loader
Sayansi, teknolojia, ubunifu ‘nyundo’ kuleta tija katika muhogo

Sayansi, teknolojia, ubunifu ‘nyundo’ kuleta tija katika muhogo

MUHOGO ni zao muhimu kwa ajili ya chakula na biashara kwani watu zaidi ya milioni 800 duniani wanalitegemea.

Katika Afrika takribani watu milioni 300 wanategemea zao hilo kwa ajili ya chakula na biashara, kutengeneza wanga unaotumika kwenye viwanda vikiwemo vya dawa lakini pia katika utengenezaji wa nishati.

Kwa Tanzania mwaka 2018/19 uzalishaji wa muhogo ulifikia tani milioni 8.2 kwa mwaka katika hekta 990,835 za mihogo zilizolimwa mwaka huo.

Meneja wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Mikocheni jijini Dar es Salaam, Dk Joseph Ndunguru, anasema zao hilo pamoja na kutegemewa kwa chakula na biashara linaathiriwa na magonjwa mawili ambayo ni ugonjwa wa batobato na michirizi ya kahawia.

Dk Ndunguru anasema kutokana na kuwepo kwa magonjwa hayo uzalishaji wa muhogo unakuwa na upotevu mwingi.

Hivyo ili kutatua upotevu huo matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu yamewezesha kubaini virusi vya muhogo na kujua aina zipi za mbegu zilizoboreshwa na zitumike kwa ajili ya kudhibiti virusi mbalimbali vya muhogo.

“Batobato hasara yake ni Dola za Marekani kati ya bilioni mbili mpaka tatu kwa mwaka Barani Afrika. Michirizi ya kahawia inasababisha hasara ya Dola za Marekani milioni 35 hadi 70 nchini Tanzania, hii inasababisha mara nyingi wakulima wanaacha kulima muhogo,” anasema.

Anazungumzia mchango wa sayansi ulivyo katika kuanzisha maabara za kupimia magonjwa ya virusi vya muhogo lengo likiwa ni kuhakikisha ni aina zile za mbegu ambazo zimethibitishwa hazina virusi ndio zipelekwe kwa wakulima.

“Kwa mfano tayari ramani imetengenezwa kwa ajili ya kuongoza usambazaji wa mbegu kimkakati, lengo ni kwamba wadau wote wanaohusika na uboreshaji wa zao hili wahakikishe kabla mbegu hazijasambazwa kwa wakulima zichunguzwe kwenye maabara ili kuthibitisha kuwa hazina virusi.

“Maabara zipo TARI Mikocheni, Wakala wa Mbegu (TOSCI) na kwenye baadhi ya maabara za vyuo vikuu,” anasema.

Lengo la kuthibitishwa kwenye maabara hizo ni ili zifanye vizuri na uzalishaji kuongezeka.

Anatolea mfano kwenye mashamba ya mihogo ya Butiama na Rorya Mara, Mbinga mkoani Ruvuma na Mkinga mkoani Tanga.

Anasema katika mashamba hayo baada ya kupata mbegu zilizoboreshwa na kustahimili aina mbalimbali za virusi, uzalishaji uliongezeka kutoka tani tano kwa hekta mpaka kufikia tani 35 kwa wale ambao walipanda mbegu hizo bora.

Kutokana na uzalishaji kuwa juu iliweza kuwaongezea wakulima kipato tofauti na awali.

Mkulima Pamela John kutoka Rorya anasema kutokana na utumiaji huo wa mbegu bora ameweza kujipatia kipato zaidi na pia aliweza kuuza mbegu kwa wakulima wenzake.

Nchini Rwanda, Dk Ndunguru anasema walipoenda huko kufanya utafiti wa zao la mihogo walikuta hali ni mbaya, hivyo kwa kutumia maabara iliyojengwa nchini kwao kwa ajili ya kuhakikisha mbegu zote wanazopata wakulima zinachunguzwa huko, wakati wa mavuno walifanikiwa kupata tani 45 kwa hekta na matokeo yake serikali ya nchi hiyo iliamuru usambazaji wa mbegu hizo kwa 

nchi nzima hali iliyochochea uanzishwaji wa kiwanda cha kuchakata muhogo kilichopo Kanazi Rwanda kilichowekezwa na nchi ya Brazil.

“Nchini Uganda, Kenya, Zambia, Malawi na Msumbiji, mambo yalikuwa ni hivyo hivyo ongezeko la tija katika mihogo baada ya njia za kisayansi kutumika,” anasema.

Anasema sasa matokeo ni makubwa kwa kuwa maabara zilizoanzishwa zilifanyiwa utafiti na wanafunzi.

“Hapa mkulima anaona namna gani sayansi imechangia kuleta mapinduzi ya kilimo chenye tija,” anasema.

Ndunguru anasema mradi huo ulikuwa ni wa miaka 10 wa kujengea nchi uwezo wa kudhibiti magonjwa ya mihogo ambayo ni batobato na michirizi ya kahawia ili kuleta tija.

Mradi huo umeshirikisha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Malawi, Zambia na Msumbiji, uliisha mwaka 2018.

Hakuna shaka kuwa mchango wa sayansi, teknolojia na ubunifu unazaa matunda katika kuleta tija kwenye zao la muhogo na mazao mengine ukitumika kwa ufasaha.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/79fcf90334874a6d73d494665831b773.png

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi