loader
SOPHIA BYANAKU  Aliyebuni miradi ya kupigania afya za wanawak

SOPHIA BYANAKU Aliyebuni miradi ya kupigania afya za wanawak

ZIMEKUWEPO juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali na wadau wa afya nchini kuhakikisha afya za Watanzania zinaimarika na hususani afya za wanawake.

Uimarishwaji wa afya za wanawake ni kampeni kubwa hasa ikizingatiwa kuwa wanawake wapo kwenye mazingira hatarishi zaidi kupata magonjwa mbalimbali hasa yale yanayohusishwa na jinsia hiyo.

Sophia Byanaku ni mmoja wa wadau wa afya anayeguswa na afya za Watanzania na hasa wanawake wenzake na anaungana na wadau wengine kupigania afya za wanawake nchini na ili kulitimiza hilo aliamua kuanzisha mradi unaojulikana kama “Women Health Talk”.

Kupitia mradi huu wanawake nchini wanapata wasaha wa kusikiliza, kujifunza na kujadiliana masuala ya afya huku wakipatiwa majibu na suluhisho la matatizo yao.

Sophia akizungumza na gazeti hili anabainisha kuwa mradi wa Women Health Talk umetokana na nia yake ya miaka mingi ya kusaidia wanawake kuwa huru kuzungumzia masuala ya afya kwa ujumla huku akibainisha kuwa ameamua kujikita katika afya za wanawake kwani wana uhitaji zaidi.

Anasema: “Uhitaji wa wanawake katika afya unahusisha zaidi masuala ya saratani, hedhi na mambo mengi ambayo yanatokana na maumbile yetu na hata magonjwa kwa ujumla wake.

“Lakini pia mila na zenyewe zinawafanya baadhi ya wanawake kuwa kwenye kundi kubwa zaidi la uhitaji wa uangalizi maalumu wa afya, hivyo niliamua kuweka mkakati wa kuwafikia wanawake na kuwawezesha katika masuala ya afya lakini pia hata kukabiliana na mila potofu ambazo nyingi zinakuja kuathiri afya za wanawake hao.”

Mradi huo hufanyika mara moja kwa mwaka na huu mwaka umetimiza miaka miwili, ni mradi ambao umetokana na jitihada zake za kuwafikia wanawake ofisini na kuzungumza masuala kadhaa ya maisha na afya.

Sophia ambaye pia ni mwazilishi mwenza wa Hospitali ya Dk Plaza akishirikiana na mumewe Profesa Mohamed Janabi, anasema siku za mwanzo baada ya kuanzisha hospitali hiyo mwaka 2012 alitoa nafasi kwa wanawake kupima afya zao na walipima saratani, kiwango cha mafuta

mwilini, walipima masuala ya uzazi na magonjwa yasiyo ya kuambukiza na majibu yake ndiyo yaliyokuja kuzalisha mradi wa Women Health Talk.

Akizungumzia kuhusiana na mwendelezo wa mradi huo tangu ulivyoanza, Sophia anasema: “Wakati tunaanzisha Dk Plaza mimi na mume wangu niliweka utaratibu wa wanawake kufika hospitalini kupata uelewa kuhusiana na afya ya akili, masuala ya lishe na magonjwa yasiyoambukiza, kati ya wanawake waliofika kupima saratani wanawake watatu walikutwa na saratani ya shingo ya kizazi lakini walikuwa hawajijui.”

Kwa mujibu wa Sophia, hata walipopigiwa simu kuja kuchukua majibu yao walikuwa ni kama wanaona ni kitu cha kawaida na walipofika na kuwaelewesha nini wanaweza kufanya kukabiliana na saratani hiyo, mmoja alipona kwa kuwa haikuwa imemuathiri sana ila wengine walifariki baada ya muda.

Anasema matukio hayo yalifanya afunguke macho zaidi na kuamua kuingia kiundani kuona ni kwa kiasi gani anaweza kusaidia wanawake wengine wengi zaidi kukabiliana na tatizo hilo na ndipo akachukua hatua ya kwenda ofisi mbalimbali kuzun

gumza na wanawake kuhusiana na afya zao lakini wengine akiwafikia kwa njia ya mtandao.

Sophia anasema akiongozana na timu ya madaktari aliweza kuzifikia taasisi na ofisi nyingi za jijini Dar es Salaam na kuzungumza na waajiri ili apewe kibali cha kuzungumza na wafanyakazi wanawake na tangu alipoanza utaratibu huo alibaini pia wanawake wengi wanakabiliwa na changamoto za msongo wa mawazo.

Anasema alipobaini changamoto hiyo alijikuta akiongeza huduma kwenye kampeni yake hiyo na kuanza kujihusisha pia na utoaji wa huduma za ushauri wa masuala ya maisha kwa ujumla.

Sophia anabainisha kuwa kwake shughuli hizo zote mbili kuzifanya haikuwa tatizo kwa kuwa shahada yake ya kwanza kutoka Chuo Kikuu Dar es Salaam aliyotunukiwa mwaka 2005 ilikuwa kuhusiana na masuala ya Sosholojia kabla ya kuja kusomea Shahada ya Uzamili kwenye Utawala, Mipango na Sera kwenye Afya.

Anatoa mfano siku moja wakiwa kwenye ofisi wakiendesha mafunzo ya afya kwa wanawake hao kuna mwanamama ambaye alielezea jinsi alivyoanza kuumwa presha kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kifamilia na kutokana na maelezo hayo, alibaini mwanamama huyo alitakiwa kupewa ushauri wa kisaikolojia kukabiliana na matatizo hayo.

Sophia anabainisha kuwa changamoto kama hiyo aliikuta sehemu nyingi alizotembelea na kupata fursa ya kuzungumza na wanawake na ikampa moyo wa kuendelea kuhusisha elimu ya afya na huduma za ushauri nasaha kwa wanawake, mradi ambao unaendelea hadi sasa huku kila mwaka ukihitimishwa kwa tukio la mwaka la Women Health Talk.

Anasema kuwa bado kuna haja ya wadau kufanya hamasa zaidi kuhusiana na umuhimu wa elimu ya afya kwa wanawake ili wanawake wengi zaidi wajitokeze kupewa elimu ya afya na anabainisha kuwa waliopo maofisini, wako bado baadhi ambao hawajui mwelekeo wa afya zao.

Anazikabili mila potofu Sophia anaamini kuwa wapo wanawake ambao wanakabiliwa na changamoto za afya kutokana na mila potofu walizopitia wakiwa watoto, kama vile ukeketwaji na nyinginezo na hivyo ameamua kuanzisha mradi pia kuwanusuru wasichana ili wasijekujiingiza kwenye matendo ya ngono wakiwa wadogo.

Harakati zake hizo chini ya Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Forward Motion zimeanzia Wilaya za Ko-

rogwe, Muheza na Tanga mjini hasa katika kata 12 na kati ya hizo sita za Maweni na nyingine sita za Pongwe na katika shule zote za kata hizo zimeanzishwa klabu za wanafunzi kujadiliana masuala mbalimbali ya afya ya uzazi.

Anaongeza kuwa wanafunzi wanafundishwa namna ya kukwepa vishawishi, athari za ngono katika umri mdogo, athari za mimba za utotoni huku akibainisha kuwa walimu na viongozi wa kata ni wadau wakubwa wanaoshirikishwa kwenye mradi huo.

Sophia anasema katika baadhi ya maeneo mkoani Tanga kuna mila potofu zinazowavutia watoto kujiingiza kwenye ngono, anatolea mfano wa unyago ambapo wasichana wanafundishwa masuala ya ndoa wakiwa bado wadogo hali inayowavutia kujaribu tendo la ndoa.

“Msichana akifundishwa kuishi na mwanaume akiwa mdogo, unategemea atakuwa na ujasiri wa kukataa akitakwa na mwanaume kimapenzi, sasa hapo ndipo wanaanza ngono katika umri mdogo na ndiyo mwanzo wa saratani ya kizazi, hivyo kama mdau wa afya nimeona nianzie chini kukabiliana na saratani hii kwa kuwaepusha watoto hawa dhidi ya ngono katika umri mdogo kwa kuwapa elimu ya afya,” anasema.

Sophia ni nani?

Mwanadada huyu mwaka 2001 alikuwa mshindi wa Miss Tanga, ni miaka 20 iliyopita lakini bado mwonekano wake ni ule ule pamoja na kuwa mama wa watoto wawili.

Sophia ambaye ni mke wa Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo, Profesa Mohamed Janabi, anasema wamejaliwa watoto wawili mmoja akiwa na miaka 11 na mwingine nane lakini ana watoto wengine wa mumewe mmoja akiwa na miaka 26 na mwingine 19.

Anasema akiwa nyumbani mbali na kufanya shughuli zake za kila siku hupendelea zaidi kutumia muda wake mwingi kuhudumia bustani na yeye ni mpenzi mkubwa wa muziki wa aina zote.

“Mbali na kufanya majukumu yangu nyumbani kama mke, huwa ninapenda sana kujihusisha na bustani kwa maana ya kila kinachohusika na bustani ni changu aisee, lakini mimi bwana napenda muziki kuucheza na kuusikiliza mimi ni mtu wa kazi na pia nina party na marafiki zangu, lakini bila huyu mume wangu nisingekuwa kwenye masuala haya ya afya,” anasema.

Sophia anasema kuwa mwaka 2009 wakati akiolewa na Profesa Janabi alikuwa akifanya kazi Benki ya Stanbic na alikuwa kwenye kitengo cha Ofisa Rasilimali Watu na baada ya kuolewa na Profesa alimshauri kusomea masuala ya afya na mwaka 2010 alianza masomo yake akisomea Tanzania na Norway kisha kuhitimu na kuja na wazo la Dk Plaza ambalo leo linaleta tija katika afya kwa kutibu wengi.

Anasema hospitali hiyo hivi sasa ndiyo ajira yake ya kudumu akihudumu kama Mkurugenzi na inatoa huduma za kibingwa lakini hailazi wagonjwa huku akiwa na mpango wa kufikisha huduma za hospitali hiyo kila kanda ya nchi.

Sophia anasema anakuwa na amani afya za Watanzania zinapoimarika na ndiyo maana kwa kuanzia kwenye hospitali hiyo wanapokea Bima za Afya mbalimbali ikiwemo bima inayotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/26f1ea307cb414568f42a45f27074e31.png

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi