loader
Dstv Habarileo  Mobile
Samia azungumzia urais mwaka 2025

Samia azungumzia urais mwaka 2025

SASA ndugu zangu, Rais mwanamke tutamweka mwaka 2025. Ndugu zangu, mwaka 2025, tukifanya vitu vyetu vizuri, tukishikamana, tukimweka Rais wetu, tutakutana hapa kwa furaha kubwa sana.”

Hiyo ni kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan katika hotuba yake kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia ambayo nchini yaliandaliwa na Taasisi ya Wanawake ya Ulingo kwa kushirikiana na taasisi zingine za wanawake. Maadhimisho hayo yalifanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.

Rais Samia amesema wanawake wakitimiza wajibu wao vizuri na kushikamana, wataweza kumweka mwanamke mwenzao kuwa rais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Samia aliwaambia wanawake hao kuwa wanawake wa Tanzania bado hawajamweka Rais mwanamke kwa sababu Rais aliyepo ambaye ni yeye amekaa kwenye nafasi hiyo kwa kudra za Mungu na matakwa ya Katiba.

Alisema alichokichangia yeye pamoja na wanawake wengine akiwemo Anna Abdallah na wengine, ni kuweka nguvu hadi mwanamke akawa Makamu wa Rais ambao ndiyo mchango mkubwa walioufanya wanawake.

“Sasa ndugu zangu, Rais mwanamke tutamweka mwaka 2025. Ndugu

zangu, mwaka 2025, tukifanya vitu vyetu vizuri, tukishikamana, tukimweka Rais wetu, tutakutana hapa kwa furaha kubwa sana,” alisema Rais Samia.

Tuzo Katika maadhimisho hayo jana, Rais Samia alipewa tuzo tatu kwa kutambua mchango wake kwa Taifa na wanawake. Tuzo hizo zilitolewa na Ulingo, Chuo Kikuu cha St Joseph na St Joseph Women Group.

Baada ya kupokea tuzo hizo, Rais Samia alisema tuzo hizo siyo zake, bali ni za wanawake wote wa Tanzania ambao kila siku wanatafuta mbinu za kulea familia, wanamka asubuhi kwenda mashambani, kazini na kwenye biashara.

“Ni tuzo za wanawake wajasiriamali ambao kila siku wanabuni miradi ili kuinua vipato na ustawi wa familia zao, vilevile tuzo hii ni ya wanawake majasiri walioingia kwenye siasa na shughuli za kufanya maamuzi katika fani na ngazi mbalimbali, na hivyo kuondoa dhana kwamba shughuli hizo ni kwa ajili ya wanaume peke yao, kwa hiyo ndugu zangu tuzo hii siyo yangu, nimepokea mimi kwa niaba yenu,” alisema Rais Samia.

Uhuru wa Demokrasia Rais Samia alisema demokrasia ni dhana pana iliyobeba tafsiri nyingi, lakini kwa kuzingatia tafsiri iliyokubalika kimataifa, dhana ya demokrasia inahusisha mambo makubwa manne ikiwemo uwepo wa uhuru katika nchi ukiwemo wa kutoa maoni, wa kisiasa, uhuru wa habari, uhuru wa kujiunga na vikundi na aina nyinginezo.

Mambo mengine aliyoyataja kuwemo kwenye dhana ya demokrasia ni kuheshimu haki za binadamu, kuheshimu utawala wa sheria na ushiriki wa wananchi katika kuiweka serikali kupitia uchaguzi huru na wa haki wenye kujumuisha wananchi wote wenye sifa ya kupiga kura pamoja na ugawaji wa rasilimali kwa uwiano.

“Kwa kuzingatia hayo yote, hakuna shaka kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongozwa kwa kufuata misingi ya demokrasia. Ukizungumzia uhuru wa demokrasia, nchi yetu tumepitia katika ngazi tatu za uhuru, tulitoka kwenye uhuru wa kisiasa ambapo mwaka 1961 Tanzania Bara ilikuwa huru, lakini mwaka 1964 Tanzania Zanzibar nayo ikawa huru,” alisema Rais Samia.

Alisema kwenye miaka ya 1980, Taifa lilianza kuufanyia kazi uhuru wa kiuchumi kwa kutoka kwenye uchumi hodhi na kuingia kwenye uchumi wa soko ambao una mambo mengi ukiwemo uchumi wa wanawake.

“Aina ya tatu ya uhuru ni uhuru binafsi, kwenye uhuru binafsi tumepewa haki hiyo kwenye katiba yetu. Lakini katika kuendesha mambo yetu ya nchi, kuna uhuru mwingine umetafsiriwa kikatiba kama uhuru wa kutoa maoni. Tunapozungumzia uhuru wa kutoa maoni Tanzania, tumefanya kazi nzuri na kubwa,” alisema.

Katika hilo, alisema kwa takwimu za hadi Mei mwaka huu, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kuwa na vyombo vingi vya habari yakiwemo magazeti 257, redio 197, televisheni 50 na televisheni mtandao 451 na blogi 122 na kuongeza kuwa zaidi ya asilimia 75 ya vyombo hivyo vinamilikiwa na watu binafsi.

Rais Samia alisema hakuna fomula moja ya demokrasia duniani kote na kwamba utekelezaji wake unazingatia mila, tamaduni, desturi na itikadi za kisiasa ni tofauti.

Kuhusu uhuru wa kujiunga kwenye vikundi, alisema Tanzania ina asasi nyingi za kiraia, vyama vya siasa takribani 20, vyama vya wafanyakazi na vyama vya wanataaluma mbalimbali, hivyo kuna uhuru mkubwa wa kukusanyika.

“…Natambua kuwa kuna changamoto za demokrasia bado zipo nchini, na hii kwa sababu kwanza hakuna taifa duniani ambalo lina ukamilifu wa katika masuala ya demokrasia,” alisema Rais Samia.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/2d579d1491054b751f1889f8bd5d2e69.jpeg

HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi