulima.

Dk Mpango katika mkutano huo wa Nairobi aliungana na viongozi wengine wa Afrika kujadili mkakati wa Afrika wa kubadili kilimo na kuweka usalama wa chakula. Viongozi hao ni  Uhuru Kenyatta (Kenya), Paul Kagame (Rwanda), Dk Lazarus Chakwera (Malawi), Yoweri Museveni (Uganda), na Hage Geingob wa Namibia.

Wengine waliohudhuria mkutano huo ni Rais wa IFAD, Gilbert Houngbo, kamishina wa uchumi wa vijijini na kilimo katika kamisheni ya  Umoja wa Afrika, Josefa Sacko; Mtaalamu mwandamizi wa masuala ya jinsia katika mradi wa UNDP-GEF, Salamatu Garba na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Akinwumi Adesina.

Rais Kenyatta alisema mkutano wa AGRF  unaweka pamoja sauti ya Afrika kabla ya mkutano wa dunia wa mifumo ya chakula utakaofanyika Septemba 23.

Meneja Mkazi wa  Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA) nchini Tanzania, Vianey Rweyendela alipongeza ushiriki wa Makamu wa Rais katika mkutano huo na kusema aliiwakilisha vyema Tanzania.

“Kwa sasa Tanzania ipo katika njia nzuri ya kuimarisha kilimo na mifumo ya usalama wa chakula kiasi cha kuweza kupata masoko ya kimataifa na Makamu wa Rais anapeleka salamu nzito kwa dunia,” alisema.

Wakati huo huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Profesa Siza Tumbo,  alisema kwamba  serikali inataka uwekezaji katika sekta ya kilimo ili kuongeza tija na hivyo kulisha viwanda vya ndani na soko la nje.

Alisema katika mkutano  huo wa Nairobi kuwa Tanzania imekuwa nchi ya amani tangu uhuru wake na kwamba sasa sera na mazingira ya uwekezaji ni mazuri zaidi. 

Mkutano wa AGRF  ulkioandaliwa na Agra na kufanyika mjini Nairobi, Kenya kwa njia ya mtandao ulishirikisha wajumbe wengi duniani kutokana na  janga la Covid-19.

Alisema wakulima wadogo nchini Tanzania sasa wana elimu ya kutosha kuhusu kilimo biashara wanachotaka ni mitaji ya kuwezesha kupatikana kwa tija na kuongeza shughuli zao.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/1816403a0603c546a7788881b9648f07.jpg

WASICHANA waliopata ujauzito katika umri mdogo ...

foto
Mwandishi: Na Mwandishi wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi