loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mkakati mpya wa miaka mitano utakavyoimarisha kaguzi NAOT

Mkakati mpya wa miaka mitano utakavyoimarisha kaguzi NAOT

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi pekee yenye jukumu la kufanya ukaguzi wa mapato na matumizi ya Serikali, kama yanavyoidhinishwa na Bunge na kutoa taarifa Bungeni. 

Ofisi hii inaongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Ipo tangu kipindi cha Ukoloni na baada ya uhuru na kufikia Julai, mwaka huu imeadhimisha miaka 60.

Mchumi katika ofisi hiyo, Emanuel Philipo, anaeleza jukumu lake ni kukagua hesabu za wizara, mikoa, halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji, Ofisi za Balozi za Tanzania zilizoko nje ya nchi, wakala za serikali, mashirika ya umma, pamoja na miradi ya maendeleo inayogharamiwa na wafadhili.

Pia, kutoa taarifa ya ukaguzi huo Bungeni kuhusu mapato na matumizi ya fedha za umma, kujenga, kukuza na kuimarisha utamaduni wa uwajibikaji katika Wizara na Taasisi za Serikali, Mikoa na Halmashauri; 

Philipo anasema Ofisi inatakiwa kuhakikisha kwamba, inajiridhisha kuwa upo uwajibikaji wa kutosha katika kusimamia na kudhibiti ipasavyo ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali kama inavyoidhinishwa na Bunge.

“Kuhakikisha kuwa jamii ya Tanzania inapata faida au tija kutokana na matumizi bora ya fedha za umma, na mali za umma zinahifadhiwa, kutunzwa na kulindwa ipasavyo,” anasema. 

Akizungumza katika warsha maalumu ya waandishi wa habari na wadau wa asasi ya kiraia kujadili toleo maalumu kwa wananchi la ripoti za CAG kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2020.

Anasema katika majukumu ya ofisi hiyo CAG anatakiwa kufanya ukaguzi angalau mara moja kwa mwaka wa fedha na kutoa taarifa kwa rais kisha ripoti hiyo inawasilishwa Bungeni na baada ya kuwasilishwa CAG kuitoa kwa waandishi wa habari na kufanya kuwa mali ya umma. 

Aidha, CAG hufanya ukaguzi ili kuhakikisha kwamba matumizi yote ya taasisi za serikali yanayotoka Mfuko Mkuu wa Hazina yamezingatia sheria na kanuni zilizowekwa na kuwa CAG anafanya ukaguzi wa taasisi zingine zote zinazotumia fedha za umma isipokuwa taasisi hiyo. 

Anataja aina ya kaguzi zinazofanywa na CAG kuwa ni ukaguzi wa hesabu za fedha chini ya serikali kuu, serikali za mitaa, mashirika ya umma na miradi ya maendeleo, ukaguzi wa uzingatiaji wa kanuni, sheria, miongozo na sera, ukaguzi wa ufanisi, wa kiufundi, kiuchunguzi, maalumu na wa mifumo ya Tehama.

Anasema Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imeandaa na kuanza utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka mitano yaani mwaka 2021/22 – 2025/26) kuanzia Julai Mosi, mwaka huu baada ya kukamilika kwa mpango wa miaka mitano uliopita. 

Anasema dira ya mkakati wa miaka hiyo ni kuwa taasisi yenye kuaminika na ya kisasa katika ukaguzi wa umma inayotoa huduma za ukaguzi za viwango vya juu zinazoimarisha imani kwa umma.

“Kutoa huduma za ukaguzi zenye kiwango cha juu kwa njia za kisasa zenye kuimarisha uwajibikaji na uwazi katika usimamizi wa rasilimali za umma” anasema ndiyo dhima yao kuu.

Anaeleza malengo yao ya miaka mitano kuwa pamoja na masuala mengine mtambuka kama kupambana na rushwa na masuala ya Ukimwi wataimarisha masuala ya rasilimali watu na taaluma kwa watumishi, kuimarisha masuala ya usimamizi, utawala na maadili na kuimarisha mawasiliano kati ya ofisi na wadau wake.

Anasema katika miaka mitano wameweka malengo saba na imeandaa shabaha 113 ili kufikia malengo hayo katika kuimarisha huduma za usaidizi kwa watumishi wanaoishi na VVU/Ukimwi na magonjwa yasiyoambukizi.

“Kutoa uelewa kwa watumishi wote juu ya VVU/Ukimwi na magonjwa yasiyoambukizi, kutoa uelewa kwa kamati ya maadili na watumishi wote juu ya mambo ya maadili na kuandaa na kutekeleza mfumo wa kudhibiti uadilifu,” anasema. 

Anasema shabaha ni kufanya kaguzi za hesabu kila mwaka chini ya  serikali kuu, serikali za mitaa, mashirika ya umma na kufanya kaguzi za ufanisi kwa kupanua mawanda ya ukaguzi katika eneo la uchimbaji wa madini, mafuta na gesi na kuimarisha ukaguzi wa kiuchunguzi na kiufundi.

“Kuwajengea uwezo wabunge kuhusu uelewa na tafsiri ya ripoti za ukaguzi za CAG pamoja na majukumu yake,” anaeleza.

Pia kufanya ukaguzi maalum kulingana na mahitaji ya CAG, Takukuru pamoja na wadau wengine pamoja na kuhuisha mifumo inayotumiwa na wakaguzi pamoja na shughuli zote za ofisi kufanyika kwa njia ya mtandao ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi.

Philipo anasema pia kujenga uwezo wa wakaguzi katika ukaguzi wa mifumo yote ya Tehama inayotumiwa katika ukusanyaji wa mapato na matumizi pamoja na ukaguzi wa kiufundi wa miradi ya kimkakati.

“Kuimarisha uwezo wa Wakaguzi katika kufanya ukaguzi wa Kiuchunguzi katika ngazi zote za Serikali, kuwapatia mafunzo Wakaguzi ili wapate ujuzi wa kukagua maeneo yote ya Serikali na hatimaye kupunguza matumizi ya Kampuni Binafsi za Ukaguzi “anasema.

Anasema wameanzisha chuo cha mafunzo ya wakaguzi, maabara ya ukaguzi wa kiuchunguzi na kiufundi na kuwezesha upatikanaji wa vitendeakazi.

Katika miaka hiyo wamedhamiria kutoa uelewa kwa wadau wa ofisi  ikiwemo asasi za kiraia, vyombo vya habari, kujenga majengo ya ofisi katika mikoa minane na kufanya ukarabati wa majengo yaliyopo na kuandaa mwongozo wa namna ya kushirikiana na wadau wa ofisi.

Philipo anasema katika miaka mitano wamepanga kufanya ukaguzi 330 chini ya wizara, idara za serikali zinazojitegemea 245, wakala na taasisi za serikali 170, kaguzi 210 za balozi na Jumuiya za Afrika Mashariki na kaguzi 130 za sekretariati za mikoa.

Pia watakagua miradi ya maendeleo 375 halmashauri 925, mashirika ya umma 960, kaguzi 60 za ufanisi na za kiuchunguzi.

Anasema katika kaguzi za mifumo ya Tehama wanatarajia kufanya 40 za kiufundi katika miradi ya ujenzi wa barabara chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) na Wakala wa Barabara nchini (Tanroads).

Pia kaguzi 100 za uchimbaji wa madini na gesi asilia, kaguzi maalumu kulingana na mahitaji ya CAG, Takukuru pamoja na wadau wengine na kushiriki vikao 925 vya baraza la madiwani.

Kushiriki vikao vya kamati za kudumu za Bunge (PAC, laac & PIC), kufanya mapitio ya mafaili 37,500 ya pensheni ya wastaafu, kufanya kaguzi 15 za ukusanyaji wa mapato.

Anasema kushiriki mikutano ya pamoja ya jumuiya za kikaguzi, kuandaa mipango, sera, mikakati na miongozo inayosimamia utekelezaji wa majukumu ya ofisi na kuimarisha mifumo ya Tehama na kuhuisha mfumo unaotumiwa na wakaguzi katika kufanya kaguzi mbalimbali.

Katika miaka hiyo mitano wameandaa viashiria vya kupima mafanikio 15 kati yake 12 zitapimwa kupitia wadau wa ofisi, vitatu zitapimwa ndani huku imeandaa viashiria vya kupima matokeo 113.

Anasema katika kutekeleza mpango huo kuanzia mwishoni mwa mwaka huu wa fedha wataanza kufanya ukaguzi wa kiufundi na kiuchunguzi kwa kutumia maabara mbili maalumu ili kubaini ubora na thamani ya miradi.

Maabara hizo zitatumika kukagua hatua kwa hatua za miradi kuanzia katika manunuzi ya vifaa mbalimbali mpaka ubora wa mradi bila kubomoa mradi.

Katika mpango mkakati huo wa miaka mitano unaoanza kutekeleza katika mwaka huu wa fedha na kueleza katika mpango huo wameanza kujenga maabara ya kisasa ili kutoa huduma za ukaguzi zenye viwango bora na kisasa.

Anasema maabara hizo mbili zitatumika kupima ubora wa miradi kwa kutumia vifaa maalumu bila kuchimba barabara au kubomoa majenga kufahamu kiwango cha ubora wa miradi hiyo.

Anaeleza kuwa katika maabara ya ukaguzi wa kiufundi kwa sasa wako katika hatua za manunuzi na mkataba tayari umesainiwa kwa ajili ya ujenzi wa maabara hiyo.

Anabainisha kuwa kufikia Septemba 13, mwaka huu wataanza kufunga mashine na vifaa mbalimbali katika maabara hiyo tayari kwa ajili ya kuanza kazi.

"Katika ukaguzi wa kiuchunguzi kwa sasa ujenzi wa maabara uko katika hatua ya manunuzi hivyo kwa kweli tuko kwenye hatua nzuri na kabla ya  mwaka huu wa fedha kuisha tutaanza kutumia maabara hizi," anasema

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/b5c6c7e87af19a55a6ac5d62873fd684.jpg

MAZAO mengi ya chakula, matunda na biashara kama ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi