loader
STELLA: Shujaa wa saratani aliyeshinda hofu  tiba ya mionzi, atoa elimu vijijini

STELLA: Shujaa wa saratani aliyeshinda hofu tiba ya mionzi, atoa elimu vijijini

“ NILIPOKWENDA hospitali tatu tofauti madaktari waliniambia kinachonisumbua ni vidonda vya tumbo wakanipa dawa nitumie lakini sikupata nafuu hivyo ikanifanya niendelee kutafuta sababu za kupata damu kwenye haja kubwa.

“Lakini siku nilipogundulika kuwa na saratani ya utumbo mpana nilipata msongo wa mawazo kwani watu walisema sintapona na pia nilikuwa na wasiwasi mkubwa wa tiba mionzi,” anasema Stella Herman (32), mkazi wa Mkoa wa Geita.

Stella ni miongoni mwa wagonjwa waliopata saratani ya utumbo mpana na kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) zote za Dar es Salaam.

“Nafurahi sana kwani kwasasa nimepona, haikutarajiwa, najiona shujaa katika hili kwani afya si suala la mchezo na huo ugonjwa ukiusikia kwa watu unakata tamaa kabisa.

“Nawashukuru mama yangu na wafanyakazi wenzangu ambao wamekuwa wakinitia moyo kwa kuniambia kuwa naweza kupona na nikaendelea na maisha yangu.

“Sasa nimerejea katika shughuli zangu kama kawaida ingawa bado nakwenda hospitali kucheki afya yangu ni faraja na si kwangu tu na kwa watu wengine.

“Nawashauri watu wanapoona dalili wasikimbilie kusema ni uchawi au ushirikina, wawahi hospitali wapate matibabu ya haraka kwani ningechelewa tu ugonjwa huo usingepona,” anaeleza Stella akiwa na furaha baada ya kupona na kuendelea na kazi zake.

SAFARI YAKE ILIANZIA HAPA

Stella ni Mwalimu wa Kiingereza wa Shule ya Sekondari Ruzewe, Bukombe. Anasimulia madhila aliyokutana nayo kabla ya kugundulika kuwa na ugonjwa wa saratani na kupata matibabu.

Alikuwa anaumwa vidonda vya tumbo tangu mwaka 2011 lakini mwaka 2019 alipata mabadiliko ya kutokwa damu kwenye haja kubwa yaliyompa wasiwasi mkubwa.

“Mwaka huo mwishoni nikaona damu inazidi kuongezeka kwenye haja kubwa nikawa najisikia kuumwa nikaenda kwenye hospitali moja (hakutaka kuitaja jina) ndipo waliponipima na wakaniambia ni madhara ya vidonda vya tumbo.

“Nilifikiria sana hili tatizo la damu kwenye haja kubwa linatokana na nini kwani kama ni vidonda vya tumbo nilikuwa navyo siku nyingi lakini niliendelea kumwamini daktari.

“Nilipewa dawa nitumie lakini sikupata nafuu ikabidi niende tena kwenye hospitali binafsi na baadaye Hospitali ya Mkoa ambapo na huko wakaniambia tatizo lile lile la mwanzo na dawa nikapewa lakini hali haikubadilika.

“Ndugu zangu na watu walionizunguka waliniambia nimerogwa, wakanishauri niende kwa waganga wa kienyeji kupata matibabu baada ya kutumia dawa za hospitalini na kutopona.

“Na hii pia ni baada ya madaktari kushindwa kugundua nini kinanisumbua kwani hawakujua kuhusu ugonjwa wa saratani, hivyo moja kwa moja watu wakapeleka kwenye imani za kishirikina,” anasema Stella.

Anaongeza: “Sikukubaliana nao nikasema ni lazima nitafute hela nikafanye vipimo vikubwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando ambapo huko waliponipima nikagundulika kuwa nina uvimbe na hawakuweza kutoa nyama na kupima.”

Stella anaeleza kuwa kutokana na hali hiyo alitamani kupata vipimo ambavyo vingeweza kusaidia kujua uvimbe huo ni nini hasa.

ALICHOKIAMUA

Stella anasema hakutamani kuwa na muda wa kupoteza kwani siku chache baadae kupitia mtandao wa whatsapp kwenye group kulikuwa na mafundisho kuhusu saratani ambayo yalikuwa yanaeleza dalili za saratani ikiwemo ya utumbo mpana huku akitaja dalili mojawapo kuwa ni choo kuwa na damu bila kuwa na maumivu.

“Nakumbuka daktari bingwa alikuwa akifundisha na hapo hapo nikaanza kujisema huenda kinachonisumbua ni saratani hivyo nikiendelea kuchelewa ninaweza nisipone kama alivyoeleza daktari yule.

“Siku iliyofuata nikaenda kazini na kuonana na mkuu wa shule ili kumuomba ruhusu ya kwenda kutafuta matibabu zaidi lakini hakutaka nikaona ni bora niende halmashauri ambapo huko nilifanikiwa kupata ruhusa na kuanza safari ya kwenda Muhimbili (MNH) kufanya vipimo zaidi,” anaeleza.

NDUGU ZANGU WALIKATA TAMAA

Kwa mujibu wa Stella baada ya kufika Hospitali ya Muhimbili akafanyiwa vipimo na kutolewa nyama sehemu yenye uvimbe. “Majibu yalitoka nikaambiwa kuwa nina saratani ya utumbo mpana katika hatua ya pili.

Baada ya kumpa mama yangu taarifa hiyo alilia sana kwa kile alichoamini kuwa sitakuwa naye muda si mrefu na ndugu zangu pia walihisi kunipoteza kutokana na kuamini kuwa ugonjwa huo hautibiki,” anasema.

“Sauti ya daktari kuwa nimewahi kutokana na hatua ya ugonjwa niliyokuwa nayo ilinitia moyo ingawa ndugu walikata tamaa, aniambia nitapona kabisa baada ya matibabu.

“Aprili 30, 2020 nilifanyiwa upasuaji ambao ulihusisha kuondoa sehemu yenye uvimbe lakini nikapata tatizo jingine la ugonjwa wa fistula ambapo ilinibidi nifanyiwe upasuaji mwingine na kurudi katika hali yangu ya awali.

WASIWASI MATIBABU YA TIBA MIONZI

Taarifa mbaya kuhusu tiba ya mionzi ilimpa wasiwasi Stella. Si yeye tu hata ndugu zake waliipinga tiba hiyo kwa kuhofikia kumpoteza.

“Licha ya wasiwasi niliamua kujitoa kufa kama hiyo tiba inaua muhimu kwangu ilikuwa nipone tu na niliendelea kumuomba Mungu aniondolee wasiwasi niliokuwa nao.

“Nilianza kupatiwa matibabu ya mionzi kule Ocean Road, niliamini kuwa kifo ni cha Mungu lakini kabla ya kupata huduma hiyo pia nilisoma mambo mengi kuhusu tiba mionzi.

“Lakini hapo hapo nilikutana na watu wengi tu hapo Ocean Road wananiambia hawataki kufanya tiba hiyo kutokana na kuogopa kufa kwani inaua seli za mwili.

Stella anasema tiba mionzi ndiyo iliyomsaidia hali yake kuimarika na sasa kuendelea na majukumu yake.

SASA MIMI NI BALOZI WA SARATANI

Ni mwaka mmoja sasa umepita na miezi kadhaa tangu Stella apate matibabu ya saratani na hali yake imeendelea kuimarika.

Anasema licha ya kuendelea kuhudhuria kliniki na kufuata maelekezo ya daktari anaendelea na kazi yake ya ualimu.

“Nimekuwa mwalimu zaidi wa kile nilichokuwa nafanya mwanzo naweza kusema nimekuwa mwalimu wa saratani kwa kuwafundisha watu wengine kuhusu ugonjwa huo na tiba ya mionzi huko Geita.

“Si mwalimu tu lakini pia najitolea kuwa balozi wa saratani na nawaelimisha watu kuwa ukiwahi ugonjwa huo unatibika na tiba mionzi ni salama.

Lakini pia ninawafundisha kuhusu ugonjwa huo na dalili zake ili kuokoa jamii yangu na ninafuraha kubwa sana leo kusimama na kuwafundisha wengine, namshukuru Mungu.”

Stella anaishauri serikali kuwa wahudumu wa afya vijijini wapewe elimu kuhusu saratani ili wawasaidie watu kwa haraka.

UTAFITI TIBA MIONZI

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), umeonesha kuwa asilimia 72 ya wananchi hawana uelewa kuhusu vipimo na tiba ya mionzi huku asilimia 64 ya wagonjwa wakipata huduma hiyo kwa kuwaamini madaktari.

Utafiti huo uliofanyika katika mikoa mitano nchini ukihusisha watu 30 kwa kila mkoa, pia ulibaini asilimia 54 ya madaktari wa ngazi zote walikuwa na ufahamu kuhusu vipimo na tiba mionzi.

Ulikuwa unaangalia ufahamu na uelewa wa jamii kuhusu mionzi inayotumika katika uchunguzi wa magonjwa na tiba kwa Tanzania na ulifanyika Dar es Salaam, Kilimajaro, Mwanza, Mbeya na Ruvuma.

“Katika kila mkoa kulikuwa na washiriki 30 ikiwa 10 ni wagonjwa ambao waliandikiwa kufanya vipimo vya X-ray au matibabu yanayohusisha mionzi, 10 madaktari na 10 wananchi ambao hawajawahi kuandikiwa kufanya vipimo vinavyohusiana na mionzi.

“Matokeo ya utafiti huo yalionesha kwamba asilimia 72 ya watu ambao hawakuandikiwa vipimo hivyo walikuwa na ufahamu mdogo wa mambo ya mionzi, asilimia 64 ya wagonjwa walikuwa na ufahamu mdogo, lakini asilimia 54 tu ya madaktari katika ngazi zote kuanzia ‘clinical officer’ na ‘specialist’ walikuwa na ufahamu wa mambo ya mionzi,” unaeleza sehemu ya utafiti huo.

TIBA MIONZI NI SALAMA

Daktari Bingwa wa Ugonjwa wa Saratani, Hellen Makwani, anasema kuwa tiba mionzi ni salama na yenye kuaminika zaidi kwa wagonjwa wa saratani.

“Napenda kuwaambia kuwa wasiogope tiba mionzi ni tiba salama na yenye kuvumilika hasa kwa teknolojia ya kisasa ya mashine za kisasa aina ya Linear accelerator ambayo husaidia kutibu kwa kiwango cha juu.

“Pia tiba hii inatumiwa na dunia nzima na imethibitika kuwa salama na yenye matokeo mazuri, elimu zaidi inatakiwa ili jamii iondoe hofu pamoja na imani potofu juu ya tiba mionzi,” anashauri Dk Makwani.

HALI YA SARATANI NCHINI

Takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zilizotolewa mwaka 2021, zinaonesha kuwa kuna ongezeko la wagonjwa wapya wa saratani wapatao 50,000 na inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030 kutakuwa na ongezeko la asilimia 50 ya wagonjwa wapya wa saratani.

Aidha, takwimu za mwaka 2018 zinaonesha kuwa hapa nchini idadi ya wagonjwa wapya wa saratani ni 14,028 sawa na asilimia 33.3 ya wagonjwa wote nchini.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/b719c7394652e638e6b1d7449f9e83b0.jpg

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: Eveline Kitomari

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi