loader
Dstv Habarileo  Mobile
RC asikitishwa watoto wadogo kuozeshwa, atoa agizo

RC asikitishwa watoto wadogo kuozeshwa, atoa agizo

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Wilbert Ibuge, amewaagiza viongozi wa Wilaya ya Tunduru kukomesha mila potofu inayowafundisha watoto wa kike wenye umri mdogo namna ya kuishi na mume.

Mila hiyo inatajwa kufanywa na baadhi ya wazazi na walezi wilayani humo, inalenga kuwaozesha mapema kwa tamaa ya kupata mahari inayofanywa na baadhi ya wazazi na walezi wilayani humo.

Ibuge alitoa agizo hilo alipotembelea Hospitali ya Misheni Mbesa iliyopo Kata ya Mbesa wilayani Tunduru akiwa katika ziara yake ya kukagua shughuli za maendeleo zinazofanywa na serikali, wadau na wananchi.

Akiwa katika hospitali hiyo kujionea huduma za matibabu zinazotolewa kwa wananchi na kuzungumza na watumishi, mkuu wa mkoa alipewa taarifa kuwa asilimia 32 ya wanawake wajawazito wanaokwenda kujifungua wana umri chini ya miaka 18.

Ibuge alisema viongozi wa Wilaya ya Tunduru wana wajibu wa kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa watoto wa kike kwenda shule badala ya kuwafundisha mila potofu zilizopitwa na wakati.

“Nimefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru hususani Jimbo la Tunduru Kusini na hapa niko Mbesa, hii ni Hospitali ya Misheni Mbesa, nimepata taarifa kuwa asilimia 32 ya wagonjwa hasa wazazi wanaokuja kwa ajili ya kujifungua ni chini ya umri wa miaka 18 imenisikitisha sana,” alisema.

Alisema jambo hilo ni hatari kwani linawaacha watoto kwenye shida kubwa na kuhatarisha maisha yao kwa kujifungua kwa tabu na hata viumbe wanaowaleta duniani.

Ibuge alisema matatizo na shida za maisha wanayopata vijana wao kwa kiwango kikubwa yanasababishwa na wazazi wenyewe, kutokana na kuendelea na imani potofu za kuozesha na kuwaacha watoto wao kupata mimba na kujifungua kabla ya umri unaotakiwa.

“Sasa natoa maagizo na kutoa rai kwa viongozi wote katika Wilaya ya Tunduru na Mkoa wa Ruvuma, tuelimishe wananchi wetu umuhimu wa elimu, tusiwafunze watoto namna ya kuanza kuishi na wanaume wakati umri bado haujafika wa kufunzwa hayo,” alisisitiza Ibuge.

Aliwahimiza wazazi na jamii kupeleka watoto shule kwa kuwa serikali imeanza kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika elimu bure kuanzia ya awali hadi sekondari na katika afya ya jamii.

Alisema Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inayozalisha kwa wingi mazao ya chakula na biashara hivyo alitaka yasaidie watoto wapate stadi za jamii.

Alisema ni vizuri wote kwa pamoja kuwa na mtazamo utakaosaidia watoto waweze kutimiza ndoto na malengo yao. Katibu wa Afya wa Hospitali ya Mbesa, Samson Hingi, alisema kwa sasa wanahudumia zaidi ya wakazi 105,000 kutoka maeneo yanayozunguka hospitali na wagonjwa kutoka wilaya za Namtumbo na Nanyumbu, mkoani Mtwara.

Alisema Hospitali ya Misheni Mbesa ina dira ya kuwa taasisi inayoongoza katika utoaji wa huduma bora za afya katika Wilaya ya Tunduru zenye kuaminika, ukamilifu na ufanisi, kuonesha upendo wa Mungu na huruma kwa wote wenye uhitaji.

Hingi alitaja huduma zinazotolewa na hospitali hiyo kuwa ni za wagonjwa wa nje, kulaza wagonjwa, huduma za kujifungua wanawake, huduma za maabara, upasuaji mkubwa na mdogo.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/5bbd8904a76e444cefdf1d5b111215c6.jpg

CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za ...

foto
Mwandishi: Muhidin Amri, Tunduru

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi