loader
Aingia katika orodha  ya mawaziri wa ulinzi   wanawake Afrika

Aingia katika orodha ya mawaziri wa ulinzi wanawake Afrika

TUNAWEZA kusema wako watu waliozaliwa na bahati na mmojawapo ni Dk Stergomena Tax.

Jina lake linaweza lisiwe jgeni kwenye masikio ya Watanzania, Afrika na ulimwengu kwa ujumla lakini safari hii mwanamama huyu ameandika historia nyingine katika maisha yake kwa kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa nchini na amekuwa mwanamke wa saba Afrika kushika nafasi hiyo.

Nchi nyingine Afrika zenye mawaziri wanawake wanaoshika nafasi hiyo ya Waziri wa Ulinzi ni pamoja Afrika Kusini Thandi Modise, Essozimna Gnakade(Togo), Angelina Teny(Sudan Kusini), Monica Juma(Kenya), Oppah Muchinguri (Zimbabwe) na Marie-Noelle Koyara(Afrika ya Kati).

Tangu Uhuru, nafasi ya Waziri wa Ulinzi nchini imekuwa ikishikwa na wanaume lakini sasa imeshikwa na mwanamama huyo aliyeteuliwa hivi karibuni kuziba nafasi ya aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Elias Kwandikwa aliyefariki dunia.

Dk Stergomena ambaye alizaliwa mwaka 1960, amejijengea heshima kubwa katika uga wa diplomasia, kwani kabla ya uteuzi huo, alitoka kumaliza muda wake kama Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini ya Afrika (SADC), nafasi aliyoanza kuishikilia tangu mwaka 2013.

Aidha, aliwahi kuwa mtumishi wa serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Aliteuliwa kushika nafasi hiyo mwaka 2008 na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, pia Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango mwaka 2006, akitoka kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Ubora (BRU), katika Mpango wa Uimarishaji wa Maendeleo ya Biashara Tanzania (BEST), chini ya Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji.

Aliwahi pia kufanya kazi katika Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) kama mratibu na mshauri. Kuanzia Mei 1991 mpaka Aprili 2002, alikuwa mfanyakazi wa Wizara ya Fedha, akiwa mhusika mkuu wa usimamizi wa misaada na uratibu (AMC).

Akiwa Wizara ya Fedha, Dk Stergomena alikuwa ofisa wa usimamizi wa fedha kabla ya mwaka 1993, alipokuwa ofisa mkuu wa dawati la Benki ya Dunia.

Mwaka 1995, alikuwa msimamizi mkuu wa dawati la Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Kwa upande wa taaluma, Dk Stergomena ni mhitimu wa Shahada ya Uzamivu (PhD), aliyotunukiwa na Chuo Kikuu cha Tsukuba, Japan akiwa amebobea katika maendeleo ya kimataifa.

Aidha, alisoma Shahada ya Uzamili ya Falsafa ya Maendeleo ya Kimataifa, Chuo Kikuu cha Tsukuba kuanzia Aprili 1995 mpaka Machi 1997.

Shahada ya kwanza aliipata kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia Julai 1987 hadi Machi 1991. Januari 1984, Dk Stergomena alijiunga na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Dodoma, akichukua diploma ya uongozi wa biashara ya kimataifa.

Amehusika pia kwenye utengenezaji wa mipango hai ya maendeleo Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Hivi karibuni Dk Stergomena Tax aliteuliwa kuwa mbunge, uteuzi ulikuja baada ya kumaliza muda wake akiwa Katibu Mtendaji wa SADC nafasi iliyomuwezesha kuteuliwa tena kuwa Waziri wa Ulinzi.

Akizungumzia uteuzi huo, Dk Stergomena anasema anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kuwa mbunge na waziri wa ulinzi na kuahidi kutumikia wadhifa wake.

“Natoa shukrani za dhati kwa Rais Samia kwa kuwa na imani na mimi na kuniteua kuwa waziri na mbunge. Nimeupokea kwa heshima na unyenyekevu mkubwa.

Nitajitahidi kadri niwezavyo kutekeleza majukumu kwa manufaa ya Watanzania ili kazi iendelee,” anasema. Hivi karibuni akihutubia kwa mara ya kwanza kama Rais, katika Mkutano wa 41 wa Wakuu w anchi na Serikali wa SADC, Rais Samia alibainisha kuwa tayari amempangia kazi nyingine atakaporudi nyumbani (Tanzania) ili kuendelea kutumia ujuzi na uzoefu wake mkubwa aliopata na wenye mafanikio katika SADC.

Rais Samia pia akizungumza wakati wa kumuapisha Dk Stergomena alisema, “nimeamua kuvunja taboo ya muda mrefu kwamba Wizara ya Ulinzi akae mwanaume mwenye misuli yake lakini kazi ya Waziri kwenye Wizara ile sio kupiga mizinga wala kubeba bunduki ni kusimammia sera na utawala wa wizara, nikaamua dada yetu Dk Tax nimpeleke huko.”

Aliongeza kuwa, “kipindi chote tukienda SADC, Dk Tax alikuwa ananisimamia vizuri mambo yote ya usalama ndani ya ukanda na alikuwa ana upeo mkubwa katika maeneo ya Afrika Mashariki kwa hiyo kwa uzoefu alioupata katika masuala ya usalama, anakwenda kutusaidia huko, yeye anajua vizuri askari wetu waliopo Msumbiji, DRC Congo na kwa nini wapo huko, mifumo yao na haki zao.”

 

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/3dfb9ff7826910deb8f21f70fe7f4a5d.jpg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi