loader
Dstv Habarileo  Mobile
Samia kuhutubia Baraza Kuu la UN

Samia kuhutubia Baraza Kuu la UN

RAIS Samia Suluhu Hassan ameondoka jana kwenda mjini New York nchini Marekani kuhudhuria Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN).

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilisema pia kwamba Septemba 23, mwaka huu Rais Samia anatarajiwa kulihutubia Baraza hilo la UN.

Pamoja na mkutano huo, taarifa inasema kwamba Rais Samia pia atahudhuria mikutano ya kilele ya kujadili masuala ya mabadiliko ya tabianchi, usalama wa chakula na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Aidha, Rais Samia anatarajiwa pia kukutana na wakuu wa nchi nyingine na viongozi wa mashirika ya kimataifa kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na uhusiano baina ya Tanzania na nchi hizo pamoja na mashirika hayo.

Katika hatua nyingine, wadau wa mazingira na wafanyabiashara wameonesha imani na ziara ya Rais Samia nchini Marekani wakisema kuwa mbali na kudumisha uhusiano wa kimataifa pia itasaidia kuifungua zaidi nchi kimataifa.

Tangu kuapishwa, hii ni ziara ya kwanza ya Rais Samia kwenda safari nje ya Bara la Afrika. Gazeti hili limezungumza na wanasiasa, wadau wa mazingira, wafanyabiashara na wanadiplomasia walioeleza kuwa ziara hiyo ina tija na itakuwa yenye mafanikio makubwa kwa nchi.

Katibu Mkuu wa Chama cha Tanzania Labor Party (TLP), Richard Lyimo alibainisha kuwa uamuzi wa Rais Samia kwenda Marekani kuhudhuria Mkutano huo wa 76 wa Baraza la Umoja wa Mataifa unaimarisha zaidi uhusiano wa Tanzania na nchi nyingine hasa ikizingatiwa kuwa kwa muda mrefu hakuna Rais wa Tanzania aliyehudhuria baraza hilo.

Alisema hiyo ni nia nzuri na yenye tija kwa nchi kwa kuwa Tanzania imekuwa ikisifika kwa kuwa na diplomasia nzuri na mataifa karibu yote duniani ambayo viongozi wake wanakutana Marekani na kwamba ziara italeta heshima na ukaribu na mataifa mengine.

Msemaji wa Chama cha ACT Wazalendo, Catherine Masao alibainisha kuwa ziara hiyo inaitangaza Tanzania kimataifa zaidi huku akishauri kuwa inapaswa iendane na maboresho ya demokrasia ndani ya nchi.

Katibu Mkuu wa Chama cha DP, Abdul Mluya alibainisha kuwa ziara hiyo itasaidia pia kutangaza utalii wa Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa hivi karibuni Rais Samia alishiriki kutengeneza makala kwa njia ya filamu inayotangaza utalii wa Tanzania, hivyo kwenda Marekani itasaidia zaidi utalii wa Tanzania kujulikana.

Kwa upande wake, Katibu wa Mtandao wa Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi Tanzania, Marcela Lungu alibainisha kuwa hatua ya Rais Samia kuhudhuria mkutano mkubwa wa Mabadiliko ya Tabianchi inaiweka Tanzania katika nafasi nzuri zaidi kunufaika na miradi ya utunzaji wa mazingira.

Alisema Tanzania ni kati ya nchi zinazotekeleza mikataba kadhaa ya mabadiliko ya tabianchi hivyo ushiriki wa Rais Samia utasaidia Tanzania kushirikishwa kikamilifu katika utekelezwaji miradi mbalimbali ya mazingira, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi inayojihusisha na lishe ya Solelo, Jurita Mongi alisema anaona Rais Samia anaenda kuimarisha sekta ya lishe hasa kwa ushiriki wake kwenye mijadala inayohusiana na sekta ya lishe ambayo imeanza kupiga hatua kubwa hapa nchini.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/df4b807a57b0c08faf5c74fdd6203670.jpg

CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi