loader
Dstv Habarileo  Mobile
Hakielimu wataka msisitizo elimu jumuishi

Hakielimu wataka msisitizo elimu jumuishi

TANZANIA imeelezwa kuwa kwa kiasi kikubwa imeweka mifumo na sheria anuai kwa lengo la kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu zinazingatiwa katika muktadha na mazingira mbalimbali.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji Shirika la HakiElimu John Kalage katika uzinduzi wa Matokeo ya Utafiti Kuhusu Upatikanaji wa Elimu Jumuishi ya Awali kwa Watoto Wenye Ulemavu nchini.

Matokeo hayo  yanatokana na utafiti uliofanywa na HakiElimu Mwaka 2020 kwa niaba ya Mtandao wa Ujifunzaji Kamili kwa Wote, ambao ulilenga kupata hali halisi ya mazingira ya shule, muktadha wa ujifunzaji na ufundishaji, mifumo ya kitaasisi ambayo inachangia watoto wenye ulemavu kukosa kwenda shule na kushiriki kikamilifu kwenye elimu jumuishi ya awali.

Kalage alisema sera, miongozo na sheria hizo zimeweka bayana ‘Kanuni ya Haki Sawa ya Kupata Elimu kwa Wote’ ambayo inalenga kutoa fursa ya elimu kwa kila mtoto na makundi yote yakiwemo ya wenye ulemavu. 

Hata hivyo, pamoja na kuwa na Sera Mahususi ya Elimu Jumuishi, bado mtaala na muhtasari wa elimu ya awali, pamoja na miongozo inahitaji kusisitiza utoaji wa elimu jumuishi.

Aidha, alisema utafiti huo ambao umefanywa kwenye mikoa 10 ya Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Tabora, Shinyanga, Kagera, Mtwara, Njombe, Kilimanjaro na Tanga kwa kuzingatia haki na sheria zilizopo za kumlinda mtoto, takwimu  zilikusanywa  kupitia maswali na majibu na uchambuzi wa maudhui ya nyaraka rejea husika umeonyesha  kuwa, hali ya uandikishaji kwenye ngazi ya elimu ya awali inabadilika, kama ilivyo uandikishaji kwenye ngazi ya taifa.

“Watoto wenye umri wa miaka mitano wameandikishwa wengi zaidi ikilinganishwa na watoto wenye umri mwingine. Takwimu zinaonyesha kuwa, uandikishaji wa watoto wenye ulemavu wa viungo na afya ya akili ukiongoza kwa miaka yote ikilinganishwa na ulemavu wa kuona ambao ulikuwa wa chini zaidi. Hata hivyo, karibu shule zote hazikuwa na takwimu kamili.” alisema

 Kalage alisema baadhi ya sababu zinazozuia upatikanaji wa elimu ya awali kwa watoto wenye ulemavu zimeonekana kuwa ni unyanyapaa, wazazi/walezi kusita kuwaandikisha shule na kuwaficha nyumbani, umbali wa kutembea kwenda shuleni na kushiriki kwenye shughuli za kijamii.

Pia kwenye ngazi za Taifa ni ukosefu wa bajeti maalum kwa ajili ya watoto wenye ulemavu, uhaba wa wafanyakazi wenye mafunzo ya elimu maalum na ukosefu wa vifaa stahiki vya kujifunza,kufundisha.

“Pamoja na msisitizo uliopo katika elimu jumuishi bado kuna shule mchanganyiko na shule maalum ambazo zinatoa elimu kwa watoto wenye ulemavu.” alisema  

 Aidha alisema Hakielimu wanapendekeza jamii ihamasishwe kuhusu umuhimu wa kusomesha watoto wenye ulemavu, kuacha tamaduni na imani kuwa watoto wenye ulemavu hawana uwezo na  hawastahili kusoma au kujumuika kwenye jamii, sekta ya umma na sekta binafsi washirikiane kuhimiza elimu jumishi ya awali. Serikali na wadau wajikite  kuondoa vikwazo vilivyopo, serikali iandae mwongozo kwa lugha nyepesi kwa ajili ya wadau wote, wakiwemo walimu wa shule/madarasa ya awali, kuwatambua watoto wenye uoni hafifu, viziwi na wenye ulemavu wa akili wakati wa kuandikisha shule.

Mapendekezo mengine ni serikali iandae miongozo na vigezo vya viwango vya chini vinavyotakiwa kuwepo kwenye madarasa ya awali ili kuwasaidia na kuwaongoza walimu kufanya madarasa yao yawe jumuishi zaidi, serikali pamoja na wadau ianzishe vituo shikizi ambavyo vitatoa fursa kwa watoto wenye ulemavu kupata elimu ya awali kwenye shule zilizo karibu na ndani ya jamii zao,  iongeze bajeti na matumizi ya fedha kwenye kuboresha elimu jumuishi ya awali.

Pia wamependekeza njia mojawapo ni kuharakisha utekelezaji wa Rasimu ya Fomula ya Ruzuku ya wanafunzi, ambayo inalenga watoto wenye mahitaji maalum shuleni.

“Serikali iboreshe  mfumo wa ukusanyaji takwimu zinazohusu watoto wenye ulemavu  kwa kuzingatia umri, aina ya ulemavu na jinsi, iwekeze katika kuzalisha na kuajiri walimu waliopitia mafunzo ya elimu maalum.” alisema

Aidha alisema serikali ipitie upya mitaala na  muhutasari  wa elimu ya awali ili kuboresha vipengele vya mitaala vinavyohusiana na viashiria vya ufanisi wa utendaji wa watoto wenye ulemavu wa kuona na viziwi na pia Taasisi ya Elimu Tanzania ifanyie maboresho ya vitabu vya elimu ya awali na vitabu vya hadithi ili kukidhi mahitaji ya watoto wenye ulemavu wa kuona.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/354a6356a3f28c98218a219de73378e4.jpg

WASICHANA waliopata ujauzito katika umri mdogo ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi