loader
Dstv Habarileo  Mobile
Vyama vingi vina upungufu unaoonesha bado vichanga

Vyama vingi vina upungufu unaoonesha bado vichanga

MWAKA 1992, Tanzania ilirejea katika mfumo wa siasa wa vyama vingi na Uchaguzi Mkuu wa Kwanza katika mfumo huo, ulifanyika mwaka 1995.

Katika uchaguzi huo, Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Benjamin Mkapa, aliibuka na ushindi hivyo akawa Rais wa Kwanza Tanzania katika Mfumo wa Vyama Vingi akiwa ni Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akiwa katika Uwanja wa Sabasaba mjini Tarime mkoani Mara akimnadi Mkapa, Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius K, Nyerere, alisema vyama vya upinzani nchini bado vichanga, viachwe vikue vipate mazoea. 

Tangu hapo kila baada ya miaka mitano kumekuwa kukifanyika uchaguzi mkuu nchini ukivishirikisha vyama vingi, lakini CCM kimekuwa kikipewa ridhaa na wananchi.

Nimekumbuka hayo kwani licha ya Tanzania kuwa na idadi kubwa ya vyama vya siasa, vingine ni vikongwe kwenye shughuli za siasa, bado vinakosa ufanisi na uimara na hivyo kuwa changamoto kubwa inayovifanya vishindwe kuendelea hali inayoonesha kuwa, bado vichanga na vinahitaji muda kukua.

Mazingira duni ya ofisi za chama husika kwa maana ya kuwepo kwenye majengo yasiyo na ubora, maeneo duni yasiyo rafiki kwa harakati za kisiasa, vitendea kazi duni na kukosa watendaji wa siku kwa siku katika vyama husika ni mambo yanayoonesha uchanga wa vyama vingi vya upinzani.

Hayo yanabainisha wazi hivi karibuni kutokana na ziara ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika vyama vya siasa nchini kukagua masuala mbalimbali yanahusu ubora na ufanisi wa utendaji kazi wa vyama hivyo.

Timu ya maofisa hao ikiongozwa na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, katika ukaguzi wake imebaini kasoro mbalimbali miongoni mwa vigezo 36 ilivyotumia katika ukaguzi huo.

Katika mazungumzo na HabariLEO, Nyahoza anasema lengo la ziara hiyo ni kuwaelimisha na kuwakumbusha watendaji wa vyama vya siasa nchini mintarafu umuhimu wa kuzingatia matakwa ya sheria ya uendeshwaji wa vyama hivyo ili kuwaepusha kupata hati chafu kutoka kwa Mdhibiti Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Wakiwa katika chama cha siasa cha National League for Democracy (NLD), timu ya watendaji kutoka Ofisi ya Msahili wa Vyama vya Siasa, ilibaini upungufu mwingi uliotokana na majibu ya Katibu Mkuu wa NLD, Tozy Matwanga.

Chama hicho kilibainika kushindwa kwa kiasi kikubwa kukidhi mahitaji husika.

Miongoni mwa mambo yaliyoshangaza timu baada ya kubainika kuwa hayapo katika chama hicho cha siasa, ni pamoja na ukosefu wa baruapepe maarufu e-mail ya chama pamoja na mkataba wa upangishwaji wa makao makuu ya ofisi ya chama hicho.

Nyahoza anasema inashangaza kuwa, katika kipindi hiki ambacho baruapepe ni kitu muhimu kwa kila mtu na taasisi kuwa nacho, eti chama cha siasa hakina.

Kingine kinachoshangaza; ni chama hicho cha siasa kukosa mkataba wa upangishwaji wa eneo zilizopo ofisi za chama hicho.

Anasema: “Yaani inashangaza sana; kwanza ni kwa nini mpo kwenye ofisi ambayo haina mkataba wa pango, vipi kama mkiambiwa kuondoka ghafla au vitu vikifungiwa mtafanyaje, nawapa wiki moja kuhakikisha mnakuwa na mkataba.”

“Kuhusu baruapepe, nataka muifungue haraka …kama hamna baruapepe, mtawasiliana vipi na wadau wakiwemo Ofisi ya Msajili?”

“Mnakumbuka wakati Rais Samia Suluhu akipokea Ripoti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC); alitoa mwito kuvitaka vyama kufanyia kazi kiteknolojia, sasa nyie mnakosaje baruapepe!”

Chama hicho pia kilikutwa kikiwa hakina katiba na kanuni za chama zinazoendana na matakwa ya sheria kama uwepo wa sera.

Kimsingi, uhakika wa sifa za viongozi wa kitaifa wa chama na uhai wa uongozi wa chama kitaifa ni miongoni mwa mambo yaliyoonekana kuwa na dosari.

Katibu Mkuu wa NLD, Tozi Matwanga, anabainisha ukosefu wa vyanzo sahihi vya mapato na kwamba ndio sababu ya kukosekana kwa ufanisi wa chama chake.

Anajitetea akisema: ”Kwa kweli najua hata hizi wiki moja siku mbili mlizotupa kuwasilisha baadhi ya nyaraka, itakuwa ngumu kupata kwa kuwa hatuna hata fedha za kufuatilia na pia ifahamike kuwa, tumepitia kwenye changamoto ya mvutano kati yetu na wanachama wa upande wa Zanzibar sasa mambo yalichanganyika.”

Ofisi ya Msajili katika ukaguzi wake huo ilivipa vyama viwili vya siasa vya NRA na AAFP wiki mbili kuwasilisha majina na picha za viongozi wake waliopo katika wilaya na mikoa yote nchini huku vikitakiwa kuwa na mfumo mzuri unaoonesha mapato na matumizi ya fedha.

Ikiwa katika ofisi za chama NRA ilibainisha kukosekana kwa picha za watendaji wa chama hicho kwa ngazi za mikoa na wilaya hatua iliyosababisha kusitishwa kwa ukaguzi na kuwataka kufanikisha kwanza uwepo wa nyaraka hizo muhimu. 

Aidha, chama hicho cha NRA kimetakiwa kutafuta ofisi yenye hadhi ya kuwa makao makuu ya chama cha siasa na kuondoka mahala kilipo kwa sasa eneo la Temeke mkoani Dar es Salaam.

Uchunguzi wa mwandishi umebaini chama hicho kimejishikiza sehemu isiyo na hadhi ya kuwa ofisi.

Nyahoza akaonesha kukerwa na ukosefu wa taarifa za matumizi ya fedha.

“Ninawapa wiki mbili kwanza kuanza na upatikanaji wa taarifa sahihi na picha za viongozi wenu nchi nzima kwa kuwa hizi ni nyaraka muhimu muwe nazo, lakini hili la kuwa na ofisi yenye hadhi nalo mlifanyie kazi pamoja na kuwa na taarifa za mapato na matumizi ya fedha,” anasema Nyahoza.  

Naye Naibu Katibu Mkuu wa NRA, Abdul Kakulwa, anasema sababu ya kukosa baadhi ya nyaraka muhimu za watendaji wake ni pamoja na chama hicho kuwa hakijafanya mkutano wake wa mwaka kwa muda mrefu.

Anasema hali hiyo imechangiwa na mambo kadhaa ukiwemo mlipuko wa Covid-19.

Kakulwa anasema, changamoto kubwa iliyopo kwa baadhi ya watendaji wa chama katika wilaya na mikoa ni kutokuwa na simujanja ambazo zingesaidia kujipiga picha na kuziwasilisha kwa wakati katika ofisi za NRA makao makuu.

Anasema hata hivyo wanaendelea na mchakato wa kuwahimiza watendaji hao kutafuta njia nyingine za kutuma picha hizo.

Katika ofisi za chama cha AAFP zilizopo Tandika wilayani Temeke, Nyahoza anasema walau huko hakuna shida sana kwani walau ipo katika hali nzuri ukilinganisha na ile ya NRA.

Hata hivyo, nao anawataka waimarishe mifumo yao ya taarifa za fedha pamoja na kuwa na taarifa sahihi za viongozi.

Kwa upande wa chama cha ADC, Ofisi hiyo ilipongeza ufanisi katika utunzaji wa kumbukumbu za wanachama nchi nzima.

Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, anasema kamati ya ukaguzi huo imebaini uwepo wa utunzaji makini wa taarifa katika chama hicho kwa kuwa zinatunzwa katika kompyuta.

Akasema hali hiyo inasaidia upatikanaji wa nyaraka mbalimbali za chama kwa urahisi zinapohitajika.

Anakipongeza chama hicho kwa kuwa na picha na taarifa za wanachama wake wote nchi nzima zilizohifadhiwa katika kompyuta.

Anasema: “Ukaguzi umekutana na kasoro nyingi katika vyama hasa changamoto za utunzaji wa taarifa za fedha na nyaraka, lakini kwa upande wa ADC hakika utunzaji wao wa nyaraka ni mzuri na tena tunavutiwa na umakini huo ingawa katika utunzaji wa taarifa kuhusu fedha, changamoto ipo kama vyama vingine.”

Anasema kati ya vyama sita vilivyokaguliwa, imebainika kutokuwapo mifumo mizuri inayoonesha mapato na matumizi ya fedha.

Kwa msingi huo anasema vyama vinashindwa kutunza fedha za michango ya wanachama na kwamba vipo vinavyotumia fedha zake bila kuonesha uhalali wa matumizi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/f52a4ff089561f7d5b88f6367a2788d4.JPG

MAZAO mengi ya chakula, matunda na biashara kama ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo 

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi