loader
Dstv Habarileo  Mobile
Epidemiolojia: Mfumo uliofanikisha udhibiti wa magonjwa

Epidemiolojia: Mfumo uliofanikisha udhibiti wa magonjwa

‘ EPIDEMIOLOJIA’ ni sayansi ya afya ya jamii inayohusika na mgawanyiko wa magonjwa na vinasaba. Sayansi hii imekuwa ikitumika duniani kote kwa ajili ya ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa pale mlipuko unapotokea kwa kuchukua taarifa na sampuli kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara.

Mfumo huo ulianza kutambulika mwaka 1854 nchini Marekani baada ya uchunguzi wa mwanasayansi maarufu, John Snow, kugundua chanzo cha maambukizi ya kipindupindu na kuleta matokeo makubwa katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Maadhimisho ya Siku ya Epidemiolojia kwa mara ya kwanza yamefanyika Septemba 7, mwaka huu (2021) hapa nchini ikiwa ni hatua ya kutambulika mchango wa wataalamu wa sayansi hiyo ambao huitwa Waepidemiolojia.

Waepidemiolojia ni wataalamu wenye ujuzi wa kutambua magonjwa na wanahusika na uchunguzi wa viashiria vya milipuko ya magonjwa na kufanya uhakiki, kutambua waathirika, watu wa karibu na waathirika na visababishi vya magonjwa.

Ujumbe wa maadhimisho haya kwa mwaka huu 2021 ni “Kuimarisha Mifumo ya Ufuatiliaji wa Matukio ya Kiafya ili kubaini haraka Matishio ya Kiafya katika Jamii”

JINSI WANAVYOFANYA KAZI

Rais wa chama cha wataalamu wa udhibiti na ufuatiliaji wa magonjwa kupitia mbinu ya epidemiolojia na maabara (TANFLEA), Dk Elibariki Mwakapeje, anasema wanafanya kazi na serikali na wadau katika kuzuia na kupambana na matishio dhidi ya afya ya jamii. Anasema kazi nyingine ni kutengeneza kanzidata ya wanaepidemiolojia wanaoweza kutoa huduma ya kitaalamu katika nyanja za epidemiolojia na maabara.

“Nyingine ni kusaidia kuhamasisha na kujenga uwezo katika nyanja za epidemiolojia na maabara, afya na kutoa machapisho ya kitafiti na ya kitaaluma katika majarida ya kitaaluma. “Pia kutafuta fursa za ufadhili kutoka kwa wadau kwa ajili ya shughuli za afya ya jamii,” anasema Dk Mwakapeje.

TAFITI 100 ZAFANYIKA

Miongoni mwa mafanikio makubwa kwa taaluma hiyo ya epidemiolojia ni kufanya tafiti 100 zilizosaidia kwa kiasi kikubwa udhibiti wa magonjwa mbalimbali nchini.

Tangu ilipoanzishwa hapa nchini mwaka 2014, miongoni mwa magonjwa yaliyofanyiwa utafiti ni kipindupindu mwaka 2015–2020 na mafua ya ndege (avian influenza) yaliyotokea mkoani Arusha.

“Magonjwa mengine ni kimeta (anthrax), surua (measles) na ugonjwa unaotikisa dunia kwa sasa wa covid-19 pamoja na matukio mengine,” anabainisha Ally Hussen mtaalamu wa Epidemiolojia. Anasema pia wameshiriki katika uchunguzi na kushughulikia magonjwa ya milipuko katika nchi zingine kama vile mlipuko wa ebola uliotokea Afrika Magharibi.

“Hata katika nchi jirani ya Congo wakati ilipopata mlipuko wa ugonjwa wa ebola tulishiriki,” anaeleza Dk Hussen. Anasema majanga waliyoshiriki kwa kutoa misaada ya kibinadamu ni mafuriko yaliyotokea wilayani Mvomero mkoani Morogoro, wilayani Kahama mkoani Shinyanga na ongezeko la wakimbizi kutoka Burundi kuingia mkoani Kigoma.

“Tumeshirikiana na ITECH kufanya tathmini ya miaka mitano ya programu ya kupambana na kuzuia saratani ya kizazi nchini iitwayo kwa Kiingereza The National Cervical Cancer Prevention and Control Program.”

Anaongeza: “Nyingine ni kufanya mafunzo juu ya Epidemiolojia ya VVU, ufuatiliaji na uchakataji wa takwimu kwa waratibu wa mkoa wa VVU/ Ukimwi katika Mkoa wa Mwanza, mafunzo juu ya Epidemiolojia katika ngazi ya halmashauri, ushauri kwa wanafunzi (FELTP) na kusaidia maabara kupata ithibati kupitia mradi wa ABBOTT.

TUNAWEZA KUTENGENEZA CHANJO YA CORONA

WATAALAMU wa Epidemiolojia wamesema Tanzania ina uwezo wa kutengeneza chanjo ya Covid-19 kutokana na kuwepo kwa miundombinu na uzoefu. Dk Mwakapeje anasema tayari nchi inakuwa na uwezo wa kutengeneza chanjo ya magonjwa mengine ambayo inakubalika.

Akitolea mfano wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA) kilichopo Morogoro, Dk Mwakapele anasema kiliweza kutengeneza chanjo ya ugonjwa wa newcastro unaoathiri kuku hapa nchini.

“Na chanjo hiyo imethibitishwa na vyombo za kimataifa likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) kwamba chanjo hiyo inafaa na inaweza kutumika. “Lakini pia ukiacha hiyo katika Wizara ya Mifugo wana kiwanda cha kutengeneza chanjo hapa nchini kilichopo Kibaha mkoani Pwani kinachoitwa Tanzania Vaccine Institution kinachotengeneza chanjo ya kimeta, ugonjwa wa kutoka mimba kwa ng’ombe, mbuzi na kondoo lakini pia ugonjwa wa sotoka na magonjwa mengine karibia sita kwa hiyo miundombinu ipo,” anaeleza Dk Mwakapeje.

Dk Ally Husein, mtaalamu wa Epidemiolojia, anasema sababu zingine za Tanzania kuweza kutengeneza chanjo ya Covid-19 ni kwamba mpango wa chanjo wa taifa umekuwa ukifanya vizuri na tathmini ya miaka 10 iliyopita WHO imetambua Tanzania kama ni nchi inayofanya vizuri.

“Kwa hiyo miundombinu tunayo na tukitengeneza tunaweza kusambaza kwenda kila mahali na ndio maana hata za nje zimeweza kusambazwa,” anasema.

Anasema sababu nyingine ni uwepo wa wataalamu waliohusika kufuatilia kirusi hicho kila kinapoibuka kikiwa na mabadiliko. Dk Hussein anasema wamejifunza tabia ya kirusi kutoka mwaka 2003 kilipotokea kwa mara ya kwanza na kilipotokea tena mwaka 2013. Anasema wameendelea kujifunza hata kilipotokea mwaka 2019.

“Huo uzoefu wa kipindi chote unajenga tabia ya uelewa, Tanzania tunaweza kutengeneza chanjo yetu kama vibali vya WHO na vyombo vinavyohusika kutoa kibali watatoa,” anasema Dk Hussein.

“Mfano wakati Covid-19 imekuja nchini tulishiriki kikamilifu kuanza kufuatilia wagonjwa na watu wa karibu wa mgonjwa (contact tracing). Pia tunatoa elimu kwa watu katika maeneo mbalimbali kuhusu magonjwa ya mlipuko.

SERIKALI YAELEZA FAIDA ZA EPIDEMIOLOJIA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima, katika maadhimisho ya Siku ya Epidemiolojia anasema matumizi ya takwimu zenye ubora katika ngazi za chini ili kuweza kufanya maamuzi yenye ushahidi wa kisayansi bado ni changamoto katika halmashauri.

Anasema kuwa mafunzo ya Epidemiolojia yamesaidia sana kuzalisha wataalamu wa Epidemiolojia na maabara kuanzia ngazi ya halmashauri mpaka taifa wenye elimu na weledi wa kutosha ambao wamesaidia kuboresha ubora wa takwimu za afya na kuongeza matumizi ya takwimu katika ngazi zote.

“Kadhalika, upekee wa mafunzo TFELTP hutolewa kwa kuwafundisha pamoja wataalamu wetu wa afya za binadamu na afya za wanyama. “Hii husaidia kubadilishana uzoefu, kuongeza ushirikiano katika utendaji warudipo katika vituo vyao vya kazi na kiujumla huimarisha dhana ya Afya Moja yaani ‘One Health approach’ kuanzia ngazi ya chini kabisa ya utoaji huduma za afya ya binadamu na wanyama,” anaeleza Waziri Gwajima.

Anasema wataalamu hao wanamchango mkubwa wa kutoa elimu ya afya kwa jamii kupitia shule, vituo vya usafiri, viwanja vya ndege na vyombo vya habari juu ya kukabiliana na mlipuko wa Covid-19 ikiwa ni pamoja na kushiriki katika uanzishwaji wa dawati la kupata tahadhari ya ugonjwa huo hapa nchini.

“Wanachama wanashiriki katika kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza kama sehemu ya utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku katika vituo vyao vya kazi ngazi ya taifa, mikoa na wilaya.

“Wanachama wameshiriki kutoa elimu ya afya kwa jamii na matibabu katika kukabiliana na baadhi ya magonjwa ya milipuko kama vile kipindupindu, sumu kuvu, kimeta, tauni na mengine mengi ambapo hadi sasa wameshiriki katika ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya milipuko isiyopungua 100 hapa nchini kwa kushirikiana na wataalamu wa wizara, mikoa na wilaya.

Anasema majukumu mengine ni kushiriki katika uelimishaji wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii, timu za kukabiliana na magonjwa ya milipuko na matukio ya kiafya (rapid response teams) kwa njia ya vitendo (mentorship) katika afua mbalimbali ikiwemo dhana ya afya moja (One Health approach) na mfumo wa ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa hapa nchini (IDSR).

“Hushirikiana na Wizara katika kutathmini utendaji kazi wa mifumo ya utekelezaji wa afua za kiafya hapa nchini kama vile mpango mkakati wa kitaifa wa kudhibiti saratani (Cancer Strategic Plan), pink/red ribbon cervical cancer control program, diseases surveillance systems na mengine.

“Wamesimamia utekelezaji wa mradi wa kufanya maboresho ya maabara za Hospitali ya Taifa Muhimbili pamoja na hospitali za mikoa za rufaa katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Mara, Tanga na Mtwara kwa ufadhili wa shirika la Abbott,” anaeleza Dk Gwajima.

KUTATUA CHANGAMOTO ZAO

Miongoni mwa changamoto zinazowakabili wataalamu wa Epidemiolojia na Maabara hapa nchini ni kutotambulika kwa kada hii kwenye mfumo wa ajira wa serikali. Hivyo basi, Waziri Gwajima anatoa wito kwa idara na taasisi za serikali kwa kushirikiana na wadau wengine ili kutambua umuhimu wa kada hii na iweze kutambuliwa kwenye mfumo wa utumishi wa umma.

“Kwa kufanya hivyo, itasaidia kutoa motisha kwa wataalamu hawa na kupelekea kuongeza ufanisi katika utendaji wao wa kazi. “Naamini kwamba, watendaji na washirika wote wa serikali watakuwa tayari na kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha kuwa mafunzo haya yanakuwa endelevu,”

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/777536e1d91969f6a9c6e756cde6148c.JPG

“TUNALIMA, tunavuna sana kuliko kawaida, unaweza ukajikuta unauza ...

foto
Mwandishi: AVELINE KITOMARY

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi