loader
Dstv Habarileo  Mobile
Ligi yaanza na utamu

Ligi yaanza na utamu

LIGI Kuu Tanzania Bara imeanza kushika kasi huku kila timu ikiwa imeshuka uwanjani mara mbili.

Wakati ligi hiyo kwa sasa ikiwa imesimama kupisha michezo ya timu za taifa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar, Polisi Tanzania iko kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi sita sawa na Yanga inayoshika nafasi ya pili, huku Namungo ikishika nafasi ya tatu na Mbeya Kwanza waikamilisha orodha ya timu nne zilizo juu katika msimamo huo.

Hadi sasa jumla ya mabao 41 yamefungwa, huku Polisi Tanzania ikiwa ndio timu iliyofunga mabao mengi ikiwa imeweka kimiani mabao manne na kufungwa moja, wakifuatiwa na Mbeya City na Mbeya Kwanza ambao kila moja amefunga mabao matatu na kufungwa mawili.

Vita ya kuwania kiatu cha ufungaji nayo imeanza kushika kasi, nyota wa Polisi Tanzania, Vitalis Mayanga yuko  kileleni akiwa na mabao mawili sawa na Reliants Lusajo wa Namungo ambaye naye amefunga mara mbili wakati mfungaji bora wa msimu  uliopita John Bocco hajafunga bao katika michezo miwili ambayo timu yake imecheza.

Hadi sasa ni mchezaji, Anuary Jabir  ndiye pekee aliyeoneshwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kiwiko Kennedy Juma katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya Dodoma Jiji na Simba ambao Wekundu wa Msimbazi walishinda kwa bao 1-0.

Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama  kwa majuma mawili hadi Oktoba 16 kupisha kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa) kuziwezesha timu za taifa zinazotafuta nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar.

MAKOCHA WANENA

Kocha wa Polisi Tanzania, Malale Hamsini alisema amefurahishwa na kiwango kilichooneshwa na vijana wake kwa kufuata maelekezo na kuongoza Ligi na kuongeza kuwa atatumia mapumziko hayo kuendelea kukiimarisha  kikosi chake ili watakaporejea waendeleze walipoishia.

“Tumekuwa na matokeo mazuri katika michezo miwili ya kwanza, hii inatokana na wachezaji wangu  kufuata maelekezo katika uwanja wa mazoezi, naamini tutakuwa na muendelezo huu pindi timu itakaporejea baada ya kalenda ya Fifa,” alisema Hamsini.

Kocha Mkuu wa Yanga, Nassredine Nabi alisema huu ni mwanzo mzuri kwa kikosi chake, kwani malengo yao msimu huu ni kutwaa mataji yote ya ndani na tayari wameanza na Ngao ya Jamii, kinachofuata ni Ligi Kuu ndio maana wameamua kuwekeza nguvu kubwa huko.

“Malengo yetu msimu huu ni kushinda kila kombe tutakaloshiriki ili kurudhisha heshima yetu, tunaenda mkoani Arusha kuweka kambi ambayo tutaitumia kurekebisha baadhi ya makosa yaliyojitokeza katika baadhi ya maeneo pamoja na kutengeneza muunganiko katika kikosi chetu.”

“Bado hatujawa na muunganiko ninaouhitaji, kikosi kina wachezaji wapya ambao wameingia moja kwa moja kwenye timu hivyo nahitaji muda ili niweze kupata pacha nzuri,” alisema Nabi.

Kocha Mkuu wa Namungo, Hemed Suleiman (Morocco) alisema kitendo cha kukusanya pointi nne katika michezo miwili sio jambo rahisi kutokana na ugumu wa ligi na kwamba amefurahishwa na ubora ulioonyeshwa na wachezaji wake na anaamini watakaporejea watakuwa bora zaidi.

“Tulikuwa na maandalizi mazuri ndio sababu tumeanza vizuri Ligi Kuu japokuwa kuna baadhi ya makosa yameonekana ambayo narudi katika uwanja wa mazoezi kuyafanyia kazi ili tutakaporudi tuendeleze tulipoishia kwa kuibuka na ushindi,” alisema Morocco.

 

Mshambuliaji kinara katika orodha ya wafungaji, Vitalis Mayanga naye alisema baada ya kutokuwa katika kiwango bora kwa misimu kadhaa, huu ni wakati wake wa kuwania kiatu cha ufungaji bora ambacho kimekuwa kikibebwa na wachezaji wa timu kubwa.

“Imezoeleka kuwa timu kubwa ndizo zimekuwa zikitoa wafungaji bora, kama nitaendelea kuwa mzima bila kupata majeraha naamini msimu huu utakuwa wangu kutwaa kiatu cha ufungaji bora,” alisema.

 

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/aa443391fb516d13e2076a6495d339b7.jpg

MAZAO mengi ya chakula, matunda na biashara kama ...

foto
Mwandishi: Na Martin Mazugwa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi