loader
Dstv Habarileo  Mobile
Shahidi kesi ya Sabaya adai  TRA ndio huunda kikosi kazi

Shahidi kesi ya Sabaya adai TRA ndio huunda kikosi kazi

SHAHIDI wa pili katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya (34) na wenzake sita, jana ameieleza mahakama kuwa mwenye mamlaka ya kuunda kikosi kazi maalumu cha kufuatilia masuala ya kodi ni Kamishina wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Akakasisitiza kwamba mkuu wa wilaya hahusiki na masuala ya kodi wala kikosi kazi hicho kwa mujibu wa taratibu. Sabaya na wenzake wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, kuongoza genge la uhalifu, utakatishaji fedha haramu na kuomba rushwa ya Sh milioni 90.

Shahidi huyo, Kayobya Majogolo (41) ambaye ni Kaimu Menaja wa TRA, mkoani Arusha alisema kikosi kazi hicho lazima kiripoti ofisi ya mkuu wa TRA mkoa wa Arusha kwa kujitambulisha na pili kujisajili katika kitabu cha wageni kilichopo ofisini.

Alidai kuwa Januari 22, mwaka huu hakukuwa na kikosi kazi maalumu cha TRA kilichokuja mkoani Arusha kutoka makao makuu au sehemu yoyote kwani nyaraka za kiofisi (kumbukumbu) hazioneshi hivyo na kama ingekuwepo yeye angeona katika kumbukumbu hizo hata kama hakuwepo Arusha.

Alidai kwanza kikosi kazi maalumu cha TRA Makao Makuu kinachokuwa na wajumbe kutoka ndani ya mamlaka hiyo na nje hakiwezi kuja Arusha kwa muamala mmoja wa kodi bali kwa shughuli nyingi za kikodi.

Akiongozwa na Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa Serikali, Ofmedy Mtenga mbele ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Patricia Kishinda, Majogolo alidai amefanya kazi TRA kwa zaidi ya miaka kumi.

Alidai mfanyabiashara akikutwa na kosa kuna taratibu za kiadhabu kwa kosa alilokutwa nalo ikiwa ni pamoja na kuandikiwa nakala kadhaa za barua.

Alidai Mkuu wa Wilaya ni Mwenyekiti wa Baraza la Kodi la Wilaya na Katibu wake ni Meneja wa TRA Wilaya na kwamba kazi ya Mkuu wa Wilaya ni kuhamashisha na kutoa elimu kwa wafanyabiashara juu ya ulipaji kodi na sio vinginevyo kwani shughuli nyingine hazimhusu.

Akihojiwa na wakili wa utetezi, Mosses Mahuna anayemtetea mshitakiwa wa kwanza na wa pili, alidai kuwa vishoka ni watu wasiosajiliwa na TRA ila wanawasaidia wafanyabiashara masuala ya kodi.

Shahidi aliulizwa kama anamfahamu Francis Mrosso, mfanyabiashara mkazi wa Kwa Mrombo akadai hawezi kuwajua wafanyabiashara zaidi ya 33,000 waliosajiliwa na TRA Arusha ila angepata namba ya usajili wa mlipa kodi angeweza kufahamu kwa kumwangalia katika mifumo ya kiofisi.

Kesi hiyo imehairishwa hadi Septemba 30 mwaka huu. Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Enock Mnkeni (41), Watson Mwahomange (27), John Aweyo, Syliverster Nyengu (26), Jackson Macha (29) na Nathan Msuya(31)

foto
Mwandishi: John Mhala, Arusha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi