loader
Dstv Habarileo  Mobile
4,000 kutua onesho la utalii EAC

4,000 kutua onesho la utalii EAC

ONESHO la Kwanza Utalii la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EARTE) litakalofanyika Tanzania Oktoba 9 hadi 16, 2021, litakutanisha wageni zaidi ya 4,000 kutoka ndani na nje ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC); imefahamika.

Katika mazungumzo na HabariLEO Afrika Mashariki mwishoni mwa wiki, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja, alibainisha namna Serikali ya Tanzania ilivyojipanga kutumia fursa hiyo kutangaza utalii wa ndani na nje ya nchi kwa kupata wawekezaji na wadau wa biashara. Alisema wageni hao wanatarajiwa kutembelea maonesho ili kupata taarifa mbalimbali zikiwemo za uwekezaji na kuingia ubia wa kibiashara.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Masanja, zaidi ya kampuni 150 za waoneshaji wa ndani na nje ya Afrika Mashariki, zinatarajia kushiriki maonesho hayo. Aliliambia gazeti hili kuwa, katika maonesho hayo kutakuwa na wanunuzi na waandishi wa habari wa kimataifa zaidi ya 200 kutoka nchi mbalimbali duniani.

Awali akitangaza maonesho hayo, Masanja alisema katika jitihada za kuvutia watalii na kukuza uwekezaji katika sekta ya utalii, Julai, 2021 mawaziri wanaoshughulikia masuala ya wanyamapori na utalii katika nchi za EAC walipitisha Mkakati wa Kutangaza Utalii wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Mwaka 2021-2025.

Alisema miongoni mwa masuala yaliyomo katika mkakati huo ni pamoja na kuanzishwa kwa Onesho la Utalii la Jumuiya ya Afrika Mashariki (East African Regional Tourism Expo – EARTE), litakalokuwa linafanyika kwa mzunguko katika nchi wanachama kila mwaka. “Napenda kuwajulisha kuwa Tanzania ndio itakuwa mwenyeji wa kwanza wa Onesho la Utalii la Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/02a591c17d4b1ad5befba0361baca762.jpeg

WASICHANA waliopata ujauzito katika umri mdogo ...

foto
Mwandishi: Na Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi