loader
Dstv Habarileo  Mobile
Ummy aanika mgawo wa bil 536/- Tamisemi

Ummy aanika mgawo wa bil 536/- Tamisemi

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu ametoa mgawanyo wa mgawo wa fedha Sh bilioni 535.6 kati ya Sh trilioni 1.3 ambazo serikali imepokea kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya kupambana na athari za ugonjwa wa Covid-19.

Katika hilo, amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha madarasa 12,000 ya sekondari na 3,000 ya vituo shikizi yanakamilika kabla ya Desemba 15, mwaka huu, ili wanafunzi wote watakaoanza masomo Januari wasikose madarasa wala viti vya kukalia.

“Ofisi ya Rais – Tamisemi imeidhinishiwa kupokea jumla ya shilingi bilioni 535.68 kati ya fedha zote zilizotolewa kwenye mkopo huo wa masharti nafuu ambayo ni sawa na asilimia 41.1. 

“Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 304 ni kwa ajili ya elimu msingi, shilingi bilioni 226.68 ni kwa ajili ya afya ya msingi na shilingi bilioni 5.00 ni kwa ajili ya kuboresha miundombinu na mazingira ya kufanyia biashara kwa wafanyabiashara wadogo,” Ummy aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dodoma.

Akifafanua, aliwataka wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha miradi ya ujenzi wa madarasa inakamilika kabla au ifikapo Desemba 15, mwaka huu na miradi mingine ikamilike kabla au ifakapo Aprili 30, mwakani.

Alisema katika kutekeleza miradi hizo, halmashauri zinaweza kutumia wakandarasi wa ndani au utaratibu wa “force account” na kusisitiza kuwa gharama za utekelezaji kwa kutumia njia yoyote zisizidi makadirio ya fedha zilizotengwa kwa shughuli husika

“Nitumie nafasi hii kuwaelekeza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini waendelee na ujenzi wa madarasa hususani kwa shule za msingi na kukamilisha ununuzi wa viti, meza pamoja na madawati katika vyumba vya madarasa ya zamani ili kujenga mazingira bora ya ufundishaji na ujifunzaji kwa watoto wetu nchini,” alieleza Ummy.

Aidha, alisema idara ya elimumsingi imepokea kiasi cha Sh bilioni 304 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika elimumsingi ikiwemo vyumba vya madarasa na mabweni. 

Alisema katika eneo hili, serikali imepanga kujenga vyumba vya madarasa 12,000 vitakavyogharimu Sh bilioni 240 katika shule za sekondari katika halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya kujiandaa kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza watakaojiunga Januari mwakani.

“Ujenzi wa idadi ya vyumba vya madarasa haya unatokana na mahitaji kulingana na idadi ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022. Ukamilishaji wa madarasa 12,000 utawezesha wanafunzi 600,000 kupata vyumba vya kusomea na utaondoa changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa kwa asilimia 100 katika shule za sekondari. Wanafunzi 1,022,936 wanakadiriwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022,” alfafanua.

Alisema gharama za ujenzi wa vyumba vyote vya madarasa zitajumuisha pamoja na ununuzi wa viti na meza 600,000 na kuwa mikoa na halmashauri zote zitanufaika na ujenzi huu kwa kuzingatia, makadirio ya kiwango cha ufaulu, idadi ya wanafunzi wanaotarajia kujiunga na kidato cha kwanza na uhaba wa vyumba vya madarasa uliopo katika kila shule.  

Alisema mikoa itakayopata fedha nyingi zaidi kutokana na wingi wa wanafunzi ni Mwanza itakayopewa Sh bilioni 19.7 zitakazojenga madarasa 985, Dar es Salaam imetengewa Sh bilioni 14.86 za kujenga madarasa 743, Geita Sh bilioni 14.84 za madarasa 742, Kagera Sh bilioni 14.18 za kujengea madarasa 709 na Morogoro imepata mgawo wa Sh bilioni 14.14 za madarasa 707.

Kuhusu vituo shikizi vya shule ya msingi, alisema kupitia mpango huu, serikali itajenga vyumba vya madarasa 3,000 katika vituo shikizi 970 ambazo jumla ya Sh bilioni 60 zitatumika. 

Ujenzi huo utawezesha wanafunzi 135,000 kupata vyumba vya madarasa bora kwa ajili ya ujifunzaji. Ukamilishaji wa vyumba vya madarasa utakwenda sambamba na ununuzi wa madawati 45,000 ambayo yatatumiwa na wanafunzi 135,000 ambapo halmashauri 143 zitafaidika

Alisema mpaka sasa kuna jumla ya vituo shikizi 1,155 katika halmashauri 148 nchini huku halmashauri 36 ambazo idadi kubwa ya halmashauri hizi zipo katika maeneo ya majiji, manispaa na miji hazina vituo shikizi vya shule. 

Alisema mikoa iliyopatiwa fedha nyingi zaidi kutokana na wingi wa wanafunzi waliopo kwenye vituo shikizi ni Singida iliyotengewa Sh bilioni 6.64 ya madarasa 332, Tabora imepewa Sh bilioni 5.3 madarasa 266, Tanga Sh bilioni 4.56 madarasa 228, Katavi Sh bilioni 4.48 madarasa 224 na Dodoma ina mgawo wa Sh bilioni 3.5 kwa madarasa 175.

Alisema kukamilika kwa madarasa 15,000 katika shule za sekondari na vituo shikizi vya shule za msingi utaleta manufaa mengi kwa walimu, wanafunzi na jamii kwa kuondoa mlundikano, hivyo kuepusha uwezekano wa kupata maambukizi ya Covid-19 na kutasaidia vituo shikizi kukidhi vigezo vya kusajiliwa kuwa shule za msingi.

Pia kuwezesha wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba kujiunga kidato cha kwanza kwa awamu moja tu, kupunguza utoro na mdondoko wa wanafunzi, na walimu na wanafunzi watakuwa katika mazingira bora ya ufundishaji na ujifunzaji.

Kuhusu mabweni, Waziri wa Tamisemi alisema serikali imeweka Sh bilioni nne kwa ajili ya ujenzi wa mabweni 50, ambazo kila bweni litagharimu Sh milioni 80. Mabweni hayo yatawezesha wanafunzi 4,000 kupata malazi bora wakati wote wakiwa shuleni wakiwamo wenye mahitaji maalumu.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/a459479e856e88a069790e5d0dcaf665.jpeg

CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi